KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, March 31, 2011

'Wahamiaji Waafrika kuondoshwa' kisiwani



Waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi ameahidi kuwa kisiwa cha Lampedusa karibu kitakuwa hakina wahamiaji Waafrika.

Maelfu ya watu wamewasili katika kisiwa hicho kusini mwa Sicily tangu Januari, wakisafiri kutoka Tunisia na Libya.

Maafisa wamesema hali ya usafi imekuwa "mbaya" sana na wakazi wa kisiwa hicho wameandamana.


Wahamiaji Lampedusa


Alipotembelea kisiwa hicho, Bw Berlusconi alitangaza kwa umati wa watu kuwa "katika kipindi cha saa 48 hadi 60 Lampedusa itakaliwa na raia wa Lampedusa pekee".

Takriban wahamiaji 20,000 wamevuka bahari ya Mediterranea tangu mageuzi yaanze huko Afrika kaskazini na mashariki ya kati mwezi Januari.





Silvio Berlusconi


Dharura
Wahamiaji 6,000- zaidi ya idadi ya watu wote waishio katika kisiwa hicho- sasa wanaishi kwenye kambi za muda.

Siku ya Jumanne usiku hakujakuwa na wahamiaji wowote waliofika kisiwani hapo, chombo cha habari cha Italia kiliripoti, usiku wa kwanza kukosa wahamiaji kuwasili tangu waanze kuingia kisiwani humo.


Siku ya Jumatano asubuhi, meli tano ziliwasili, zilizoagizwa na serikali ya Italia kwenda Lampedusa kuchukua wahamiaji na kuwapeleka bara.

Ndege ya Bw Berlusconi ilifika kisiwani hapo baada ya saa 1300.

Baada ya kukutana na gavana wa eneo hilo na meya wa Lampedusa, alihutubia umati wa wakazi wa kisiwa hicho, huku akiwaahidi msururu wa hatua zitakazochukuliwa zikiwemo kufutwa kwa kodi na ruzuku.

Alisema pia kutakuwa na mpango wa kuzindua upya shughuli za utalii za Lampedusa, ambazo zimeathirika sana na kiwango kikubwa cha watu kutoka Afrika ya kaskazini.

Siku moja kabla, aliwaelezea wahamiaji hao waliokuwa wakienda Lampedusa kuwa ni "fukara" wakikimbia ulimwengu usiokuwa na uhuru wala demokrasia.

Japokuwa wengi wa wahamiaji hao wanatarajiwa kupelekwa Sicily au kambi zilizo bara ya Italia, majadiliano yanaendelea ya kuwarejesha wengi wao Tunisia.

Wengi waliowasili kisiwani hapo tangu mwezi Januari wamesafiri kwa maji kutoka Tunisia, lakini katika siku za hivi karibuni boti zimetoka kutoka Libya pia.






Mabomu yagunduliwa Dortmund




Ofisi ya polisi inayohusika na uhalifu nchini Ujerumani imelizima jaribio la shambulio la bomu katika uwanja wa mpira wa miguu wa Dortmund. Gazeti la Bild limeripoti kuwa wapelelezi waligundua maeneo mawili ardhini yaliyokuwa na mabomu na silaha.

Moja liligunduliwa karibu na uwanja wa mpira wa Dortmund na jingine mjini Krefeld. Ofisi hiyo imethibitisha kuwa ilikuwa inafanya uchunguzi wa mabomu yanayodhaniwa kupatikana katika jimbo la North-Rhine Westphalia.

Mjerumani mwenye umri wa miaka 25 anayetuhumiwa yuko chini ya ulinzi baada ya kukamatwa mjini Cologne. Wapelelezi wanasema bado haijafahamika iwapo mabomu hayo yalikuwa yatumike wakati wa mechi dhidi ya Hanover siku ya Jumamosi, ambapo mashabiki 80,000 wanatarajia kuhudhuria pambano hilo.








Bomu la ndani ya barua laripuka Uswisi




Bomu lililokuwa ndani ya barua limeripuka katika ofisi za shirika la nishati ya nyuklia la Uswisi na kuwajeruhi watu wawili.

Polisi wamesema kuwa barua hiyo imeripuka katika ofisi hizo zilizoko kwenye mji wa kaskazini mwa nchi hiyo wa Olten. Waathirika wote wamepatwa na majeraha madogo. Hakuna mtu au kundi lililodaii kuhusika na shambulio hilo








Kan na Sarkozy wataka masharti magumu ya nyuklia






Waziri Mkuu wa Japan, Naoto Kan na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wametoa wito wa kuimarishwa viwango vya kimataifa vya usalama wa nyuklia kutokana na janga la nyuklia katika kiwanda cha nyuklia cha Fukushima nchini Japan.

Katika ziara yake kuonyesha mshikamano na Japan kufuatia maafa hayo, Rais Sarkozy ametaka kufanyike mkutano miongoni mwa mashirika ya usalama wa nyuklia kutoka kundi la mataifa 20 yaliyoendelea kiuchumi duniani-G20, ili kuanzisha sheria za kimataifa.

