Kikundi cha waasi cha zamani cha SPLM, kimesema hakitahudhuria mazungumzo kuhusu kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika mapema mwakani kuhusu hali ya Sudan Kusini iwapo iendelee kuwa sehemu ya Sudan au ijitenge.
Mazungumzo hayo yamepangwa kufanyika mjini Khartoum, leo.
Waziri katika serikali ya Sudan Kusini Pagan Amum amesema chama hicho cha SPLM hakikushauriwa kuhusu mkutano huo ambao umeitishwa na Rais Omar al-Bashir.
"Tulikuwa tumekubaliana na chama tawala cha National Congress pamoja na vyama vingine husika kwamba kungeundwa kamati ya maandalizi ya mkutano huo lakini chama cha National Congress kilifumbia macho makubaliano hayo na kuandaa agenda ya mkutano huo, kuafikia siku ya kufanyika kwa mashauriano", amedai Amum.
Chama hicho cha SPLM pia kimedai kwamba chama cha National Congress kiliamua kuchagua wajumbe wa SPLM watakaoshiriki mkutano huo bila kufanya mashauriano yoyote.
Amum amedai chama cha National Congress kinajaribu kushawishi watu wa Sudan Kaskazini kupinga makubaliano ya amani ya kudumu, pamoja na kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa mwakani ambayo itatoa fursa ya watu wa Kusini kujitawala.
No comments:
Post a Comment