KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, June 24, 2010

Wabunge Nigeria waumizwa bungeni


Mbunge mmoja Nigeria amevunjika mkono katika fujo zilizotokea bungeni.

Solomon Ahwinahwi ni mmoja wa wawakilishi wanaojaribu kumlazimisha spika aachie madaraka.

Amejeruhiwa wakati vurugu zilipoanza baada ya wafuasi wa spika walipojaribu kutoa mapendekezo ya muswada kuwasimamisha kwenye bunge la wawakilishi.

Mwakilishi mwengine, Doris Uboh, naye alijeruhiwa. Bw Ahwinahwi ametibiwa katika kliniki moja ya bunge hilo kabla ya kupelekwa hospitali.

Mwandishi wa BBC Mohammed Aba mjini Abuja amesema polisi wamejaribu kuwakamata wapiga picha wawili waliopiga picha za fujo lakini baadae waliachiwa huru.

Anasema kundi linalojaribu kumwondoa spika Oladimeji Bankole linajulikana kama Progressives. Wametoka chama tawala cha People's Democrat.

Siasa za Nigeria ziko katika hali tete tangu baada ya kifo cha Rais Umaru Yar'Adua mwezi Mei.

Mpaka sasa haijajulikana iwapo mrithi wake Goodluck Jonathan atawania urais kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mapema 2011.

No comments:

Post a Comment