KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, August 27, 2009

BISMILLAHIR RAHMANIR RAHIM 22/08/09




UTANGULIZI:
SIFA ZOTE NJEMA ANASTAHIKI MWENYEZI MUNGU MOLA WA VIUMBE VYOTE. NA REHMA NA AMANI ZIMSHUKIE MTUME WETU MUHAMMAD (S.A.W) NA JAMAA ZAKE NA MASWAHABA WAKE WOTE. NYARAKA HIZI ZIMEKUSANYA HUKUMU ZILIZOKUWA LAZIMA KUZIJUA KWA KILA MFUNGAJI WA MWEZI WA RAMADHANI, ILI MFUNGAJI AWE NA UJUZI KAMILI KATIKA KUTEKELEZA IBADA HII TUKUFU YA SWAUMU YA MWEZI WA RAMADHANI. KWAHIVYO NDUGU MUISLAMU, JITAHIDI SANA KUZISOMA NYARAKA HIZI KWA MAKINI SANA NA UYAELEWE YALIYOMO. NAOMBA MWENYEZI MUNGU ATUFANYIE WEPESI KATIKA KUZIJUA HUKUMU ZA KUFUNGA.

1) HUKUMU YA KUFUNGA
KUFUNGA KATIKA MWEZI WA RAMADHANI NI FARADHI (LAZIMA) KWA KILA MUISLAM ALIYEBALEHE, MWENYE AKILI TIMAMU NA MWENYE KUWAJIBIKA KUFUNGA.


2) MAANA YA KUFUNGA KATIKA SHARIA YA KIISLAM.
MAANA YA KUFUNGA KATIKA SHARIA YA KIISLAMU NI KUJIZUIA NA YOTE YANAYOFUNGUZA, KUANZIA ALFAJIRI YA KWELI, MPAKA MAGHARIBI, PAMOJA NA KUTIA NIA YA KUFUNGA USIKU.

3) NGUZO ZA KUFUNGA (SWAUMU) NI MBILI (2)

NGUZO ZA KUFUNGA NI MBILI:
NGUZO YA KWANZA NI :
1) KUTIA NIA YA KUFUNGA USIKU KATIKA SIKU ZOTE ZA MWEZI WA RAMADHANI. NIA NI DHAMIRA ANAYOKUA NAYO MTU MOYONI MWAKE KUWA ATAFUNGA, NIA MAHALA PAKE NI MOYONI.
MFUNGAJI ANALAZIMIKA KUTIA NA YA KUFUNGA KILASIKU USIKU KATIKA MWEZI WOTE WA RAMADHANI. MWANZO WA NIA NI BAADA YA KUFUTURU HADI MWISHO WA KULA YAANI MWISHO WA KULADAKU, NDIO MWISHO WA KUTIA NIA. KWA HIVYO MWENYE KUFUNGA BILA YA KUTIA NIA (KUNUWIYA) FUNGA YAKE NI BATILI.





NGUZO YA PILI NI :
2) KUJIZUIA NA YOTE YANAYOFUNGUZA KUANZIA ALFAJIRI YA KWELI MPAKA MAGHARIBI.

4) MASHARTI YA KUWAJIBIKA KUFUNGA

MASHARTI YA KUWAJIBIKA KUFUNGA NI KAMA IFUATAVYO :

1) MFUNGAJI AWE MUISLAM.
2) AWE NA AKILI TIMAMU
3) AWE NA UWEZO WA KUFUNGA KIAFYA.(ASIWE MGONJWA).
4) AWE MKAZI WA MJI (ASIWE MSAFIRI).
5) AWE AMEBALEHE.
6) ASIWE KATIKA HEDHI AU NIFASI.


5) MAMBO YANAYOHARIBU SWAUMU (YANAFUNGUZA)
MFUNGAJI LAZIMA AJIZUIE NA VITENDO VINAVYOWEZA KUHARIBU SWAUMU (FUNGA) YAKE.
MAMBO YANAYOHARIBU SWAUMU NI HAYA HAPA YAFUATAYO:
1) KULA AU KUNYWA KWA MAKUSUDI.
2) KUJITAPISHA KWA MAKUSUDI.
3) KUJITOA MANII(MBEGU ZA UZAZI) KWA MAKUSUDI.
4) KUFANYA TENDO LA NDOA(KUJAMIIANA) MCHANA WA RAMADHANI.
5) KUINGIZA KITU CHOCHOTE KATIKA TUNDU SABA ZA MWILI KWA MAKUSUDI(MAKUSUDIO YA TUNDU SABA ZA MWILI, NI TUNDU MBILI ZA MASIKIO, TUNDU MBILI ZA PUA , MDOMO, SEHEMU INAPOTOKA HAJA KUBWA NA SEHEMU INAPOTOKA HAJA NDOGO).
6) KUNUWIA KUFUNGULIA. MFUNGAJI AKINUWIA KUFUNGULIA HATA KAMA HAKUFUNGULIA SWAUMU YAKE ITAHARIBIKA.
7) KUVUTA SIGARA.
8) KUBWIA UGORO
9) KUNUSA TUMBAKU
10) KUPATWA NA WAZIMU
11) KUTAFUNA TAMBUU
12) KURTADDI (KUTOKA KATIKA UISLAMU)
13) KUPATWA NA HEDHI
14) KUPATWA NA NIFASI.


