KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, May 6, 2010

Mkutano wa hali ya hewa Bonn

Jitihada za kufikiwa makubaliano ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yamepiga hatua katika mkutano huo wa kimataifa unaomalizika hii leo.

Ujerumani imesema mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa unaonekana kupiga hatua katika kupatikana makubaliano ya kukabiliana na ongezeko la ujoto duniani, ingawa masuala muhimu bado yanaonekana hayajapatiwa ufumbuzi.

Akizungumza katika mkutano huo unaoangalia njia za kufufua mazungumzo ya hali ya hewa unaofanyika mjini Bonn, Ujerumani, Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, Norbert Roettgen, amesema kuwa wajumbe wa mkutano huo wamekubaliana katika juhudi za kumaliza tofauti zilizokuwepo baada ya mkutano mkuu wa hali ya hewa uliofanyika mwaka uliopita mjini Copenhagen, Denmark, kutofikia makubaliano ya msingi.

Akizungumza na waandishi habari, Waziri Roettgen amesema kuwa makubaliano juu ya kulinda misitu na kubadilishana teknolojia ya hali ya hewa kutoka mataifa tajiri kwenda mataifa masikini, yanakaribia kufikiwa. Amesema ana matumaini masuala hayo yatakamilishwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa uliopangwa kufanyika huko Cancun, Mexico, mwezi Novemba mwaka huu.

Aidha, waziri huyo wa mazingira wa Ujerumani amesema makubaliano kuhusu kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira pamoja na msaada wa fedha kwa nchi masikini bado ni masuala ambayo yanajadiliwa. Baada ya kukatishwa tamaa na mkutano wa Copenhagen, mawaziri wa mazingira sasa wataangalia kati ya malengo makubwa mno au ya kawaida ambayo yanatakiwa kufikiwa katika mkutano wa Cancun.

Jose Romero, mpatanishi wa ngazi ya juu wa hali ya hewa nchini Uswisi na mkongwe wa mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa, amesema kuwa mkutano wa Copenhagen ulikuwa wa kuangalia hali halisi. Romero ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa wanazingatia zaidi kiini, kwani wanataka mabadiliko halisi kabla ya kuzungumzia kuhusu mkataba wenyewe.

Akizungumza jana katika mkutano huo, Mkuu wa kitengo cha hali ya hewa cha Umoja wa Mataifa, Yvo de Boer alielezea matumaini yake kuwa majadiliano yaliyokwama juu ya mabadiliko ya hali ya hewa sasa yanaeza kuanza tena, licha ya kushindwa kwa mkutano wa Copenhagen.

Mkutano huo wa siku tatu unaojulikana kama ''Majadiliano ya hali ya hewa ya Petersberg'', ni mkutano wa ngazi ya juu wa hali ya hewa tangu ule wa mwezi Desemba wa Copenhagen uliozusha mivutano unamalizika hii leo. Mkutano huo uliohudhuriwa na kiasi mataifa 40, ulifunguliwa kwa pamoja na Ujerumani na Mexico ambayo itakuwa mwenyeji wa mkutano huo wa mwezi Novemba.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri: Othman, Miraji

No comments:

Post a Comment