KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Friday, March 11, 2011
Merkel atangaza kufungwa kwa muda kwa vinu saba vya nyuklia
Kansela wa Ujerumani leo ametangaza kwamba vinu saba vya nyuklia vilivyoanza kufanya kazi tokea mwaka 1980, vitafungwa kwa muda.Kansela Markel ametoa tangazo hilo baada ya kukutana na viongozi kadhaa wa mikoa ya Ujerumani kuhusiana na suala la nishati ya nyuklia.
Hapo jana Kansela Merkel alisema kuwa usalama wa vinu vyote vya nyuklia vya Ujerumani utapitiwa upya na kutoa amri ya kusitisha kwa muda wa miezi mitatu hatua ya kuruhusu kuendelea kufanyakazi kwa vinu hivyo.
Mwaka jana serikali yake ilichagiza kurefushwa muda wa kuendelea kuwepo kwa vituo vya nguvu za nyuklia kwa wastani wa kipindi cha miaka 12 zaidi, na kubatilisha uamuzi hapo kabla wa serikali wa kuvifunga vituo vyote vya nishati hiyo ifikapo mwaka 2021
UN yasema mionzi ya nyuklia yaingia katika mfumo wa hewa duniani
Shirika la nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa leo limesema kuwa moto uliyoripuka katika kinu cha nyuklia katika mji wa Fukushima uliyoharibiwa na tetemeko la ardhi nchini Japan, umetoa mionzi iliyokwenda moja kwa moja katika hewa angani.
Kiwango cha mionzi ya nyuklia leo kimeongezeka ghafla huko nchini Japan mnamo wakati ambapo miripuko miwili imetokea katika kinu cha nyuklia kwenye mji wa Fukushima uliyoharibiwa na tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba nchi hiyo.
Serikali ya Japan imeonya kwamba kiwango cha mionzi hiyo karibu na kinu cha nyuklia cha Dai Ichi huko Fukushima kina hatarisha maisha ya watu na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Naoto Kan amewataka watu wanaoishi katika eneo la kilomita 30 kuzunguka kinu hicho kubakia majumbani mwao.
Wakati huo huo ubalozi wa Ufaransa mjini Tokyo umeonya kwamba kiwango cha chini cha mionzi hiyo ya nyuklia kinaweza kuukumba mji huo mkuu mnamo muda wa saa 10 zijazo, kutokana na upepo.Upepo huo unavuma kutoka kusini magharibi kuelekea Japan, lakini unatarajiwa kubadilisha uelekeo baadae hii leo kuelekea magharibi.
Kwa upande mwengine kiwango kamili cha madhara yaliyotokana na tetemeko la ardhi lililotokea Ijumaa iliyopita ambalo lilikuwa cha kiwango cha 9.0 richa na kusababisha Tsunami, bado hakijajulikana.
Maafisa wanasema kuwa takriban watu elfu kumi wameuawa kutokana na tetemeko hilo.Katika eneo la kaskazini mwa Japan kiasi ya nyumba elfu 85 hazina umeme, huku nyumba nyingine kiasi ya millioni moja unusu hazina huduma ya maji.Bei katika soko la hisa la Japan Nikkei zimeanguka kwa asilimia 14.
Masikini Japan, temeko na Tsunami yaiwacha nchi vipande
Maafa makubwa nchini JapanMaelfu ya walionusurika na mtetemeko mkubwa wa ardhi na mawimbi ya Tsunami, wanasongamana katika maeneo ya kuwahifadhi, huku juhudi za kuwatafuta wahanga wa maafa haya zikiendelea katika maeneo ya mwambao wa nchi hiyo.
Sura katika maeneo hayo ni ya kuitisha na kusikitisha. Magari na maboti yamekwama katika matope.
Picha za kutoka angani zinaonesha majumba na magari moshi yakirushwa juu kama vitu vya kuchezea watoto. Mawimbi makubwa ya maji kutoka baharini yaliyakumba maeneo yanayozunguka mji wa Sendai, kilomita 130 kutoka kwenye kiini cha mtetemeko huo, na moja ya kati ya maeneo yaliyopigwa vibaya sana.
