KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, August 27, 2009

Nigeria kuwakamata zaidi vigogo wa benki


Kikosi maalum cha polisi wa kuzuia ubadhirifu nchini Nigeria kimesema kinajiandaa kawakamata zaidi wafanyabiashara wakubwa walioshindwa kulipa madeni ya mabilioni ya fedha wanayodaiwa katika benki mbalimbali.

Hatua hiyo inafuatia kumalizika kwa muda maalum uliokuwa umewekwa kuhakikisha wale wanaodaiwa wawe wamekwisharudisha fedha hizo kwa benki hizo zinazoelekea kufilisika.

Serikali ililazimika kuokoa benki tano na kuwafukuza kazi viongozi wote wa benki hizo wiki iliyopita katika juhudi za kuzuia benki hizo kuanguka.

Baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu kabisa wa benki hizo wanashikiliwa na polisi, lakini wawili wangali mafichoni.

Maafisa hao wawili wanatafutwa na polisi kuhusiana na tuhuma za wizi wa pesa na ukiukwaji wa maadili ya utoaji mikopo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, kikosi hicho maalum cha polisi pia kinawasaka wadaiwa.

Wiki iliyopita gavana wa benki kuu ya Nigeria aliwaaibisha hadharani baadhi ya matajiri wakubwa barani Afrika akiwataja kwa majina kwa kushindwa kulipa mikopo mikubwa waliokopa kutoka katika benki mabalimbali.

Maafisa wa kuzuia ubadhrifu wanasema baadhi ya fedha hizo zimerejeshwa, lakini kiasi kikubwa bado hakijarejeshwa.

Tarehe ya mwisho kurejesha fedha hizo ilipangwa kuwa Jumanne wiki hii.

Wengi wa wataalamu wa sheria wanasema kuwa deni ni suala ya kesi ya madai na hivyo wamekosoa kisheria uhalali wa kuwakamata wadaiwa.

Lakini mkuu wa kikosi cha polisi cha kuzuia ubadhrifu, Farida Waziri anasisitiza kuwa kuna kesi ya kujibu.

''Tunaweza kuwakamata maafisa hao kwa kula njama pamoja na wafanyakazi wa benki mbalimbali.''

''Baadhi ya mikopo ilitolewa pasipo utaratibu, na baadhi ilitolewa katika mazingira ya udanganyifu,'' amesema

Aliendelea kwa kuzitaka mahakama kutotoa kile alichokiita ,haki ya kuwalinda wadaiwa.

Amesema kuwa anatambua kuwa wadaiwa hao wapo mahali wakifanya mikutano ya siri na wamekuwa na mipango ya kuishitaki serikali.

Hawa ni kundi la watu wenye nguvu na nia moja walio tayari kupambana kulinda maslahi yao binafsi.

Lakini kikosi maalum cha kuzuia ubadhirifu cha Nigeria chenyewe kina utata.

Wanakosolewa kwa kiwango kikubwa nchini Nigeria kwa kupoteza mwelekeo katika vita dhidi ya rushwa kutokana na kusisitiza kwao kwamba, wadaiwa walipe madeni moja kwa moja kwa kikosi hicho kwa njia ya hundi za mamilioni ya dola za kimarekani.

No comments:

Post a Comment