PAMOJA NA HAYA PIA, MFUNGAJI NI LAZIMA AJIEPUSHE MAASI YOTE KAMA VILE :
KUACHA SWALA, ULEVI, WIZI, DHULMA, RUSHWA, UTAPELI, UONGO,UMBEYA, KUSENGENYA, KUTUKANA, KUGOMBANA, KUPIGA POROJO, KUSIKILIZA ALIYOYAKATAZA MWENYEZI MUNGU. KWA UFUPI NI KWAMBA , MFUNGAJ ANTAKIWA AJIEPUSHE NA KILA KITENDO KITAKACHOPELEKEA KUVUNJA AMRI YA MWENYEZI MUNGU NA MTUME WA MUHAMMAD (S.A.W). KWANI KUFUNGA SI KUACHA KULA NA KUNYWA TU BALI KUFUNGA NI KUACHA KULA NA KUNYWA NA MAASI YOTE NILIYOYATAJA, KINYUME CHA HAYO HAKUNA FUNGA, BALI NI KUSHINDA NA NJAA PAMOJA NA KIU.
KWA HIYO EWE MFUNGAJI KUWA MAKINI JUU YA HAYA, USIJE UKAIHARIBU FUNGA YAKO KWA KUTENDA MAASI HAYA NILIYOYATAJA.

6) MAMBO YASIYOHARIBU SWAUMU(FUNGA)

HAITAHARIBIKA SWAUMU KWA MATENDO YA FUATAYO:
1) KULA AU KUNYWA KWA KUSAHAU AU KWA KULAZIMISHWA KIASI CHA KUTISHIA MAISHA.
2) KUTAPIKA BILA KUKUSUDIA
3) KUTOKWA NA MANII(MBEGU ZA UZAZI) KWA KUOTA AU KWA NAMNA AMBAYO HAKUKUSUDIA.
4) KUOGA MCHANA WA RAMADHANI AU WAKATI WOWOTE.
5) KUAMKA NA JANABA
6) KUPIGA MSWAKI
7) KUSUKUTUA
8) KUTIA DAWA YA MACHO
9) KUPAKA WANJA
10) KUUMIKA (KUPIGA CHUKU)
11) KUJIPAKA MAFUTA AU MANUKATO
12) KUPIGA SINDANO
13) KUWEKA DAWA KWENYE JERAHA.
14) KUTOKA DAMU AU USAHA KWENYE JERAHA AU KWA KUJIKATA
15) KUTUMBUA JIPU
16) KUCHEKA
17) KULALA
18) KUNG’OA JINO
19) KULIA

7) WANAORUHUSIWA KULA MCHANA WA RAMADHANI KWA MUJIBU WA SHARIA YA KIISLAM NI HAWA WAFUATAO :

1) MGONJWA : MTU AKIJIONA MGONJWA HANA AFYA NZURI YA KUMUWEZESHA KUFUNGA, ANARUHUSIWA KULA, KISHA ATALIPA AKIPONA UGONJWA WAKE. NA KAMA UGONJWA WAKE NI WA KUDUMU USIOTARAJIWA KUPONA, ATATOA FIDIA AMBAYO NI KIBABA KIMOJA CHA CHAKULA KUWAPA MASIKINI KILA SIKU KATIKA MWEZI WOTE WA RAMADHANI.
KIBABA KIMOJA NI SAWA NA KAMA KILO KASROBO YA CHAKULA KINACHOTUMIWA SANA, KATIKA MJI HUSIKA KAMA HAPA KWETU (DAR ES SALAAM NA PWANI) NI MCHELE.

2) MSAFIRI : MTU AKIWA SAFARINI ANARUHUSIWA KULA KISHA ATALIPA SIKU ALIZOKULA AKIWA SAFARINI. SAFARI AMBAYO MTU ANARUHUSIWA ASIFUNGE NI SAFARI INAYOANZIA UMBALI WA KILOMITA THAMANINI NA MOJA (81 KMS)
3) MZEE : MTU MZIMA (KIKONGWE AU AJUZA) AMBAE HAWEZI KUFUNGA KWA SABABU YA UZEE, ANARUHUSIWA KULA, NA BADALA YAKE ATATOA FIDIA AMBAYO NI KIBABA CHA CHAKULA, KUMPA MASIKINI KILA SIKU, KATIKA MWEZI WOTE WA RAMADHANI.
4) MJAMZITO NA MWENYE KUNYONYESHA
MWANAMKE MJAMZITO AU ANAYENYONYESHA WANARUHUSIWA KULA, KISHA WATALIPA SIKU WALIZOKULA BAADA YA KUJIFUNGUWA NA KUACHISHA ZIWA.

