KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Wafanyakazi Wizara ya elimu waonywa


Habel Chidawali,Dodoma

WATENDAJI wababaishaji katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wametakiwa kujisafisha wenyewe na wakishindwa watimke ili kuondoa aibu yao katika kufukuzwa.

Wito huo ulitolewa jana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Filipo Mlugo wakati akifungua mkutano wa 19 Baraza la wafanyakazi wa wizara.

Mlugo alisema hatakuwa tayari kuona watu wakiendelea kufanya kazi kwa mazoea katika kipindi hiki ambacho yeye ni naibu waziri katika wizara hiyo na kwamba kila mtu atapimwa ufanisi wake kwa vitendo.

Naibu waziri huyo alisema kuwa tangu zamani kumekuwa na tabia ya umangimeza kwa watumishi katika kazi zao hususani wale ambao wamepewa vitengo vya kusimamia wenzao jambo linalokwamisha na kurudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini.

Alisema wafanyakazi wengi wamekuwa wakifanya kazi zao kisiasa zaidi na kuacha vitendo hivyo akasema umefika wakati kila mmoja wao azidishe vitendo zaidi katika kazi yake kuliko maneno na kwamba mageuzi ya elimu hayatafikiwa ikiwa wafanyakazi wataendeleza siasa.

“Wengi wamekuwa na dharau sana katika kazi za wenzao na kubebana kumezidi jambo ninalosema kuwa iwe ni mwisho na mwiko kutokea tena maana kuna Miungu watu katika mitandao yenu ambayo ndiyo inakwamisha maendeleo yetu kazini” alisema Mlugo.

Mbunge huyo wa Songwe alisema kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imejaa watu wavivu ambao hawataki kufanya kazi kwa kujituma kama ilivyo kwa wizara nyingine na mara nyingi hawana jipya zaidi ya kueneza mbegu za chuki na ubinafsi katika maeneo yao ya kazi.

Akimkaribisha kwenye ufunguzi wa Mkutano huo wa 19, Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi Selestin Geshimba alisema kuwa baraza hilo limejizatiti katika kupunguza migogoro ya wafanyakazi pamoja na kuondoa ukiritimba kazini.

Geshimba alisema kuwa baraza limetengeneza mikakati ya kuhakikisha kuwa kila mmoja anakuwa na mpango wa mikakati katika mapinduzi ya kazi ambayo yanaweza kuifanya Tanzania ifikie katika malengo yanayotarajiwa

No comments:

Post a Comment