Katika mkutano na waandishi habari pamoja na Rais Sarkozy, Waziri Mkuu Kan amesema Japan iko tayari kushirikiana na ulimwengu katika kuelezea uzoefu wake kuhusu maafa ya nyuklia, lakini nchi hiyo itaendelea kutumia nishati ya nyuklia.

Mkusanyiko wa madini ya joto yenye mionzi ya nyuklia katika maji ya bahari karibu na kiwanda cha Fukushima umefikia viwango vipya karibu mara 4,400 zaidi kuliko kiwango halali kinachotakiwa. Kiwanda hicho kiliharibiwa kutokana na tetemeko la ardhi na tsunami iliyoikumba nchi hiyo tarehe 11 ya mwezi huu wa Machi na kuharibu mfumo wa kupoza mitambo, hivyo kusababisha vinu vya nyuklia katika kiwanda hicho kupata joto kupita kiasi.







San Pedro wadhibitiwa na wapiganaji wa Ouattara






Wapiganaji wanaomtii kiongozi wa Cote d'Ivoire anayetambuliwa kimataifa, Alassane Ouattara wameudhibiti mji wa San Pedro, bandari kubwa nchini humo inayosafirisha kakao. Hatua hiyo imefikiwa baada ya taarifa kueleza kwamba tayari wameudhibiti mji mkuu wa utawala wa Yamoussoukro. Rais anayeng'ang'ania madaraka, Laurent Gbagbo bado anaudhibiti mju mkuu wa Abidjan.

Wakati huo huo, mkuu wa jeshi la Cote d'Ivoire, Jenerali Philippe Mangou ameomba hifadhi ya ukimbizi katika makaazi ya balozi wa Afrika Kusini nchini humo. Jenerali Mangou, mshirika muhimu wa Gbagbo aliwasili jana jioni katika makaazi ya balozi huyo wa Afrika kusini nchini Cote´d´Ivoire, Zodwa Lallie, akiwa na mkewe na watoto wake watano.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 4,600 wameuawa katika mapigano nchini Cote d'Ivoire kutokana na mzozo wa uchaguzi wa rais wa Novemba mwaka uliopita ambao Umoja wa Mataifa unaamini kuwa Gbagbo alishindwa.

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linamtaka Gbagbo kukabidhi madaraka kwa Ouattara. Azimio hilo pia limeweka vikwazo vya marufuku ya kusafiri na kuzuia mali za Gbagbo, mkewe pamoja na wasaidizi wake watatu muhimu.





Marekani na Uingereza zapeleka majasusi Libya




Marekani na Uingereza zimewapeleka mawakala wa kijasusi nchini Libya kuwasiliana na waasi na kukusanya data za kuongoza mashambulizi ya anga yanayofanywa na jeshi la muungano.

Gazeti la Marekani la New York Times limeripoti kuwa Rais Barack Obama amesaini amri ya siri kuruhusu operesheni za Shirika la Ujasusi la Marekani-CIA nchini Libya. Rais Obama amehakikisha kuwa hakuna wanajeshi wa ardhini watakaopelekwa Libya katika juhudi za kuwalinda raia wa Libya.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, makundi madogo ya mawakala wa Kimarekani yamekuwa yakifanya shughuli ndani ya Libya kwa wiki kadhaa sasa. Vikosi maalum vya Uingereza na mashirika ya kijasusi ya siri pia viko Libya vikikusanya data za vikosi vya serikali na silaha.






Baraza la mawaziri Kuwait lajiuzulu



Shirika la habari la Kuwait limesema kuwa Baraza la mawaziri la nchi hiyo limejiuzulu leo kutokana na mzozo katika eneo hilo la Ghuba ukilengwa mzozo nchini Bahrain. Shirika hilo limesema kuwa baraza hilo limejiuzulu kutokana na matukio ya hivi karibuni ya nchi hiyo katika umoja wa kitaifa, usalama na utulivu.

Hatua hiyo inaonekana kuwa jaribio la mawaziri watatu kutoka familia inayotawala kuepuka kujibu masuali kwa nini Kuwait haijachangia kupeleka majeshi katika kikosi cha nchi za Ghuba ambacho kilipelekwa Bahrain. Mwanzoni mwa wiki hii, wabunge waliwaita mawaziri hao watatu kueleza uamuzi wa nchi hiyo kutopeleka wanajeshi wake Bahrain.







Kisiwa cha Mayote chawa rasmi sehemu ya Ufaransa









Visiwa vya ComoroKisiwa cha Mayotte kimejiunga rasmi hii leo kuwa sehemu ya nchi ya Ufaransa. Hatua hii inafuatia baada ya wananchi wa kisiwa hicho kupiga kura ya maoni iliyoandaliwa na Ufaransa kuhusu kujitenga na Comoro.

Hata hivyo utawala wa serikali kuu ya Comoro huko Moroni una msimamo mwengine kuhusu hatua hiyo.Ili kujua zaidi kuhusu vipi suala hili lilivyopokelewa na serikali,Saumu Mmwasimba amezungumza na mkuu wa kamati ya Komoro inayohusika na suala la kisiwa cha Mayotte na balozi wa Komoro nchini Afrika Kusini Ahmed Thabit






Mji mkuu wa Ivory Coast wazingirwa




Majeshi yanayomtii Rais wa Ivory Coast anayetambuliwa na jumuiya za kimataifa , Alassane Ouattara, yamezingira mji mkuu wa Abidjan kutoka maeneo mbalimbali

Hatua hiyo inatishia kusababisha mapambano kwenye mji huo, ngome ya mwisho ya Rais mpinzani Laurent Gbagbo.


