KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, June 30, 2010

Kiongozi wa FNL Agathon Rwasa mafichoni

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Burundi ambaye zamani alikuwa kiongozi wa kundi la waasi Agathon Rwasa ,amethibitisha kuwa yuko mafichoni.

Kwenye ujumbe uliorekodiwa na kutumwa kwa radio moja nchini humo, Bw Rwasa amesema amejificha kwa kuhofia usalama wake.








Aliondoka nyumbani kwake wiki moja iliyopita kabla ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumatatu huku mgombea pekee akiwa Rais wa sasa Pierre Nkurunziza .

Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza kufanyika nchini humo,tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 12.

Wanadiplomasia wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikarejea katika hali ya mzozo wa kivita.

Waandishi wa habari wanasema idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo wa urais, ilikuwa ndogo ikilinganishwa na uchaguzi wa mikoa uliofanyika mwezi uliopita.

Wananitafuta kwasababu nilisema ukweli,nilisema wazi kuwa sitakubali matokeo ya uchaguzi wa mikoa, walitaka kunikamata na nilipopata fununu nikaamua kukimbia

Kiongozi wa chama cha FNL Agathon Rwasa

Vyama vitano vya upinzani vilidai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura, na vikajiondoa katika uchaguzi wa urais.

Bw Rwasa, ambaye alitia saini mkataba wa amani mwaka jana, hakusema yuko wapi lakini inaripotiwa kuwa yuko katika nchi jirani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wakati alipotoweka kwa mara ya kwanza ,chama chake kilisema alikuwa ''likizoni''.

Bw Rwasa na Rais Nkurunziza ,waliongoza makundi ya waasi wa Kihutu kupigana na jeshi ambalo lilikuwa likiongozwa na Watutsi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Bw Rwasa, alikataa kuhusika katika mpango wa kumaliza mapigano baada ya makundi yaliyokuwa yakizozana kuamua kuunda serikali ya muungano na baadaye uchaguzi ukafuata mwaka 2005.

Aliongoza kundi la National Liberation Forces (FNL) kusalimisha silaha mwezi Aprili mwaka 2009, na anaaminika kuwa mshindani mkubwa wa Rais Nkurunziza.

Watu wapatao 300,000 walikufa wakati wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

No comments:

Post a Comment