KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, August 28, 2010

Kenya yakosolewa juu ya ziara ya Al-Bashir


Kenya imekosolewa kwa kumwalika Rais wa Sudan Jenerali Omar al-Bashir, kwenye sherehe za kuzindua katiba mpya ya nchi hiyo siku ya Ijumaa.

Rais Barack Obama wa Marekani alisema alihuzunishwa na hatua ya Kenya.

Rais Bashir anatakikana kwa makosa ya uhalifu wa kivita na mauaji ya kuangamiza katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC imewasilisha repoti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Kenya juu ya hatua yake ya kushindwa kumkamata Jenerali al-Bashir alipowasili mjini Nairobi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alisema mataifa yote ambayo yalitia saini mkataba wa Rome uliounda mahakama ya ICC yana wajibu wa kushirikiana na mahakama hiyo, wazo ambalo pia liliungwa mkono na Muungano wa Ulaya.

Afisa mkuu wa Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Kenya, Muthoni Wanyeki ni miongoni mwa watu walioishutumu serikali ya Rais Kibaki kumwaalika kiongozi huyo wa Sudan.

Wanyeki amekaririwa akisema " Ni aibu kwa Wakenya ambao waliuchagua utawala ambao unatakiwa kusimamia hazi za binadamu na badala yake wamekiuka hilo, jambo ambalo dhahiri linaashiria mwisho wa kuwaadhibu wakosaji si tu nchini Kenya bali katika ukanda huu wa Afrika.

Amesema, "Si mwanzo mwema wa utekelezaji wa katiba mpya. Katiba Mpya inabainisha wazi kuwa tunawajibika kutekeleza mikataba yote ya kimataifa ambayo tumeridhia, ikimaanisha tunalazimika kushirikiana na mahakama hiyo ya ICC."

Hata hivyo, serikali ya Kenya imetetea uamuzi wake wa kumwalika Rais Omar al Bashir, kuhudhuria sherehe hizo.

Akizungumzia wito wa kuitaka Kenya kumkamata Rais huyo wa Sudan, Waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Moses Wetangula, amekaririwa akisema, Rais Bashir yupo nchini hapa kwa mwaliko uliofanywa na serikali ya Kenya kwa jirani zake wote kuwaomba kuhudhuria tukio hili la kihistoria.

Bw Wetangula amesema, "Kenya haijavunja sheria yoyote na ni nchi huru, hivyo ina haki ya kumwalika yeyote inayetaka aje hapa nchini."

No comments:

Post a Comment