KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Waziri Kombani achafua hali ya hewa


Waandishi Wetu
WASOMI, wanasheria, wanasiasa, wanaharakati na wananchi wameIpinga kauli ya Waziri wa Katiba na SheriA, Celina Kombani kuwa hakuna haja ya kuwa na katiba mpya kutokana na serikali kutokuwa na uwezo wa kifedha.
Kombani, ambaye ndio kwanza alianza rasmi kazi wiki hii akiiongoza wizara nyeti inayoshughulika na sheria na katiba, alikaririwa mapema wiki hii akisema kuwa suala la kuunda katiba mpya haliwezekani kwa kuwa serikali haina fedha na kwamba itaendelea na utaratibu uliozoeleka wa kufanya marekebisho ya katiba pale inapohitajika.


Lakini kauli yake imeibua hisia tofauti kwa wananchi katika kipindi ambacho wadau mbalimbali wameanza kujitokeza kudai katiba mpya, wakiongozwa na Chadema ambayo iliweka msisitizo kwenye dai hilo kwa kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema kauli hiyo inaweza kusababisha mvurugano na kusababisha machafuko ndani ya nchi kwa kuwa kwa sasa kuna vuguvugu la kutaka mabadiliko ya katiba.
Aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, Kalistus Shekibaha alisema kauli ya Kombani inapaswa kulaaniwa na wapenda amani nchini kwa kuwa imetolewa kwa lengo la kuikandamiza demokrasia ya nchi.

“Nimemshangaa sana na kauli ya Kombani... hakupaswa kuzungumza hayo wakati ndiyo kwanza anaanza kukabidhiwa wizara; hata waliomtangulia hawakufanya hivyo,” alisema Shekibaha.
Mwanaharakati wa masuala ya walemavu, Josephat Torner alisema kauli hiyo haina lengo jema kwa mustakabali wa taifa kwa kuwa kama serikali itang’ang’ania msimamo huo wa Kombani, basi ifahamu kuwa nguvu za wananchi itabidi zichukue mkondo wake.
Aliitaka serikali kuiga mfano wa nchi ya Kenya na Zanzibar ambako hivi sasa mambo yanakwenda vizuri baada ya kurekebisha katiba.

Naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema katiba ndiyo msingi wa sheria na sera za taifa na kwamba kimsingi msimamo wa Chadema upo wazi kwamba katiba mpya ni lazima kwa wakati huu.
“Msimamo wa Chadema ni clear (wazi). Katiba mpya ni lazima, badala ya kuweka viraka tufanye ‘overhaul’ (kuandika upya katiba),” alisema Zitto, ambaye hata hivyo hakuwepo wakati wabunge wenzake wa chama hicho wakitoka kwenye ukumbi wa Bunge kupinga matokeo ya urais na kudai katiba mpya.
Zitto, ambaye ameandikiwa barua na chama chake kutaka ajieleze kutokana na kutoingia bungeni siku hiyo, alifafanua kuwa ni muhimu kwa serikali katika kutimiza miaka 50 ya uhuru ikaandika katiba mpya badala ya kuendelea kung’ang’ania katiba ambayo tayari imefanyiwa marekebisho mara 15.

“Katiba ikiwa mbovu, uchumi haukui; taifa haliendelei; wananchi hawamiliki mali; haki haziheshimiwi. Kama sehemu ya kuelekea miaka 50 ya kujitawala, ni muafaka kuangalia tulivyojitawala, katiba mpya ni sehemu ya kujiangalia huko," alisema Zitto.

"Kama Waziri amekosea... si kazi ya chama cha siasa pekee kudai, katiba ni ya watanzania ambao tayari wamefanya hivyo. Madai haya si ya kupuuzia, ni jukumu la serikali kusikiliza wananchi. Kombani kama anataka kuweka historia, akumbukwe au asikumbukwe na Watanzania kama waziri mwanamke wa sheria, aruhusu katiba mpya kuandikwa au azuie asikumbukwe,” alisema Zitto.
Mkurugenzi wa asasi ya vijana mkoa wa Tanga (Tayodea), David Chanyeghea alisema kwa sasa kipaumbele ni marekebisho ya katiba kwa sababu iliyopo ina dosari nyingi ambazo zilijitokeza hata wakati wa uchaguzi.

“Miongoni mwa malalamiko ni Tume ya Uchaguzi ambayo wajumbe wake huteuliwa na rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala na mgombea urais, matokeo yake inashindwa kufanya kazi kulingana na matakwa ya nchi,” alisema Chanyeghea.

Mkurugenzi huyo alisema suala la katiba lisichukuliwe kiitikadi kama inavyofanyika kwa kuwa ni suala nyeti na lenye mahitaji ya haraka kuliko inavyodhaniwa na baadhi ya wanasiasa.
Wanaharakati wa mauala ya kijinsia, wamesema kauli hiyo ya Kombani imewachochea moto na kwamba wanajiandaa kufanya midahalo ya kudai marekebisho ya katiba haraka iwezekanavyo.
Mmoja wa wanasheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abdallah Safari alisema kauli ya kiongozi huyo ni ya kisiasa isiyo na maana kwa Watanzania.

