KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, May 26, 2009

Nyerere na Amin walipokutana



Nyerere na Amin walipokutana

Watoto wa Nyerere na Amin walipokutana kwa mara ya kwanza, tangu kumalizika vita....








Ilikuwa ni siku ya Alhamisi, tarehe tisa Aprili 2009, wakati historia ya Afrika Mashariki ilipoandikwa upya. Mtoto wa kiume wa Idi Amin aliyekuwa rais wa Uganda na mwingine wa rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere walikutana kwa mara ya kwanza miaka 30 tangu nchi hizo zilipopigana vita.

Angalia picha za Butiama

Kwa mtizamo wa Jaffar Amin, familia hizo mbili zilitakiwa kuwa zimeshakutana kwasababu “wao ndiyo walikuwa vinara”. Ilichukua muda mrefu kumshawishi Madaraka Nyerere, lakini hatimaye alikubaliana na wazo “kwasababu baba zetu sasa walishafariki.”

Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kitengo cha mahusiano ya umma cha BBC ikitangaza mpango wa kuwakutanisha Madaraka Nyerere, 47, na Jaffar Amin, 42, ilipokelewa kwa hisia tofauti.

Baadhi walimaka: “Huu upuuzi! Haiwezekani na wasiruhusiwe kukutana.” Wengine walikuwa na mtizamo tofauti wakaimwagia BBC sifa kwa kubuni wazo la kuwakutanisha.

Mipango ya kuwakutanisha wana hao wawili ilianza katikati ya mwaka 2008, wakati kikosi cha Idhaa ya Kiswahili ya BBC kilipozuru Arua, kaskazini magharibi mwa Uganda na kufanya mahojiano marefu na Jaffar.


Madaraka na mgeni wake Jaffar walishiriki matangazo ya BBC baada ya kukutana Butiama, Aprili 9, 2009.



“Tumekuwa tukitengwa kisiasa”, Jaffar alisema huku akimwelezea baba yake kwa fahari, ambaye alibebeshwa majina yote mabaya: muuaji, mla watu, mpenda wanawake na mbaguzi wa rangi - kwa kuwafukuza raia wenye asili ya Asia kutoka Uganda mwaka 1974. Orodha ya maovu yanayodaiwa kufanywa na baba yake ni ndefu isiyo na mwisho.

Utawala wake ulisambaratishwa na Rais Nyerere ilipofika April 1979 wakati wanajeshi wa Tanzania walipoingia mji mkuu Kampala kwa kishindo, Idi Amin pamoja na familia yake walikimbilia uhamishoni, kwanza Libya na baadaye Saudi Arabia ambako alifariki dunia mwaka 2003.

Changamoto
Baada ya kufanikiwa kupata ridhaa ya Jaffar na Madaraka, changamoto nyingine ilikuwa kutafuta mahali pa kufanyia mkutano wao huo mkubwa, kulikuwa na wazo la kufanyia katikati - isiwe Butiama wala Arua.

Lakini Jaffar alisisitiza kuwa yuko tayari kusafiri kwenda Butiama kutoa heshima kwa to mtu ambaye alimng’oa baba yake madarakani na kukimbilia uhamishoni. Madaraka alikubali mara moja kuwa mwenyeji. Kwa baadhi ya wasikilizaji wetu hili halikuwa jambo walilolikubali kwa urahisi.

Safari ya Jaffar kwenda Tanzania ilianza Jumatatu, tarehe 6 mwezi Aprili, kutoka nyumbani kwake Arua akielekea mji mkuu Kampala kabla ya kuvuka mpaka na kuingia ardhi ya Tanzania.


Angalia picha za Butiama

Huku Jaffar akifanya safari yake katika njia walikopita wanajeshi wa Tanzania wakati wa vita, Madaraka Nyerere alikuwa akifanya maandalizi ya mwisho kumpokea mgeni maalum kutoka Uganda.

Mchana wa Alhamisi, tarehe tisa, gari aina ya Toyota Prado iliyokuwa imembeba Jaffa iliingia katika lango la makazi ya hayati Mwalimu Julius Nyerere. Akiwa katika vazi la kiafrika, alitoka nje ya gari huku akitabasamu.

Mwenyeji wake, pia katika vazi la kiafrika, hakuficha shauku yake. Wawili hao walikumbatiana na kucheka kabla ya kuingia kwenye jengo lenye kaburi la Mwalimu Nyerere aliyefariki mwaka 1999.

Akiwa mbele ya kaburi la hayati Nyerere, Jaffar ambaye ni mswalihina alisoma dua zake. “Nimekuja hapa kwa amani,” alisema kabla ya kuweka shada la maua.

Mazungumzo
Ilikuwa wazi kuwa wana hao wawili wa kiume walikuwa na mtizamo sawa na haikushangaza watu waliokuwepo, pale walipoomba kufanya mazungumzo ya faragha. Yaliyozungumzwa bado ni siri kati yao wawili.

Umati ulilipuka kwa nderemo, ngoma za jadi za kabila la wazanaki zilirindima wakati wana hao waliposhika vinasa sauti kuanza kuzungumza.

“Imepita miaka 30 ambayo katika familia zetu hakuna aliyefikiria wazo la kukutana,” Jaffar alisema, “Madaraka na mimi tulifanya uamuzi mgumu lakini wa kihistoria. Tusingependa kuwa upande mbaya wa historia.”

Katika machache aliyozungumza kumkaribisha mgeni wake, Madaraka alimwelezea baba yake kuwa ni mpenda amani. “Hata baada ya vita, angekubali kukutana na Idi Amin na hata kumwalika Butiama.”

“Tofauti zozote walizokuwa nazo kabla, tunachoweza kufanya sasa ni kujifunza na yaliyotokea na kuanza ukurasa mpya.”

Uhasama
Siasa za Afrika Mashariki kunako miaka ya 1970, zilitawaliwa na uhusiano mbaya kati ya Nyerere wa Tanzania – msomi na mpigania ujamaa na Amini wa Uganda ambaye hakuwa na elimu kubwa na mtoto wa mkulima aliyeinukia kutoka jeshini kabla ya kufanya mapinduzi ya kijeshi na kunyakua madaraka.

Katika matukio tofauti, wawili hao waliwahi kurushiana maneno. Nyerere wa Tanzania alimwita Idi Amini mpuuzi, mdhalimu na kibaraka wa nchi za Magharibi, wakati Amin alimwita mwenzake wa Tanzania mwoga.


Jaffar alifika kutoa heshima kwenye kaburi la hayati Mwalimu Nyerere.



Jitihada za kumng’oa Amin zilipamba moto wakati majeshi ya Uganda yalipovamia na mkoa wa Kagera, ulioko kaskazini magharibi mwa Tanzania mwezi Oktoba 1978.

Wanajeshi wa Tanzania waliingia Uganda, si tu kuwatimua wavamizi, lakini kwenda mpaka Kampala kumng’oa Idi Amin.

Takriban watu milioni moja waliuawa na uchumi wa mataifa hayo mawili kuathirika kwa kiasi kikubwa.

Nani angedhani miaka 30 baadaye, wana wa kiume wa Amin na Nyerere wangeweza kuweka kando tofauti za baba zao? Kama alivyosema mzungumzaji mmoja katika mkutano huo wa Aprili tisa 2009, historia imeajiandika upya, kwa hisani ya BBC.

No comments:

Post a Comment