Shahidi mmoja wa mkasa huo alisema aliiona barabara ikienda juu na chini kama mawimbi, majumba yalikuwa yanawaka moto na wakati huo huo theluji ikianguka.
Mripuko kwenye kinu cha nyukliya
Kansela Angela Merkel Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel
Ulimwengu waungana na Japan
Kansela Angela Merkel Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ameahidi kuipa Japan msaada wa muda mrefu ili kuyajenga upya maeneo yalioathirika na mtetemeko huo wa ardhi.
"Nataka kuwaambia watu huko Japan kwamba sisi katika dakika hii ngumu na isiokuwa ya kawaida tunawakumbuka. Kuna watu wengi waliokufa, na bila ya shaka ukumbwa wa balaa hilo utaonekana katika masaa yajayo.
"Tuko tayari kutoa msaada wote tunaoweza. Tayari tumepeleka mabingwa wa uokozi hadi Japan, na Ujerumani itafanya kila inachoweza, sio tu katika siku zijazo, lakini pia katika muda mrefu ujao, kushiriki katika ujenzi mpya wa maeneo yalioharibika." Alisema Merkel hapo jana akiwa mjini Brussels.
Pia Rais Barack Obama wa Marekani, amepeleka salamu zake za pole kwa serikali ya Japan; huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akiahidi kuisaidia Japan katika kipindi hiki kigumu.
Licha ya kwamba Wajapani wana vitabu vya kudurusu pale unapotokea mtetemeko wa ardhi, na kila wakati wanafanya mazoezi juu ya kujikinga na balaa zinazofuatana na jambo hilo, lakini kweli mtu anakumbuka kitabu alichosomeshwa wakati mtetemeko unapopiga?
Kila mtu wakati huo hukimbia wakati kila kitu kinapotikisika, na watu huambiwa tu fungeni gesi na moto katika nyumba zenu, lakini mambo hayo wakati huo hayagongi katika ubongo wa mtu.
Waziri Mkuu wa Japan, Naoto Kan, leo amewahimiza wananchi wawe watulivu, hasa wale walioko karibu na kinu cha kinyukliya kilichopigwa na tetemeko la ardhi.
Kan ameapa kuwa serikali yake itafanya kila iwezekanavyo kuhakikisha hakuna mtu hata mmoja atakayesumbuliwa na matatizo ya kiafya.
Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, Nobert Röttgen, amesema licha ya matatizo yaliotokana na vinu vya kinyukliya vya Japan, lakini hakuna hatari kwa Ujerumani.
"Kutokana na ujuzi wote tulio nao, haiwezekani kwa miyale ya kinyukliya kuwa na athari hapa Ujerumani. Hii inatokana na masafa makubwa kutoka Japan na pia kutokana na ujuzi tulionao kuhusu hali ya hewa." Alisema Röttgen.
Lakini mabingwa wa mambo wanasema huweza kukatokea na athari za kimazingira katika maeneo yalio karibu na Japan, hasa katika Bahari ya Pasifiki
Japan
Kinu cha Fukushima Dai-ichi Namba 3, baada ya mripukoWaokaji nchini Japan tayari wamegundua zaidi ya maiti 2,000 za wahanga wa tetemeko la ardhi la Ijumaa, huku kitisho kipya cha kuvuja kwa miale ya atomiki baada ya miripuko kwenye vinu viwili vya nyuklia nchini humo.
Juhudi za uokoaji zinaendelea, ambapo miili takribani 1000 imepatikana katika mji wa Minamisanriku, mji ambao umevurugwa vibaya na tetemeko hilo lililoambatana na Tsunami.
Jeshi la Polisi nchini kwa upande wa mji wa Miyagi linasema idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na balaa hilo inaweza kuzidi 10,000.
Katika tukio lingine, Serikali ya Japan imesema watu 11 wamejeruhiwa, mmoja akiwa hali mbaya sana, baada ya kutokea mripuko uliosababishwa na tetemeko hilo katika kinu kimoja cha nyuklia nchini
Miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na Tsunami nchini JapanKatibu Kiongozi wa Serikali ya Japan, Yukio Edano, amewataja wanajeshi wanne na wafanyakazi saba wa kinu hicho cha Fukushima Dai-ich kilichoripuka mapema leo, kuwa miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo.