“Mjadala wa wananchi kudai katiba mpya, ni suala nyeti linalohitaji busara za hali ya juu katika kulizungumzia. Sasa hawa viongozi wetu kila suala wanalijibu kisiasa, gharama kubwa za kuandika katiba zinamhusu nini wakati wananchi ndiyo wanaoihitaji, na wao ndiyo walipakodi wenye fedha,” alisema.

Alisema suala la gharama halina maana kwa sababu umuhimu wa katiba katika ustawi wa nchi kuliko fedha.
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Harold Sungusia alisema kuwa Waziri Kombani hajui jukumu lake kama Waziri wa Sheria na Katiba.
“Hivi huyo waziri anajua majukumu yake kweli? Hadi sasa hajui mahitaji ya Waanzania ni nini hadi aletewe mezani? Mabadiliko ya katiba siyo lazima yaletwe kama mapendekezo. Ni jukumu la serikali kuyafanya kwa kuwa katiba iliyopo sasa ina mapungufu mengi. Ni haki ya Watanzania kuwa na katiba nzuri” alisema Sungusia.

Naye mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema kuwa hawajakosea kutoa mapendekezo yao kupitia vyombo vya habari. Alisema kuwa wataendelea kutoa mapendekezo yao hata Bungeni na kwa wananchi.
“Kwani kuyazungumzia kwenye vyombo vya habari kuna kosa gani? Tutapeleka hoja Bungeni, ikishindikana tutawapelekea wananchi. Serikali isifikiri haya ni maneno matupu ambayo hayavunji mfupa,” alisema Lissu.

Mhadhiri wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Maina alisema mabadiliko ya katiba hayahitaji mapendekezo wala shinikizo, bali ni jukumu la serikali kuyafanya.
“Si lazima yaletwe kama mapendekezo, serikali yenyewe inapaswa kuyafanya. Mbona mabadiliko ya 14 yalifanywa na serikali yenyewe? Kulikuwa na mabadiliko mwaka 2005 wakati serikali ilipoingiza vipengele vya haki za binadamu bila kusinikizwa na mtu yoyote, kwa hiyo serikali isisubiri mapendekezo,” alisema Profesa Maina.

Naye mwanasheria maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari alisema waziri huyo hajui analofanya kwa kuwa madai hayo ni ya muda mrefu lakini serikali imekuwa ikiyapuuza.
“Huyo waziri hajui kitu... mapendekezo hayo ni ya muda mrefu. Kulikuwa Tume ya Jaji Nyalali na Tume ya Jaji Kisanga, zote zilikuwa ni tume zilizoundwa na serikali na zote zilipendekeza mabadiliko ya katiba, lakini bado waziri anasema eti hakuna mapendekezo yaliyoletwa serikalini,” alihoji Profesa Safari.

Alikumbushia rasimu ya katiba iliyokuwa ikiandaliwa na vyama vya upinzani vikiongozwa na CUF, akisema kuwa hayo yalikuwa ni mapendekezo mengine ya mabadiliko ya katiba.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Felix Kibodya alimtetea Waziri Kombani akisema kuwa bado anajipanga, hivyo si rahisi kutoa jibu la kuridhisha kwa sasa.

“Ukiniuliza kuhusu mabadiliko ya Katiba nitakwambia kuwa tunayahitaji, lakini kwa sasa waziri ndiyo kwanza ameingia ofisini na rais bado anateua watendaji. Bado hatujajua hata katibu mkuu atakuwa nani. Sasa hawezi tu kusema kuwa kutakuwa na mabadiliko ya katiba; tumwache kwanza atulie”
Lakini Kibodya alisema kuwa wataandaa mapendekezo ambayo wataishauri serikali iyafanyie marekebisho.
Naye Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema chama chake kimekuwa kikipigania kuwepo kwa katiba mpya ambayo ndiyo chombo cha umma.

"Hivi visingizio vinavyotolewa na Waziri Kombani kwamba serikali haina fedha vimepitwa na wakati. Wananchi wanafahamu haki zao,” alisema.
"Katiba inayotumika hivi sasa ni zao la watu wachache ambao hata vikiwekwa viraka bado inakuwa haina manufaa kwa wananchi".

Juma Msemwa, mfanyabishara wa matunda jijini Dar es Salaam, alisema viongozi wa vyama vya upinzani wanapaswa kusimama kidete kushinikiza kuandikwa kwa katiba mpya, vinginevyo kila chaguzi zinapofanyika watakuwa walalamikaji baada ya kushindwa.

“Katiba mpya ndiyo inayoamua Tume ya Uchaguzi iundwe vipi. Wengine wanaingia kwenye chaguzi bila kufahamu haya, wanaposhindwa ndiyo wanaanza kulalamika. Unganeni kudai katika mpya kwanza, vinginevyo itakuwa vigumu kuchukua dola,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Burhani Yakub - Tanga, Raymond Kaminyoge, Elias Msuya, na Exuper Kachenje

No comments:

Post a Comment