8) MWANAMKE MWENYE HEDHI AU NIFASI
MWANAMKE ALIYE KATIKA HEDHI AU NIFASI NI HARAMU KWAKE KUFUNGA MPAKA ATAKAPOTAKASIKA NA ATALAZIMIKA KULIPA SIKU ALIZOACHA BAADA YA KUKATIKA HEDHI YAKE AU NIFASI YAKE.
9) SUNNA ZINAZOAMBATANA NA FUNGA YA RAMADHANI
KATIKA MWEZI WA RAMADHANI KUNA MAMBO KADHAA ALIYOYAFANYA MTUME (S.A.W) NA KUTUSISITIZA NASI TUYAFANYE. MIONGONI MWA MAMBO HAYO NI KAMA IFUATAVYO:
1) KULA DAKU NA KUCHELEWESHA
DAKU NI CHAKULA KINACHOLIWA USIKU WA MANANE KWA AJILI YA KUJIANDAA KUFUNGA SIKU INAYOFUATA. KULA DAKU NI SUNNA ILIYOKOKOTOZWA NA MTUME (S.A.W). VILEVILE NI SUNNA KUCHELEWESHA KULA DAKU. KILA INAPOLIWA DAKU KARIBU ZAIDI NA ALFAJIRI NDIVYO INAVYOKUA BORA ZAIDI.
2) KUHARAKISHA KUFUTURU(KUFUTURU MAPEMA)
NI “SUNNA ILIYOKOKOTEZWA” KUFANYA HARAKA KUFUTURU MARA LINAPOKUCHWA JUA NA KABLA YA SWALA YA MAGHARIBI. PIA NI SUNNA KUANZA KUFUTURU KWA TENDE AU KWA MAJI.
3) KUOMBA DUA WAKATI WA KUFUTURU.
NI SUNNA KUOMBA DUA WAKATI WA KUFUTURU KAMA VILE KUOMBA KWA KUSEMA : « EWE MOLA WANGU NIMEFUNGA KWA AJILI YAKO NA NIMEFUNGULIA RIZIKI YAKO «
4) KUSOMA QUR-AN
5) KUTOA SADAKA KWA WINGI
6) KUSWALI SWALA YA TARAWEHE
7) KUZIDISHA KUTENDA MAMBO YA KHERI. KAMA VILE KUMFUTURISHA ALIYEFUNGA, KUSAIDIA MAYATIMA, KUSAIDIA WENYE MATATIZO,N.K.
8) KUZIDISHA KUFANYA IBADA KATIKA KUMI LA MWISHO
9) KUKAA ITIKAFU KATIKA KUMI LA MWISHO
10) KUUTAFUTA USIKU MTUKUFU WA LAILATUL QADRI KATIKA KUMI LA MWISHO.


HITIMISHO :
NIMEGUNDUA KWAMBA BAADHI YA WAUMINI WANAOFUNGA MWEZI WA RAMADHANI, KWAMBA HAWASWALI SWALA TANO. KUACHA KUSWALI NI KOSA KUBWA LINALOWEZA KUMTOA MTU KATIKA DINI YA KIISLAM. KWA HIVYO, WALE WENYETABIA YA KUFUNGA TU BILA KUSWALI WAACHE TABIA HIYO, BALI WAFUNGE PAMOJA NA KUSWALI SWALA TANO SIKU ZOTE, NA SIO KUSWALI KATIKA MWEZI WA RAMADHANI TU.


WABILLAH TAUFIQ
IMEANDIKWA NA :
ALLY MUHIDINI MKOYOGORE
IMAM WA MASJID SWAHILINA
KINONDONI MOROCCO BLOCK 41
NA USTADH KATIKA MASJID
AL – QADIRIYYA TEMEKE
WAILES MTAA WA CHANGANI
P.O.BOX : 45635
KWA MAONI, MASWALI TUMIA NJIA YA SIMU YA MKONONI AU POSTA.
MOB : 0787 73 04 30
OR
0767 73 04 30

2 comments:

  1. JAZAKA LLAHU KHEYR, MUNGU akulipe inshaalah umenielimisha na unatuelimiha.SALUM PAZZY, 0715282984

    ReplyDelete
  2. Shukrani sana sheikh kwa Makala Nzuri yenye kutoa elimu.Allah akupe umri na mafanikio zaidi, inshallah

    ReplyDelete