KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, October 14, 2009

WASOMI nchini na baadhi ya nchi za Afrika, wamesema mfumo wa utawala wa nchi za bara hilo, Tanzania ikiwamo


WASOMI nchini na baadhi ya nchi za Afrika, wamesema mfumo wa utawala wa nchi za bara hilo, Tanzania ikiwamo, unawatenga watawala na watawaliwa.

Wamesema hali hiyo inajionyesha katika njia mbalimbali, lakini hasa katika uchumi ambako watawala huangalia maslahi yao zaidi kuliko ya wanaowaongoza, kwa mfano, kwa viongozi kujilipa posho kwa kulinganisha na wenzao wa nchi zilizoendelea, na si kwa kulinganisha hali halisi ya wananchi wao.

Kwa mujibu wa wasomi hao, wananchi wa kawaida sasa wanazidi kutupwa nje ya uzio wa utajiri wa nchi zao, wakati viongozi wakizidi kujiimarisha katika himaya ya kupora rasilimali za nchi husika na kujinufaisha.





Mwalimu Nyerere
Hata hivyo, katika kuonyesha hali ya kutokata tamaa, wakizungumza katika tamasha la wiki la kazi za kisomi la Mwalimu Julius Nyerere, sehemu ya Mlimani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wasomi hao walisema bado Afrika inaweza kujisahihisha.

Kwa upande wake, mhadhiri mwandamizi wa UDSM, Profesa Mwesiga Baregu, alisema matukio yanayoendelea kuibuka nchini yanaiweka jamii katika hali ya wasiwasi huku nchi ikipoteza upeo na mustakabali wake pia ukiwa haueleweki.

“Matukio mengi kama ya ufisadi, udhaifu wa kiutawala na usimamizi mbovu wa misingi ya demokrasia…yote haya yanatufanya kama Taifa kujikuta katika shinikizo la kutafuta mustakabali wetu upya,” alisema Profesa Mwesiga akiongeza:

“Tamasha hili limekuja wakati mwafaka kwa kuwa tunapata fursa ya kufikiri ndani ya mawazo ya Mwalimu Nyerere. Tunatafakari iweje wakati ule tulikuwa na viwanda na maendeleo mengine lakini leo hii tumepoteza.”

Kwa mujibu wa Profesa Baregu, ni lazima Tanzania ijihami kwa mbinu zote zikiwamo za kifikra, hasa ikizingatiwa kuwa ulimwengu hauna huruma dhidi ya Taifa lisilo na mustakabali unaofahamika kwa wananchi wake wote.

Naye mhadhiri msaidizi wa UDSM, Idara ya Sayansi ya Siasa, Bashiru Ali, alisema kwa sababu Tanzania ilizubaa kuchangamka katika kujijengea nguvu za kufaidika na rasilimali zake, Benki ya Dunia (WB) na wadau wengine wa kimataifa waliingia nchini wakiwa na mawazo yaliyoziba pengo hilo la uzubaifu wa Taifa kifikra.

“Kinachofanyika ni kwamba wenzetu kwa mfano Benki ya Dunia wamekuja kwetu na ajenda-wamekuja na mawazo hawakuja kwa mabavu kama wakati ule wa ukoloni.

“Wakaja wakapendekeza tupunguze wafanyakazi, lakini leo hii tunalazimika kuongeza umri wa kustaafu…utaona Structural Adjustment Program ilivyopokewa nchini wakati ule wa Rais Ali Hassan Mwinyi,” alisema.

Alishauri kuwa ni busara zaidi sasa kuwa na mawazo mbadala na kwamba kwa kuwa nchi imetumbukia katika dunia ya jamii isiyokuwa na mwelekeo ni lazima kusaka mwelekeo.

“Mfumo wa kiutawala nchini pia umekuwa ukiwatenganisha viongozi na wananchi kiuchumi na katika nyanja nyingine. Viongozi wamekuwa wakijilipa posho kubwa kwa kulinganisha na wenzao wa nchi nyingine na si kwa kuangalia maisha ya watu wao,” alisema Bashiru.


Katika kuonyesha kuvutiwa na mwenendo wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mhadhiri huyo alisema; “Nyerere amekufa hakuacha majengo, barabara nyingi au vyuo vikuu…aliacha ideas na ndiyo maana leo hii anaheshimika kuliko hao wanaojenga barabara na majengo….ukweli ni kwamba watu wana-win by ideas.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu msaafu, Jaji Joseph Warioba alionyesha kukerwa na tabia ya sasa ya viongozi kuzungumza zaidi kuliko kutenda akirejea mwenendo wa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa akifanya yote mawili kwa pamoja na matokeo yake yakathibitishwa na wananchi.

Alitofautiana na msimamo wa baadhi ya viongozi kuamini kuwa suluhu ya matatizo ya Taifa ni kuomba ufadhili kutoka nchi tajiri, huku wakiachia mianya ya uvujaji wa rasilimali za nchi ikibaki wazi.

Katika maelezo yake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ibadan nchini Nigeria, Profesa Wole Soyinka, alisema Afrika bado inakabiliwa na ubeberu mamboleo na kwamba ni lazima ubeberu huo upigwe vita kwa njia ya Afrika kuwa na nguvu za pamoja.

Wasomi wengine waliozungumza na kuonyesha kuunga mkono mawazo ya Mwalimu Nyerere mbali na Profesa Soyinka, ni pamoja na Profesa Issa Shivji.

Tamasha hilo linatarajiwa kuhitimishwa Aprili 17, wiki hii, ikiaminika kuwa Taifa litanufaika kwa kupata mkusanyiko wa mawazo tofauti lakini yanayounganishw ana lengo linalofanana, ambalo ni maendeleo kwa raia wote.

Maelezo ya wasomi hao ambao walikuwa wakirejea fikra za Mwalimu Nyerere, yanawiana na kauli ya hivi karibuni ya Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo wa Kanisa Katoliki.

Pengo aliyekuwa akihubiri katika misa ya Jumatatu ya Pasaka, katika Kanisa Katoliki Sinza jijini Dar es Salaam, alionyesha kukerwa na mwenendo wa viongozi wa Afrika.

Askofu huyo alifikia hatua ya kuhoji ni serikali ngapi barani Afrika zimeua na kuwahukumu vifungo bila hatia watu wake kwa sababu tu hawana watetezi, akiweka bayana kuwa katika mazingira kama hayo ukweli hununuliwa na wenye fedha.

No comments:

Post a Comment