KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, January 10, 2011

Ghasia za Tunisia zaitwa 'ugaidi'


Maandamano Tunisia


Rais wa Tunisia Zine El Abidine Ben Ali amesema wale walioshiriki kwenye maandamano ya hivi karibuni ndio wanaohusika na "vitendo vya ugaidi."

Pia ameitetea serikali yake kufuatia maandamano yanayoendelea juu ya ukosefu wa ajira, na kuahidi kuingeza nafasi za kazi.

Muungano wa Ulaya umeitaka Serikali ya Tunisia kuacha kutumia nguvu dhiidi ya waandamanaji wanaodai ajira na hali bora ya maisha.

Takriban watu 14 wamefariki dunia mwisho wa wiki wakati polisi walipowafyatulia risasi waandamanji hao.

Maandamano mapya yalifanyika kote nchini humo siku ya Jumatatu.

Vifo hivyo vimetokea katika miji ya Thala, Kasserine na Regueb, upande wa magharibi na katikati ya nchi. .

Taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ilisema katika miji ya Thala na Kasserine, polisi walifyatua risasi ili kujilinda baada ya wafanya fujo kushambulia majengo ya serikali.

Maandamano yalizuka kwa mara ya kwanza mwezi Desemba yakilalamikia ukosefu wa uhuru na ajira.

Shirika la habari la Tunisia official Tap limesema watu watano wamekufa kutokana na mapambano katika mji wa magharibi wa Thala usiku wa Jumamosi na watano waliuawa katika mji uliopo kando mwa Kasserine.

Taarifa hiyo iliongeza kusema kuwa majengo kadhaa ya serikali yalishambuliwa na makundi ya watu walioziteketeza benki tatu, kituo cha polisi na kituo cha petroli na gari moja la polisi.

Watu wanne waliuwawa katika mji wa Regueb, karibu na jiji la Sidi Bouzid, .

Lakini kiongozi wa chama cha upinzani cha Progressive Democratic Party, Ahmed Najib Chebbi, alisema anaamini takriban watu 20 wameuawa katika mapambano hayo.

Maandamano hayo yalianza baada ya mchuuzi mmoja kujichoma moto Desemba 17 katika eneo la Sidi Bouzid akilalamika dhidi ya kitendo cha polisi cha kukamata bidhaa zake za matunda na mboga kwa madai kuwa hakuwa na kibali.

Alifariki dunia siku ya Jumanne huku mwengine inaarifiwa alijiteketeza kwa nguvu za umeme kama sehemu ya malalamiko hayo.

Waandishi wa habari wamesema ghasia hizo za nchini Tunisia zinaelekea kuchochea maandamano kama hayo ya fujo nchini Algeria dhidi ya kuongezeka bei za bidhaa na kuilazimisha serikali ya huko kupunguza bei za bidhaa muhimu.

No comments:

Post a Comment