KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, May 26, 2010

Kesi ya maharamia yaanza Uholanzi

Kesi ya kwanza kufanyika barani Ulaya dhidi ya maharamia wa Kisomali inaanza hii leo katika mahakama ya Rotterdam huko Uholanzi.

Watu hao watano wanakabiliwa na mashtaka ya kuiteka meli moja ya mizigo katika Ghuba la Aden mwezi Januari. Wakipatikana na hatia watafungwa miaka kumi na miwili kila mmoja.

Jaribio lao lilitibuka baada ya mashua yao ya mwendo wa kasi kukamatwa na wanamaji wa Denmark. Meli hiyo ijulikanayo kama Samanyolu, ilisajiliwa huko kisiwani Antilles, Caribbean.

Uholanzi ilitoa vibali vya Jumuiya ya Ulaya kukamatwa kwa maharamia hao ambao walisafirishwa kwa ndege ya kijeshi kutoka Bahrain hadi Uholanzi ambako wamezuiliwa hadi sasa.

Mawakili wao wanasema watapinga uwezo wa mahakama ya Uholanzi kuwashtaki kwa sababu meli hiyo ilipeperusha bendera ya koloni ya Uholanzi ambayo ni huru sasa.

Hata hivyo upande wa mashtaka umeelezea nia ya kuendelea na kesi hiyo ili kutetea maslahi ya mwenye meli na mabaharia ambao walishambuliwa na kushikiliwa mateka na maharamia hao.

Maharamia katika ufuo wa pwani ya Somalia wameteka meli mia mbili katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

No comments:

Post a Comment