Majeshi yanayomtii Ouattara

Awali mkuu wa majeshi wa Bw Gbagbo aliomba hifadhi kwa balozi wa Afrika Kusini.

Umoja wa Mataifa umesema Bw Gbagbo alishindwa kwenye uchaguzi mwaka jana, lakini amekataa kukabidhi madaraka kwa Bw Ouattara.

Majeshi yanayomwuunga mkono Bw Gbagbo yamekuwa yakishika doria kwenye wilaya za mji huo, na kuweka vizuizi vya barabarani.

Mwandishi wa BBC Valerie Bony mjini Abidjan alisema kumekuwa na mapigano makali kwenye kituo cha televisheni cha taifa liliopo eneo wanalokaa wakazi, na milipuko kwenye vitongoji kaskazini mwa nchi hiyo






Muammar Gadhafi ajigamba kushinda vita




Kiongozi wa Libya Leader Muammar Gadhafi Muammar Gadhafi amejigamba kuibuka na ushindi dhidi ya maadui zake wakati huu ambapo kanisa katoliki nchini Libya likitoa taarifa inayosema watu 40 wameuawa kutokana na hujuma za ndege za kivita za muungano.


Akizungumza baada ya taarifa za Waziri wa Mambo ya Nje, Mussa Kussa kuasi na kwenda nchini Uingereza hapo jana, Msemaji wa Serikali, Mussa Ibrahim amesema,hujuma inayofanywa na ndege za kivita ni uadui ulio wazi kabisa dhidi ya Walibya.

Waandishi wa habari walimuulza msemaji huyo kama Gadhafi na watoto wake bado wapo nchini Libya,alisema wapo na kuongeza kuwa wataendelea kuwepo mpaka mwisho.

Alisema,Libya ni nchi yao na wako madhibuti kukabiliana na kila jambo,akidai mapambano yanayoendelea sasa ni ya Walibya wote,wala si ya mmoja mmoja.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha France 24 hivi punde, Ibrahim alizungumzia suala ka kujiuzulu kwa Mussa Kussa kwa kusema serikali imempa kibali cha kuondoka nchini humo na hasa kwa kuzingatia matatizo yake ya kiafya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya,Mussa KussaIbrahim aliendelea kusema kwamba, Mussa Kussa ni mtu mzee,amechoka na mgonjwa kwa hiyo amepewa ruhusa kwa kuwa pengine itamsaidia kiafya na kisaikolojia.

Msemaji huyo wa serikali, alisema mataifa lazima yafahamu kwamba Gadhafi anapendwa kwa kuwa pamoja na mashambulizi ya anga ya majeshi ya muungano katika miji mingi nchini humo, lakini mpaka sasa hakuna kikundi,wala kabila lilioandamana na kutaka kiongozi huyo aondoke.

Huko Misrata,mji wa tatu kwa ukubwa nchini Libya bado mambo si shwari,vikosi vya Gadhafi vimekuwa vikifyatua mabomu kwa kutumia vifaru na upande wa Waasi unadai watu 20 wameuwawa.

Kwa upande wao waratibu wapya wa operesheni ya kuzuia ndege kuruka nchini Libya,NATO wamesema hivi sasa wanafanyia kazi ripoti inayosema mashambulizi yaliyofanyika mjini Tripoli yameuwa watu 40.

Moja wa waratibu,Luteni Generali Charles Bouchard amesema hivi kuna mjadala unaendelea kufuatia tuhuma hizo ambazo zimetolewa muda mfupi baada vikosi vya NATO kupata mamlaka kamili ya kuongoza operesheni hiyo.

Ripoti hiyo iliyosambazwa kwa vyombo vya habari imemnukuu Mwakilishi wa Baba Mtakatifu nchini Libya,Askofu Giovanni Innocenzo Martinelli ikisema hujuma ya mashambulizi ya anga iliyofanywa na vikosi hivyo katika wilaya ya Buslim imesabisha vifo vya watu 40.

Katika hatua nyingine NATO imesema imefanikiwa kunyong'onyesha mfumo wa kijeshi wa Libya ingawa hatua hiyo haimaanishi jeshi la Gadhafi lipo katika hatua ya kupoteza nguvu zake za kupambana.

Na huko Benghazi,Msemaji wa Waasi, Mustafa Gheriani amesema hivi sasa wapo katika mchakato wa kununua silaha kutoka mataifa ya nje ili kuweza kuvimudu vikosi vya serikali.

Hata hivyo Gheriani alikataa kuzungumzia taarifa zinazosema kuna vikosi maalum vya ardhini vya Marekani na Uingereza ambavyo hivi sasa vipo Libya kwa shabaha ya kuwasaidia Waasi hao

No comments:

Post a Comment