KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, November 25, 2009

Vinyonga wapya wagunduliwa Tanzania


Vinyonga wapya wagunduliwa Tanzania

Mwanasayansi mmoja wa Uingereza aliyekuwa akifanya utafiti wa viumbe hai katika msitu wa Magombera huko Tanzania ametangazwa rasmi kugundua aina mpya ya vinyonga ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani isipokuwa Tanzania.
Dr Andrew Marshall kutoka chuo kikuu cha York nchini Uingereza alimgundua mnyama huyo ambaye hatimaye alipewa jina la ni Kinyongia magomberae, miaka minne iliyopita, lakini sasa ndiyo amethibitishwa rasmi na wataalam wenzie.


Kinyongia magomberae aliyegunduliwa na Dr Andrew Marshall. Picha kwa hisani ya Andrew Marshall.



Dr Andrew Marshall, mwanaikolojia kutoka chuo kikuu cha York, ameieleza BBC kuwa alikuwa akifanya utafiti wa mbega wekundu, ndipo siku moja alipokumbana na nyoka ambaye alishtuka na kumtema kinyonga huyo miguuni mwake na kukimbia.

Ingawa mwenzake alimshauri asimguse kutokana na wasi wasi wa kuathirika na sumu ya nyoka, Dr Marshall alihisi kiumbe huyo alikuwa mpya machoni mwa wanasayansi akampiga picha na kuwatumia wenzake ambao walithibitisha aliyokuwa akifikiria.

Kinyongia magomberae

Kinyongia magomberae, ikiwa na maana ya "kinyonga wa Magombera", ni matokeo ya mkasa huo na akaieleza BBC kwamba haikuwa rahisi kwake kumtambua ndiyo maana akavutiwa kumchunguza.

"Unajua, rangi si kigezo kizuri kuwatofautisha vinyonga, kwasababu wanabadilika rangi kutokana na mazingira. Kwa kawaida hutambuliwa kutokana na maumbile ya vichwa vyao, na mpangilio wa magamba. Kwa tukio hili ilikuwa ni magamba yaliyotuna juu ya pua yake."

Kwa bahati njema, Dr Marshall alifanikiwa kumwona kinyonga wa pili akiwa hai na alifanikiwa kumpiga picha.

Viumbe hao walipatikana umbali wa kilometa 10 kutoka kila mmoja, jambo linalomfanya aamini inaweza kuwa umbali halisi wa eneo linalokaliwa na Kinyongia magomberae.

Utafiti

Ingawa aliwagundua viumbe hao mwaka 2005, nyaraka zake za utafiti zilizochapishwa Novemba 2009, zinatambulisha rasmi uvumbuzi huo.

"Inachukua muda mrefu kuzishawishi mamlaka kuwa umevumbua aina mpya ya viumbe," alieleza.

"Tulipowasilisha matokeo ya ufafiti wetu kwa wanakijiji wa eneo hilo walifurahishwa kwamba dunia sasa inatambua mnyama huyo kwa jina la kienyeji Magombera," alisema.

Magombera ni msitu wa asili ulioko eneo la hifadhi ya Udzungwa mpakani mwa mikoa ya Morogoro na Iringa.

No comments:

Post a Comment