KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 15, 2010

Polisi watawanya wanafunzi kwa mabomu Udom


Habel Chidawali na Masoud Masasi, Dodoma

VURUGU kubwa ziliibuka jana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), na kufanya eneo la chuo hicho kugeuka uwanja wa mapambano kati ya Kikosi cha Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) na wanafunzi.

Vurugu hizo zilizodumu kwa takribani saa tano, zilikolezwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Msekela kwamba, madai ya wanafunzi hao, yatatekelezwa baada ya juma moja.

Chanzo cha vurugu hizo ni madai ya fedha za mazoezi kwa vitendo ambazo wanachuo hao wanadai kuwa zimekuwa zitolewa kwa mbinde na udanganyifu mkubwa. Wanafunzi hao walifanya vurugu kuonyesha kutoridhishwa na kitendo cha wenzao wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii kutofanya mazoezi kwa vitendo hadi sasa wanapokaribia kumaliza chuo.

Madai mengine yaliyowafanya wanafunzi wapange kuandamana jana kutoka Chimwaga chuoni kwao hadi Uzunguni, Dodoma Mjini zilipo ofisi za Waziri Mkuu ni ubovu wa miundombinu, kupanda kwa bei ya chakula na uhaba wa maji.

Habari zilieleza kuwa mgomo huo ulianza baada ya kupata baraka za Bunge la wanafunzi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii, Chuo cha Sanaa na Lugha ambalo pamoja na mambo mengine liliwataka wanafunzi wote wanaoshiriki mgomo huo, kuwa na maji kwa ajili ya kukabiliana na mabomu ya machozi.

"Matatizo hayo yanayotukabili wanafunzi wa Chuo cha Sanaa na Lugha na Sayansi ya Jamii ni ya muda mrefu. Matatizo mengine ni kutokuwapo kwa mafunzo kwa vitendo kwa baadhi ya kozi, ubovu wa miondumbinu (vyuo, mabafu mifumo ya maji taka, makazi, bei ya bidhaa mbalimbali kuwa juu, kutokuwa na wahadhiri wa kutosha kwa baadhi ya kozi," ilisema taarifa ya kiongozi wa Kitivo cha Sayansi, Leonard Ringo na kuendelea:

"Wanafunzi wote wamedhamiria kufanya mgomo wa amani kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mgomo umeanza leo tarehe 20/12 mwaka 2010 saa 6:00 usiku mpaka tutakapopatiwa ufumbuzi."

Hata hivyo, wanafunzi hao waliingia kwenye mgomo huo saa 10:00 alfajiri kwa kufunga geti la lango kuu hadi saa 1:00 asubuhi baada ya askari FFU kufika chuoni hapo na baadaye mkuu wa wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa ambaye alifika majira ya saa 2:00 asubuhi.

Kutokana na hali kuendelea kuwa mbaya, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Msekela alifika eneo la tukio, lakini aliambulia kuzomewa na wanafunzi hao ambao walimtaka aondoke kwa kile walichoeleza kuwa anawaletea siasa.

“Hayo ni mambo yenu ya kisiasa, sisi tumechoka mambo ya kisiasa. Hatutakuelewa hapa hadi tukakutane na Waziri Mkuu mwenyewe, atuambie kinachoendelea vinginevyo hapatoshi hapa,” zilisikika sauti za wanachuo hao.
Baada ya kusikia hayo Mkuu wa Mkoa alikwenda kando ya eneo hilo na kumpigia simu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuomba ushauri wake kuhusu suala hilo.

“Ndugu zangu Waziri Mkuu amekubali kushughulikia maombi yenu ndani ya wiki moja kuanzia sasa. Hivyo naomba msitishe mgomo wenu hadi wiki moja itakapopita. Naomba sasa muingie madarasani,” alisema Msekela baada ya kuzungumza na waziri mkuu.

Kauli hiyo ya mkuu wa mkoa iliwaongezea hasira wanafunzi hao ambao walianza kumzomea wakisema alichowaambia ni 'danganya toto'.

Hali hiyo iliwalazimu polisi waliokuwa wamemwagwa chuoni hapo kuanza kurusha mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kazi ambayo waliifanya kwa takriban saa moja tangu saa 4:00 asubuhi.
Hata hivyo, kazi hiyo haikuwa rahisi kwani wanafunzi hao walikuwa wakijifuta kwa vitambaa vilivyowekwa maji kila bomu lilipotupwa jambo lililowalazimu polisi kuongezeka eneo hilo kuwasaidia wenzao waliokuwa wakipambana na wanafunzi hao tangu asubuhi.

Baadaye polisi hao walifanikiwa kuwadhibiti wanafunzi hao na kuwatia mbaroni sita kati yao akiwamo Ringo ambaye ni kiongozi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Udom, Profesa Idrisa Kikula hakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa yuko nje ya nchi kikazi.

Alipotakiwa kuzungumzia sakata hilo Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Shaaban Mlacha ambaye anashughulikia fedha na taaluma alisema kuwa yupo kwenye kikao na hivyo asingekuwa tayari kuzungumzia sakata hilo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Elizabeth Masaga ambaye alikuwepo eneo la tukio hilo alisema hali ilikuwa mbaya zaidi kwa vijana hao ambao walikuwa wakirusha mawe na kwamba kama hali hiyo ingeachwa bila ya polisi kutumia nguvu kungeweza kusababisha machafuko makubwa.

Hata hivyo, habari zilisema kuwa baadhi ya wananfuzi walilazimishwa kugoma na wenzao waliotambulika kama vinara wa mgomo huo.
“Kuna wengine walikuwa wakilazimisha wenzao kushiriki mgomo na wale waliokataa walipigwa na kuumizwa kama unavyomuona yule pale kwenye gari amepigwa kwa kukataa kushiriki mgomo na kuumizwa mguu hadi sasa tunasubiri gari ya kumpeleka hospitali kwa matibabu,” alisema Masaga huku akimuonyesha mmoja wa wanafunzi aliyeumia mguu ambaye alikuwa ndani ya gari la Polisi.

Mmoja wa wanafunzi hao aliambia Mwananchi, “Sisi wengine tulilazimishwa kufanya mgomo huo na kila aliyekataa alipata kichapo kutoka kwa wanachuo vinara kama mbwa mwizi. Lakini ukweli ni kuwa njia tuliyotumia katika kudai haki yetu haikuwa nzuri kabisa.”

No comments:

Post a Comment