KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, June 24, 2010

Idadi ya vifo vyaongezeka ajalini Congo


Maafisa wamesema zaidi ya watu 75 wamefariki dunia katika ajali ya treni kaskazini mwa Congo-Brazzaville.

Mkuu wa reli, Chemin de Fer Congo-Ocean (CFCO), amesema ajali hiyo ilitokea siku ya Jumatatu usiku takriban kilomita 60 kutoka mji wa Pointe-Noire.

Treni hiyo ilitoka katika reli wakati ikikata kona katika kijiji kimoja baina ya Bilinga na Tchitondi, na kuangusha mabehewa manne kwenye makorongo.

Maafisa wanasema huku shughuli za uokoaji zikiendelea idadi ya waliokufa inatarajiwa kuongezeka.

Shirika la habari la AFP limenukuu msemaji wa serikali Bienvenu Okiemy akisema, "Kulingana na hali halisi, kasi kubwa ndio sababu kuu ya ajali hii ya treni."

Bw Okiemy amesema siku tatu za maombolezo zitaanza siku ya Jumamosi na serikali italipa gharama zote za mazishi.

Amesema shughuli za kunyanyua mabehewa yaliyoanguka kwenye makorongo zinaendelea.

Mkurugenzi mkuu wa CFCO Sauveur Joseph El Bez ameiambia AFP kwamba idadi ya waliofariki dunia bila shaka itaongezeka "kutokana na treni kujaa kupita kiasi."

Amesema, " Kulikuwa na abiria wengi sana."
Matunzo hafifu

Congo Brazzaville

Watu waliofariki dunia na waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini na maeneo ya kuhifadhi maiti huko Pointe-Noire.

Afisa mmoja ambaye jina lake halikutajwa katika kitengo cha kupamana na maafa huko Pointe-Noire ameiambia AFP kuwa, " Asubuhi hii, idadi mpya ya waliokufa ni 76. Miili yao ipo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti huko Pointe-Noire."

Mwandishi wa BBC Will Ross amesema reli hiyo yenye urefu wa kilomita 500 ilijengwa katika miaka ya 1920 na 1930 wakati nchi hiyo ilipokuwa koloni la Ufaransa.

Maelfu walifariki dunia wakati wa mradi huo.

Waandishi wetu wanasema, tangu wakati huo reli hiyo imekuwa haifanyiwi matunzo vizuri.

Reli nzima hiyo kutoka mji mkuu Brazzaville na Pointe-Noire ilifungwa katika miaka ya 90 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Kumekuwa na takriban ajali mbaya mbili tangu reli hiyo ifunguliwe upya.

Hii ni ajali ya pili kutokea katika siku za hivi karibuni. Ndege moja iliyobeba wakurugenzi kutoka Austarlia wanaoshughulikia masuala ya migodi mwishoni mwa juma ilianguka, na kusababisha vifo vya watu wote 11 waliokuwemo kwenye ndege hiyo.

No comments:

Post a Comment