KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 3, 2010

Waasi Somalia wavamia 'kambi' ya maharamia

Waasi Somalia wavamia 'kambi' ya maharamia
Waasi wa Kisomali wamedhibiti moja ya miji inayotumiwa na maharamia kama maficho yao, kusini mwa Somalia.
Wakazi wa huko wamesema mamia ya wapiganaji wa kundi la Hizbul Islam, wamechukua udhibiti wa mji wa mwambao wa Haradhere. Wakazi hao wamesema maharamia wameukimbia mji.

Kiongozi wa kundi hilo ameiambia BBC kuwa Hizbul Islam inataka kuanzisha matumizi ya sheria za Kiisilam, Sharia, ili kuleta hali ya utaratibu na kumaliza harakati za uharamia.

Somalia haijakuwa na serikali thabiti kwa karibu miaka 20.
"Karibu wanamgambo 200 wakiwa na silaha nzito wameingia mjini humo alfajiri ya leo na kuteka maeneo muhimu kama vile kituo cha polisi na maeneo ya zamani ya serikali," amesema Aden Jim'ale, mkazi wa Haradhere.



"Tumeingia Haradhere sasa, tumekuja baada ya wakazi wa hapa kutuomba tuje kuwalinda," mkuu wa shughuli za kijeshi wa Hizbul Islam, Mohamed Abdi Aros ameiambia BBC.

Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu, Mohammed Olad Hassan amesema hatua ya Hizbul Islam kuingia Haradhere inaongeza tishio la jitihada za kundi la waasi kutaka kumaliza biashara ya uharamia.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa kutoka kwa maharamia zinasema, ujumbe wa kundi la Hizbul Islam ulitembelea mji huo siku chache zilizopita na kudai kupatiwa makato ya fedha yatokanayo na biashara ya uharamia.

Katika miaka ya hivi karibuni, maharamia wameteka meli nyingi katika Bahari ya Hindi na katika
Ghuba ya Aden.

Maharamia hao hivi karibuni wamekuwa wakifanya utekaji wao mbali zaidi, ili kuepuka meli za doria zinazoranda katika mwambao wa Somalia.

No comments:

Post a Comment