Awali hali kama hiyo iliashiria kujitokeza katika kinu kingine, ambacho kilipoteza uwezo wa kujipoza na kuonesha kila dalili ya kuweza kuripuka.
Edano amesema majeruhi mmoja hali yake ni mbaya sana, na amepoteza kabisa fahamu, huku askari wanne ambao hawakujeruhiwa sana hivi sasa wamerejea katika vituo vyao vya kazi.
Hata hivyo, katibu mkuu huyo kiongozi amezugumzia kitisho cha kuvuja miyale ya nyuklia.
"Siwezi kukataa kwamba kuna uwezekano wa mabadiliko ya kimaumbeile ndani ya kinu chenyewe cha kuhifadhia nyuklia yaliyotokana na joto kali. Na kuna kipindi njia zenyewe hazikuwa katika mfumo wa kupozwa na maji." Amesema Edano.
Wanasayansi katika maeneo tofauti duniani wanaanza kufuatilia kwa karibu athari zinazoweza kutokea kutokana na kuripuka kwa vinu hivyo vya nyuklia.
"Kwa sasa inaonekana baada ya miripuko hii hakuna miyale ya nyuklia iliyovuja katika eneo lililokaribu na kinu cha nyuklia, kwa kuwa hakuna thibitisho la la kuvuja na miyale hio na kwamba miripuko imeharibu tu jengo la kiwanda hicho. Hivyo basi hizo ni habari njema." Amesema msemaji wa Shirika la Ujenzi na Usalama wa Vinu vya Nyuklia la Ujerumani (GRS), Sven Dokter.
Tayari wanauchumi ndani na nje ya Japan wameendelea kutathimini hali ilivyo na athari zitakazotokana na balaa hilo kwa kusema uchumi utatetereka kwa ujumla.
Kampuni ya kutengeneza magari ya Honda tayari imetengaza kusitisha uzalishaji mpaka Machi 20 kutokana na tetemeko hilo la ardhi lililotokea Kusini Mashariki mwa Japan.
Kampuni hiyo imefunga karakana zake zote za kutengeneza magari nchini humo na kuacha kiwanda cha kutengeneza pikipiki kilichopo Kisiwa cha Kyushu.
Kutokana na hali hizo zaa athari za tetemeko hilo kubwa, nchi zaidi ya sabini zimeahidi kutoa misaada ya kila aina kwa Wajapani.
Wasiwasi watanda Japan kuhusu kuvuja miale ya nyuklia
Maafisa wa polisi waliovaa vichuja hewa wapiga doria nje ya kinu cha Fukushima
Hatma ya kinu cha nyuklia cha Fukushima Daichi, na vinu nyengine vya nyuklia katika pwani ya mashariki ya Japan vinabakia katika hali ya kutia wasiwasi kufuatia tetemeko la ardhi
Shirika la kimataifa la kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia, IAEA, linasema wahandisi katika kinu cha nyuklia kilichoharibiwa kaskazini mwa mji mkuu wa Japan Tokyo wameanza kutumia maji ya baharini yaliyochangwa na kemikali aina ya boron kusaidia kupunguza uharibifu uliosababishwa na mlipuko mkubwa. Mlipuko huo ulitokea kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini humo Ijumaa iliyopita, lililokuwa la ukubwa wa 8.9 katika kipimo cha Richter.
Hatma ya kinu cha nyuklia cha Fukushima Daichi, yapata kilomita 240 kaskazini mwa Tokyo na vinu nyengine vya nyuklia katika pwani ya mashariki ya Japan vinabakia katika hali ya kutia wasiwasi kufuatia tetemeko hilo. Shirika la Japan linaloshughulikia masuala ya nyuklia na usalama wa viwanda, NISA, limsema wahandisi wamekuwa waking'anga'ana kupunguza shinikizo katika vinu hivyo ili kuzuia kuyeyuka kwa mitambo katika vinu hivyo.
