KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, August 28, 2010

Mauaji ya Congo 'huenda ni ya kimbari'

Ripoti iliyotayarishwa na Umoja wa Mataifa inasema kuwa uhalifu uliofanywa na jeshi la Rwanda na washirika wake katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inaweza kuwekwa katika fungu la mauaji ya kimbari.

Ripoti hiyo, iliyosomwa na BBC inatoa maelezo ya undani kuhusu uchunguzi uliofanywa nchini Kongo kuanzia mwaka 1993 hadi 2003.

Inasema kuwa maelfu ya Wahutu wakiwemo wanawake, watoto na wazee waliuawa na Jeshi la Rwanda lenye askari wengi wa kabila la Kitutsi.

Wakimbizi wa Rwanda

Waziri wa sheria wa Rwanda amekanusha madai hayo akiyaelezea kama ''upuuzi mtupu''.

Ripoti hiyo vile vile inaorodhesha ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya nchi nyingine zilizoshiriki kilichokuja kujulikana kama ''Vita vya kwanza vya Afrika''.

Ripoti kamili ya shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa itachapishwa hivi karibuni. Ingawaje mgogoro huo umemalizika rasmi, hali katika eneo la mashariki mwa Kongo lililopakana na Rwanda bado ni ya wasiwasi.

Siku ya Alhamisi, Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa na kikao cha dharura kujadili madai kuwa waasi wa Kihutu walikuwa miongoni mwa watu waliobaka takriban wanawake 150 pamoja na wavulana katika mji wa Luvungi na vitongoji vilivyo karibu yake mapema mwaka huu.

Ripoti hiyo yenye kurasa 545, iliyotayarishwa na maofisa 20 wa shirika la haki za binadamu, inaorodhesha kilichoitwa mashambulio yaliyopangwa na kutekelezwa na jeshi la Rwanda pamoja na waasi wa AFDL.

Waasi hao wa AFDL walikuwa wakiongozwa na Laurent Kabila, baba yake Rais aliye madarakani Joseph Kabila.

Walengwa wa mashambulio hayo walikuwa Wahutu wa Rwanda waliokimbilia katika nchi inayojulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati huo ikijulikana kama Zaire, baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Ikumbukwe kuwa wakati huo Wahutu wenye msimamo mkali waliua takriban Watutsi 800,000 pamoja na Wahutu wenye misimamo ya wastani.

Walioshiriki mauaji waliikimbia Rwanda wakati wakitimuliwa na Watutsi waliokuwa waasi.
'Shinikizo dhidi ya Rwanda'

Ripoti hiyo inasema kuwa mashambulizi dhidi ya Wahutu ambao hawakuwa wakimbizi yanaonekana kuthibitisha kuwa hata Wahutu ambao ni raia wa Kongo pia walilengwa.

Katika maeneo kadhaa, inasema ripoti hiyo, vizuizi viliwekwa kwa ajili ya kuwasaka na kuwatambua Wahutu, na kuwaua.

Serikali ya Rwanda imejibu vikali madai ya ripoti hiyo kama ilivyofanya kuhusu ripoti za awali kwamba vikosi vyake vilishiriki mauaji ya kimbari ya Wahutu nchini Rwanda baada ya kushika hatamu za uongozi kukomesha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Mara kwa mara Rwanda imesisitiza kuwa iliingia nchi ya Zaire kuwasaka wanamgambo wa Kihutu walioshiriki mauaji ya kimbari.

Waziri wa Sheria wa Rwanda Tharcisse Karugarama ameiambia BBC kuwa madai ya ripoti hiyo hayana msingi.

Waziri huyo ameongezea kuwa, ndiyo sababu imepingwa moja kwa moja, haina thamani yoyote, na hata nchi zilizotajwa zimeipinga pia.

Mwandishi wa BBC wa Afrika ya magharibi Thomas Fessy aliyeiona ripoti hiyo, alisema kuwa duru zilizo karibu na upelelezi zinasema viongozi wa Rwanda wameshinikiza Umoja wa Mataifa upunguze makali yaliyomo katika ripoti hiyo.

Gazeti la Le Monde nchini Ufaransa limesema kuwa Rais wa Rwanda Paul Kagame ametishia kuondoa vikosi vya nchi yake kutoka shughuli ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika jimbo la Sudan la Darfur.

No comments:

Post a Comment