KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 30, 2010

Spika wa Bunge Tunisia ashika hatamu

Hali ya taharuki inaendelea kutanda nchini Tunisia siku moja baada ya Rais wa nchi hiyo kulazimika kutoroka kufuatia maandamano makubwa na fujo.

Baraza la katiba nchini humo limesema spika wa bunge Fouad Mebezza atashika hatamu za Urais kwa mudaa na uchaguzi lazima ufanyike katika kipindi cha siku sitini zijazo

Kaimu Rais wa Tunisia Fouad Mebezza


Waziri Mkuu wa Tunisia Mohammed Ghannouchi, ambaye alichukua madaraka kwa muda, ametoa wito kwa raia wa Tunisia, kusaidia kuijenga nchi hiyo kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Wanajeshi wanaendelea kulinda majengo ya serikali katika mji mkuu wa Tunis. Hata hivyo maafisa wa serikali wanasema uwanja mkuu wa ndege nchini humo umefunguliwa.

Awali, Bw Ghannouchi alisema anachukua mamlaka ya nchi na atakutana na vyama vyote vya kisiasa kujadili uundwaji wa serikali mpya.

Wakati huo huo watu walipuuza amri ya kutotembea usiku na kuandamana wakisherehekea kuondoka madarakani Rais Ben Ali, baada ya kuwa madarakani kwa muda wa miaka ishirini na mitatu.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito wa kudumishwa utulivu.

Saudi Arabia imethibitisha aliyekuwa kiongozi wa Tunisia, Zine al-Abidine Ben Ali, na familia yake wamewasili nchini humo.

Hapo awali, wakati mahali alikoelekea Rais huyo aliyelazimika kuachia madaraka kulikuwa hakujulikani. Ufaransa ilitangaza kuwa Ben Ali hatoruhusiwa kukanyaga ardhi ya nchi hiyo.

Muungano wa nchi za Kiarabu umetoa wito kwa vyama vya kisiasa nchini Tunisia, kushirikiana kudumisha amani ya nchi hiyo.

Muungano huo umetoa wito wa kuwepo kwa amani, huku ukichagiza wadau kuafikiana ili kuepusha nchi hiyo na ghasia zaidi.

Mapema msemaji wa serikali ya Qatar alisema nchi hiyo inaheshimu uamuzi wa raia wa Tunisia.


Hata hivyo mataifa mengi ya Kiarabu yamekuwa kimya kuhusiana na matukio nchini Tunisia.

Akitoa mchango wake juu ya matukio nchini Tunisia, Rais Obama wa Marekani, amewapongeza wananchi wa Tunisia kwa kile alichokiita mapambano yaliyonuiwa kudai haki kwa wote.


Alizihimiza pande zote kuepusha ghasia na kutoa wito kwa utawala wa Tunisia kufanya uchaguzi huru na wa haki.

habari zaidi kutoka Tunisia zinasema moto mkubwa katika gereza eneo la Monastir, unasemekana kusababisha vifo vya zaidi ya watu arobaini.

Mmoja ya walioshuhudia alisema gereza lote linateketea huku baadhi ya wafungwa wakitoroka.

Haijulikani kilichosababisha moto huo

No comments:

Post a Comment