KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, October 6, 2010

Ghailani "alitishwa kutaja shahidi"


Jaji katika kesi ya kwanza kabisa ya kiraia dhidi mfungwa kutoka gereza la Guantanamo, ametoa uamuzi kuwa shahidi mkuu kutoka serikali ya Marekani hatotoa ushahidi.

Hatua hiyo ni pigo kwa waendesha mashitaka.

Mshukiwa huyo Ahmed Khalfan Ghailani anakanusha kusaidia kundi la Al Qaeda kufanikisha mauaji ya watu 224 mwaka 1998 katika balozi za Marekani zilizoko Afrika Mashariki.

Jaji huyo ametoa uamuzi kuwa shahidi huyo wa serikali hatotoa ushahidi, kwa sababu Bw. Ghailani alimtaja shahidi huyo wakati akiwa "chini ya vitisho".

Mwandishi wa BBC anasema hatua hiyo inazidi kuongeza ugumu katika mipango ya kutaka kuwashitaki washukiwa na Guantanamo katika mahakama za kiraia.

Utawala wa Rais Obama una matumaini ya kuendesha kesi hizo kwa washukiwa kadhaa, hasa wenye 'majina makubwa', akiwemo Khalid Sheikh Mohammed anayetuhumiwa kupanga mashambulio ya Septemba 11 nchini Marekani.



Vitisho

Jaji Lewis Kaplan wa New York ameahirisha kesi ya Bw. Ghailani iliyokuwa ianze kusikilizwa Jumatano.Kesi hiyo sasa iko katika hatua ya kutafuta wazee wa mahakama itakayofanyika Oktoba 12.

Katika uamuzi wake, jaji huyo wa New York amesema shahidi huyo wa serikali aliyependekezwa, alitajwa katika "taarifa alizotoa Ghailani kwa CIA wakati akiwa katika vitisho".


Taswira ya mchoraji ya Ghailani mahakamani

Mtu huyo, Hussein Abebe, alitarajiwa kutoa ushahidi kuwa alimuuzia Ghailani milipuko ya TNT, ambayo ilitumika katika mlipuko wa bomu katika ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, mwezi Agosti mwaka 1998.

Uamuzi huo, iwapo hautabatilishwa, ni kikwazo kwa kesi ya serikali ya Marekani dhidi ya Ahmed Khalfan Ghailani, na pia hatua hiyo kutatiza zaidi sera ya utawala wa Obama wa kuwashitaki washukiwa wa Guantanamo katika mahakama za kiraia.

Shahidi mkubwa

Hussein Abebe alitarajiwa kutoa ushahidi. Bila ya shahidi huyo kutoa ushahidi wake, serikali itapata tabu kuwasilisha ushahidi wake mbele ya wazee wa mahakama. Hatua hiyo inawapa waendesha mashitaka tatizo kubwa -- iwapo ushahidi uliopatikana katika magereza ya CIA au gereza la Guantanamo hauwezi kutumika katika mahakama ya kiraia, je kuna uwezekano wa kukuta mshukiwa na hatia?.

Mwendesha mashitaka mmoja wa Marekani amemuelezea Bw. Abebe kama shahidi "mkubwa" kwa serikali, na wanafikiria kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa jaji.

Bw. Ghailani, ambaye inaaminika umri wake ni kati ya miaka thelathini na arobaini , alikuwa amevaa sweta la rangi ya kijivu, suruali nyeusi na tai, wakati alipofikishwa mahakamani, siku ya Jumatano.

Kifungo cha maisha

Bw. Ghailani anatuhumiwa kununua gari la milipuko iliyotumika katika shambulio nchini Tanzania, na pia kutuhumiwa kuwa mjumbe wa Osama Bin Laden. Anakanusha mashitaka hayo.

Bw. Ghailani aliyekamatwa nchini Pakistan mwaka 2004, alipelekwa kisiri katika kituo kimoja cha CIA kabla ya kupelekwa Guantanamo mwaka 2006.

Bw. Ghailani anakabiliwa na kifungo cha maisha jela, iwapo atakutwa na hatia.

No comments:

Post a Comment