KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, August 24, 2009

Uskochi yajitetea kumwachia al Megrahi


Serikali ya Uskochi imetetea uamuzi wake wa kumwachilia huru Abdelbaset Ali al-Megrahi, mtu aliyepatikana na hatia ya kulipua ndege ya Pan Am huko Lockerbie, huku ikikosolewa ndani na nje ya nchi.

Hatua hiyo inafuatia kauli kali kutoka kwa mkuu wa shirika la upelelezi la FBI, ambaye alisema kuachiliwa huru kwa Bw al-Megrahi iliwa ni kufanyia mzaha sheria.

Aliyewahi kuwa waziri kiongozi wa Uskochi, Jack McConnell alisema lilikuwa ni kosa kubwa la kiuamuzi.

Lakini waziri kiongozi wa sasa, Alex Salmond alisema kumwachilia huru Megrahi katika misingi ya huruma ulikuwa uamuzi sahihi.

Alisema Scotland ina uhusiano imara na wa kudumu na Marekani, "lakini haitarajiwi kila wakati tuwe tunakubaliana kwa kila jambo."

"Tunatambua kuwa kero. Tunatambua kutokubaliana. Lakini tunatakiwa kufanya kile kilicho sahihi kwa kuzingatia mfumo wetu wa sheria, hilo ndilo jambo tunalowajibika kulifanya," alisema.

Awali rais Barack Obama wa Marekani alisema hatua hiyo ilikuwa ni ''kosa'', na jamaa wa waathirika wa Marekani wamechukizwa na uamuzi huo.

Wengi wa watu 270 waliokufa katika ulipuaji wa ndege hiyo walikuwa ni Wamerekani.

Serikali ya Scotland imesema ilifanya mashauriano ya kina kabla ya Waziri wake wa Sheria, Kenny MacAskill kufanya uamuzi huo, kufuatia maombi ya Megrahi ya kuachiwa kwa sababu za kibinadamu au kuhamishiwa katika gereza la Libya.

Hata hivyo ushauri wa kidaktari ulikuwa unaonyesha kuwa Megrahi anategemewa kuwa amebakiza muda wa miezi mitatu tu kuishi.

Megrahi alipatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia mwezi Januari mwaka 2001 katika kesi iliyoendeshwa chini ya sheria za Scotland nchini Uholanzi.

No comments:

Post a Comment