Juhudi za serikali
Kufuatia kuvuja kwa miale ya nyuklia aina ya caesium 137 na iodine 131 katika eneo lililo karibu na kinu cha nyuklia cha Fukushima, shirika la NISA limesema kwene tovuti yake kwamba viwango vya miale hiyo angani vimeonekana vikipungua. Msemaji wa serikali ya Japan, Yukio Edano amesema wanafanya mambo mawili kwa wakati mmoja: kutoa hewa nje ya kinu hicho na wakati huo huo kutia maji.
Waziri mkuu wa Japan Naoto Kan
Msemaji huyo aidha amesema miale ya nyuklia iliyovuja sio mingi vile kiasi cha kuathiri afya ya wananchi. Edano amesema kulighulikia janga la tetemeko la ardhi litahitaji jitihada kubwa za kitaifa kwa kuwa ni janga lisilo na mithili. Kutahitajika pia ushirikiano mkubwa kati ya vikosi vya usalama na mashirika mengine. "Lengo letu ni kuokoa maisha na tunatarajia kiasi cha dola bilioni 2.4 katika bajeti ya mwaka huu kutosha, lakini ni vigumu kukadiria fedha zitakazohitajika katika bajeti ya mwaka ujao wa kibiashara unaoza Aprili mosi. Bunge litakuwa na jukumu la kuamua." amesema afisa huyo.
Vyombo vya habari vya Japan vimemkosoa waziri mkuu wa nchi hiyo, Naoto Kan, kwa jinsi serikali yake inavyoushulikia mlipuko uliotokea katika kinu cha nyuklia cha Fukushima, uliozusha hofu ya kuvuja kwa miale ya nyuklia angani. Naoto Kan amesema ameamuru watu umbali wa kilomita 20 kutoka kinu hiyo waondoke.
Kitisho cha Chernobyl
Wakati huo huo, wataalamu wa nyuklia wa Marekani wameonya juu ya kutokea mkasa kama ule wa Chernobyl nchini Ukraine uliotokea mnamo mwaka 1986 na ule mwingine katika kinu cha nyuklia cha kisiwa cha Three Mile katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani mnamo mwaka 1979. Robert Alvarez, anayeshughulikia masuala ya kupunguza silaha za nyuklia katika taasisi ya mafunzo ya sera, amesema hali imekuwa ya kukatisha tamaa mno kiasi kwamba Wajapani hawana uwezo wa kupata maji safi au maji yasiyo na chumvi kupoza mitambo katika kinu chake cha nyuklia cha Fukushima, na sasa wamelazimika kugeukia maji ya baharini.
Polisi ya Japan umesema leo kwamba idadi ya vifo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi inakaribia 900, huku watu 642 wakiwa hawajulikani waliko. Watu 1,570 walijeruhiwa katika tetemeko hilo la Ijumaa iliyopita.
Mripuko wa nyuklia Japan wazitikisa siasa za Ujerumani
Kansela Angela Merkel
Kuripuka kwa vinu vya nyuklia nchini Japan, kulikotokana na janga la tetemeko la ardhi na tsunami, kumezua mjadala mkali hapa Ujerumani, juu ya hatima ya vinu vya nyuklia vya taifa hili, huku wanasiasa wakitafautiana.
Imesadifu kwamba janga la kuripuka kwa vinu vya nyuklia vya Japan, linatokea wakati majimbo sita ya Ujerumani yakielekea kwenye chaguzi katika miezi michache ijayo.
Hili limezifanya siasa za atomiki ziingie kwenye siasa za chaguzi, hata ndani ya serikali ya mseto wa "Weusi na Manjano", kama inavyojuilikana serikali ya mseto ya vyama vya CSU/CDU na FDP inayoongoza Shirikisho la Ujerumani.
Ni serikali hii hii ambayo, katika majira ya mapukutiko ya mwaka jana, ilipitisha uamuzi wa kuongeza muda wa kutumika kwa vinu vikongwe vya nyuklia kwa miaka mingine 12. Lakini sasa, Kansela Angela Merkel, anasema uamuzi ule unadurusiwa upya, angalau kwa kipindi hiki.
