KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, May 6, 2010

Serikali yazuia maandamano Tanzania


Serikali ya Tanzania siku ya Jumatano ilizuia maandamano ya wanaharakati zaidi ya 500 wa masuala ya afya na UKIMWI kutoka nchi mbalimbali za Afrika. Wanaharakati hao walipanga kuandamana wakati Kongamano la Uchumi Duniani kwa bara la Afrika likianza nchini humo, ili kuwashikiza viongozi wa dunia kushughulikia masuala ya afya hususan UKIMWI.

Jeshi la polisi limesema wanaharakati hao wana njia nyingine ya kufikisha ujumbe wao tofauti na maandamano, na kwamba Tanzania ina taratibu zake za ulinzi na usalama. Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati hao, wameweza kujipenyeza hadi eneo unapofanyika mkutano huo na kumkabidhi ujumbe wao mwanamuziki wa Afrika Kusini, Yvonne Chaka Chaka, ili awe balozi wao.

Jeshi la polisi linasema ingawa wanaharakati hao waliomba kibali cha kufanya maandamano hayo, lakini wameona kuwa hawakuona sababu ya kufanya maandamano kwa sababu waliwatilia mashaka kuhusu masuala ya usalama. “Isitoshe siyo sahihi mpaka wangoje mkutano ambao unashughulikia uchumi ndiyo wawe na maandamano. Na hawakuwa katika utaratibu wetu wa usalama,” Kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar Es Salaam, Suleiman Kova, alieleza.

Kufikisha ujumbe

Baada ya kutii amri hiyo tangu asubuhi, wanaharakati hao mnamo saa 11 jioni, walifika katika eneo hili la Mlimani wakiwa kama kondoo waliomwagiwa maji ili wapate fursa ya kumwona Yvone Chaka Chaka.

Hata hivyo iliwachukuwa dakika kadhaa kuwashawishi walinzi kupita. Baada ya msuguano mkubwa Yvone mwenyewe anayehudhuria mkutano huu wa uchumi, alilazimika kutoka nje ya na kuwasikiliza pembeni mwa mlango wa kuingilia.

Ujumbe umewakilishwa na mkurugenzi wa kanda wa taasisi inayoshughulikia masuala ya afya kusini mwa Afrika, Paula Akugizibwe. Katika ujumbe wake huo Paula amesema iwapo viongozi wa dunia wanatambua kuwa masuala ya afaya ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya watu, kwa nini wasitimize malengo ya milenia kwa njia ya kutoa ya huduma bora?

Ahadi ni deni

Na kwa viongozi wa mataifa makaubwa kama Marekani wamewataka kuhakikisha wanatimiza ahadi yao ya kuchangia mfuko wa kupambana na magonjwa sugu duniani, ili waweze kuokoa maisha ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI au wanaougua ugonjwa huo ambao wengi wao wako Afrika.

Yvone amepokea ujumbe wao na kusema kuwa mkutano wao hauwezi kuwa na maana kama hawawezi kuwasikiliza watu wanaowatumikia, ambao waliwapatia kura. Akasema mikutano haiponyi matatizo ya watu bila kuwasikiliza. Kwa hiyo anasema atafanya kila awezavyo kuufikisha ujumbe wao kwa viongozi wa Afrika.

Lakini serikali imesema mambo yaliyowahi kufanywa na wanaharakati wengine katika mkutano ya dunia, siyo lazima yafanyike Tanzania.

No comments:

Post a Comment