KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 30, 2010

Serikali yajiandaa kuilipa Dowans

SERIKALI imeanza mchakato wa kuilipa Kampuni ya Dowans, siku chache baada ya Mwanasheria wake Mkuu (AG), Jaji Frederick Werema, kusema ameridhika na hukumu dhidi ya kampuni hiyo na kuishauri Serikali kuubeba mzigo huo.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliliambia gazeti hili juzi kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kuufanyia kazi ushauri huo wa Jaji Werema na kwamba itatoa taarifa yake wakati wowote kuhusu suala hilo. Desemba 27 mwaka huu, Jaji Werema alisema Serikali imekubali kulipa fidia ya Sh 185 bilioni kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Ltd na hivyo kuufunga mjadala kuhusu suala hilo.


“Mimi nikiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali nimeisoma hukumu hiyo kwa makini na nimeridhika nayo kuwa iko sawa,” alisema Jaji Werema alipokuwa akizungumza na gazeti hili baada ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya, Mohamed Othman Chande. Alisema “Kwa hukumu hii siwezi kusema tutalivalia njuga suala la Dowans maana kwa hukumu hii hata ukiivalia hiyo njuga itafikia mahala njuga hizo zitakatika tu,” alisisitiza Jaji Werema.

“Watu wamezungumza sana, nendeni mkaisome muone ile Dowans ni ya nani na imesajiliwa wapi, maana watu walitaka kupotosha kidogo,” alisema Jaji Werema. Juzi, Waziri Ngeleja alilieleza gazeti hili kuwa “Tayari tumemsikiliza Mwanasheria Mkuu na hatuna budi kuyafanyia kazi maagizo yake kuhusu suala hilo”.

Lakini, alipotakiwa kuzungumzia taarifa za Serikali kuanza kuwekeza Sh50 bilioni katika benki moja nchini kwa ajili ya malipo hayo, Waziri Ngeleja alisema "Sina taarifa". “Sijawahi kusikia kabisa suala linalohusiana na mambo ya kufungua hiyo akaunti ndio kwanza nakusikia wewe, silijui hilo,”alisema.




Ulipaji wa fidia hiyo unafuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhishi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker uliamuru Tanesco iilipe Dowans kiasi hicho cha fedha.

"Jopo la wasuluhishi limeamuru zaidi ya Sh36bilioni (dola za Marekani 24,168,343) na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka inayofikia kiasi cha zaidi ya Sh 26bilioni (dola za Marekani 19,995,626) tangu Juni 15, 2010 hadi fidia hiyo itakapolipwa,’ ilieleza sehemu ya uamuzi huo.

Pia jopo hilo la wasuluhishi wa migogoro ya kibiashara liliamuru Sh60bilioni (sawa na dola za Kimarekani 39,935,765) na riba ya kiasi cha asilimia 7.5 ambayo ni sawa na Sh 55bilioni (dola za Marekani 36,705,013.94) zilipwe kuanzia Juni 15, 2010 hadi wakati wa malipo.

Jopo hilo lilisisitiza kuwa ada na gharama za wasuluhishi na za utawala Sh1bilioni (dola za Marekani 750,000) kwa wasuluhishi wa ICC zinatakiwa zilipwe na pande zote husika yaani Tanesco na Dowans. "Tanesco wanatakiwa kumlipa mdai (mlalamikaji) Sh3bilioni (dola 1,708, 521) ikiwa ni gharama za uendeshaji wa kesi na gharama zingine na kwamba madai mengine yaliyotolewa na pande zote katika kesi hiyo yanatupwa.

Awali baada ya uamuzi huo kufikiwa, Tanesco ilionyesha nia kwamba ingechukua hatua za kukata rufaa, lakini tangu Jaji Werema alipoweka wazi ushauri wake uongozi wa shirika haujawahi kutoa taarifa yoyote kuhusu msimamo wake. Ends edited by Mwambona

No comments:

Post a Comment