KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, August 28, 2010

Mwanamke wa Kisomali afungwa kwa utekaji





Mwanamke wa Kisomali afungwa kwa utekaji

Mwanamke wa Kisomali aliyejaribu kuteka ndege ndogo inayofanya safari za ndani huko New Zealand mwaka 2008 amehukumiwa kifungo cha miaka tisa jela.

Katika tukio la kwanza la aina yake huko New Zealand, Asha Ali Abdille alipanda ndege hiyo akiwa na visu vitatu ambapo alijaribu kuwalazimisha marubani waelekee Australia.

Alipoambiwa ndege hiyo haikuwa na mafuta ya kutosha aliamuru ipelekwe kwenye bahari.

Ndege hiyo ilitua kwa salama kwenye mji wa Christchurch na alizidiwa nguvu na wafanyakazi wa ndege hiyo.

Abdille, mkimbizi mwenye umri wa miaka 36, aliwafuata marubani takriban dakika 10 baada ya ndege hiyo kupaa na kudai ana mabomu mawili.

Alikuwa karibu tu afanikiwe kusababisha ajali ya ndege hiyo alipoanza kuingilia shughuli za uendeshaji wa ndege hiyo.
Kutafakari upya njia za usalama

Alipokataliwa ombi lake la kubadilisha mwelekeo wa safari, aliwashambulia marubani na abiria mmoja, akihimiza ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 19 itue baharini.

Gazeti la kila siku la Christchurch, the Press, liliripoti kuwa abiria saba waliokuwemo kwenye ndege hiyo walibaki kwenye viti vyao.

"Walikuwa na hofu na wengi wa abiria walikuwa wakilia." Rubani alisema, " Wakati mmoja alisema sote tutakufa. Hakusema tutakufa vipi."

Abiria mmoja wa kike alimwelezea Abdille kama aliyefadhaishwa : "Kuna wakati unamwona ana hamaki, nyakati nyingine kama ana woga, mara analia na kufuta machozi yake."

Rubani huyo alifanyiwa upasuaji mkubwa wa kuunganisha upya kano, misuli na neva baada ya kukatwa mikono yake yote miwili.

Abdille amekuwa akiishi Blenheim kwa miaka mitano, akifanya kazi kwenye shamba la mizabibu.

Aliwahi kushtakiwa kwa kutishia kummwagia petroli mfanyakazi mmoja wa shirika la msalaba mwekundu Red Cross huko Wellington na kumrushia polisi ndoo yenye kinyesi huko Hastings na tayari alikuwa nje kwa dhamana kwa kosa jengine.

Hakimu Christine French alisema, wakati wa hukumu, suala la matatizo ya akili lilizingatiwa.

Bado haijajulikana kwanini alitaka ndege hiyo ibadilishe mwelekeo wake wa safari.

No comments:

Post a Comment