"Jumamosi hii tumeamua kuwa, vinu vyote vya nyuklia vitafanyiwa uchunguzi kwa kuzingatia janga lililowapata wenzetu wa Japan. Katika uchunguzi huu hakuna jambo la kufichwa. Na kwa sababu hii, tunasitisha kidogo ule uamuzi wa kurefusha matumizi ya vinu hivi, angalau kwa miezi mitatu." Amesema Kansela Merkel.
Ndani ya kipindi hiki, timu ya wataalamu itapaswa kuthibitisha usalama wa mitambo yote, kama vile mfumo wa upozaji mashine, ambao unatajwa kuwa kufeli kwake ni miongoni mwa sababu za miripuko ya siku mbili zilizopita kwenye vinu vya Fukushima Daichi, nchini Japan.
Viongozi wa Die Grüne, Claudia Roth na Cem Oezdemir
Ndani ya kipindi hiki, timu ya wataalamu itapaswa kuthibitisha usalama wa mitambo yote, kama vile mfumo wa upozaji mashine, ambao unatajwa kuwa kufeli kwake ni miongoni mwa sababu za miripuko ya siku mbili zilizopita kwenye vinu vya Fukushima Daichi, nchini Japan.
Lakini kwa chama cha upinzani cha ulinzi wa mazingira, Die Grüne, ambacho tangu mwanzo kimekuwa kikipinga matumizi yoyote ya nishati ya atomiki, bado serikali inaichukulia kadhia ya Japan kijuujuu na kisiasa tu.
"Mtu anaweza kutuona kama vile tunaishi kwenye dhana tu, maana hawa jamaa ndio hawa hawa ambao hadi jana walikuwa wakituambia kuwa nishati ya atomiki ni salama. Lakini kile tulichokuwa tukikihofia sisi, ndicho hicho kinachotokea sasa." Amesema mwenyekiti mwenza wa Die Grüne, Cem Özdemir
Kiongozi wa SPD, Sigmar GabrielKiongozi wa chama cha upinzani cha SPD, Sigmar Gabriel
Mionzi ya nyuklia si jambo linalopendelewa wala linalohimilika kwa wanaadamu, lakini ni bunge la Ujerumani lililopiga kura katika mwezi Oktoba 2010, kuongeza muda wa vinu 17 vilivyo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, huku vikiwemo vile vilivyofikia umri wa miaka 30.
Kiongozi wa SPD, Sigmar GabrielKiongozi wa chama cha upinzani cha SPD, Sigmar Gabriel anasema kwamba, hata huu muda wa miezi mitatu uliowekwa na serikali kudurusu upya vinu hivi, hauna maana panapohusika hatari ambayo inalikabili taifa.
"Kwa mara nyengine tunajifunza kwamba, hicho kinachoitwa kizibo cha vichwa vya nyuklia, si kitu cha kudhania, bali ni kitu cha uhakika, kwamba kinaweza kuzibuka na kusababisha ajali mbaya sana. Kwa hivyo si jambo ambalo mtu anaweza kulidharau, na ndio sababu tunapaswa kuachana kabisa na masuala ya nishati ya atomiki badala ya kuongeza uwezekano wa kuingia hatarini." Amesema Sigmar.
Kwa vyovyote vile, siasa za atomiki zimesadifu kuchanganyika na siasa za uchaguzi nchini Ujerumani. Na kipimo cha kwanza kitakuwa uchaguzi wa wiki mbili zijazo katika jimbo la Baden-Württemberg, ambapo waziri mkuu wa jimbo hilo, Stefan Mappus, kutoka chama cha kihafidhina cha Kansela Merkel, CDU, anapigania tena nafasi hiyo.
Ikiwa Mappus, ambaye amenukuliwa akipuuzia kitisho chochote cha hatari za vinu vya nyuklia, atashindwa, basi utakuwa ujumbe mwengine wa Kansela Merkel, kuwa nyukulia itakuwa silaha nyengine ya kummaliza yeye mwenyewe kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment