KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, May 15, 2012

Biashara ya dawa za kulevya sasa tishio

Kamanda wa Polisi wa Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa Kiwango cha uingizaji wa dawa za kulevya nchini kinaongezeka kwa kasi kubwa na ya kutisha licha ya serikali kusema inakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote. Hali hiyo inatokana na kiwango cha dawa za kulevya zilizokwishaingizwa kwa kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu kukaribia kiwango cha dawa zilizoingizwa katika kipindi cha mwaka mzima wa 2011. Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa, alisema katika kipindi cha Januari mpaka Mei mwaka huu, kikosi chake kimefanikiwa kukamata kilo 234 za heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 10.53 Kamanda Nzowa, alisema vilevile kikosi chake kilifanikiwa kukamata kilo 16 za cocaine zenye thamani ya Sh. milioni 880 katika kipindi hicho cha kati ya Januari na Mei, mwaka huu. Kamanda Nzowa alibainisha kuwa, katika kipindi hicho, kikosi chake pia kilikamata kilo 2,623 za mirungi (miraa) yenye thamani ya Sh. milioni 131.15 pamoja na bangi kilo 4,562 zenye thamani ya Sh. milioni 912.4. Kwa mujibu wa Kamanda Nzowa, jumla ya dawa zote za kulevya zilizokamatwa kati ya Januari na Mei mwaka huu ni kilo 7,435. Takwimu zilizoko katika ofisi ya Kamanda Nzowa zinaonyesha kuwa, kuanzia Januari mpaka Disemba 2011 zilikamatwa kilo 264 za heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 10.8, na cocaine kilo 126 zenye thamani ya Sh. bilioni 6.9. Kiongozi huyo wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, alisema kuwa, kiwango hicho cha dawa kingefanikiwa kuwafikia watumiaji ina maana kuwa kingetumiwa na watu wasiopungua 2,127,800, jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi wa taifa na kuongeza kuwa, jumla ya watuhumiwa 28 walikamatwa kwa kukutwa na heroine na watuhumiwa 8 kwa kukamatwa na cocaine, na wote kesi zao ziko Mahakama Kuu ya Tanzania. “Kazi kubwa tunayoifanya ni kuhakikisha kuwa dawa hizo zinakamatwa kabla hazijawafikia walengwa, ndiyo maana unaona kiwango cha dawa zilizokamatwa ni kubwa kuliko watuhumiwa kwa mfano, kilo 97 zilizokamatwa Septembea mwaka jana ziliingizwa na watuhumiwa wanne tu,” alisema Kamanda Nzowa. Aidha aliongeza kuwa, kiwango cha ukamataji kimekuwa ni kikubwa na cha kuridhisha, kwa kuwa elimu ya kutosha imetolewa kwa wananchi ambao wameonyesha ushirikiano mkubwa sana kwa kutoa mchango wao katika vita hivyo kwa kutoa taarifa pale wanapohisi kuwepo kwa biashara hiyo au watuhumiwa huko mitaani kwao. Alipotakiwa na NIPASHE kuthibitisha kama Tanzania imekuwa ni kituo kikubwa cha kusafirisha dawa hizo au ndiyo imekuwa soko kubwa, Kamanda Nzowa, alisema kuwa ni vigumu sana kulithibitisha hilo kwani zipo nchi nyingi ambazo zimekuwa aidha wasafirishaji wakubwa au watumiaji. Hata hivyo, Kamanda Nzowa, alisema ni vigumu kubaini kwa kuwa wasafirishaji wa dawa hizo wamekuwa wakiibuka na mbinu mpya na tofauti tofauti kila siku

No comments:

Post a Comment