Mjumbe mmoja wa Umoja wa mataifa amesema majeshi ya Umoja wa Mataifa yasingeweza kuzuia ubakwaji wa zaidi ya wanawake 150 na wavulana, uliofanywa na waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,- DRC kwa sababu majeshi hayo hayakuwa yakifahamu kinachoendelea.
Zaidi ya wanawake 3,500 wamebakwa tangu kuanza kwa mwaka huu kwa mujibu wa UN
Majeshi hayo ya kulinda amani yalipita katika eneo la tukio mara mbili, lakini waliambiwa waasi walikuwa wakiweka vizuizi vya barabarani tu na sio zaidi, amesema mjumbe huyo.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki Moon amesema 'alikasirishwa' na kitendo hicho na ametuma wajumbe wawili kwenda kuchunguza.
Wanawake 200
Umoja wa Mataifa (UN) umeitisha kikao cha dharura cha Baraza la usalama, kujadili jinsi ya kukabiliana na suala hilo. Ubakaji huo ulitokea katika mji wa Luvungi na vijiji vya karibu, ikiwa ni umbali mdogo tu kutoka ilipo kambi ya jeshi la kulinda usalama la Umoja wa Mataifa, amesema mfanyakazi mmoja wa utoaji misaada na daktari raia wa nchi hiyo.
Baadhi ya taarifa zinasema waasi waliteka eneo moja na kubaka wanawake 200 na baadhi ya wavulana wadogo katika kipindi cha siku nne.
Wakinamama DRC wakijiandaa na chakula cha usiku Goma mwaka 2009
Kundi la pamoja la haki za binaadam la Umoja wa Mataifa limethibitisha tuhuma hizo za ubakaji kwa wanawake wasiopungua 154, uliofanywa na waasi wa kundi la FDLR wa Rwanda na Mai-Mai wa Kongo Kinshasa katika kijiji cha Bunangiri.
Siku 10
Hata hivyo Roger Meece, afisa wa UN mashariki mwa Kongo, amesema wakazi wa huko waliwaambia wanajeshi wa Umoja wa mataifa waliokuwa wakifanya doria kuhusu vizuizi vya barabarani, lakini hawakusema lolote kuhusu vitendo vya ubakaji. Umoja wa Mataifa uliambiwa kuhusu jambo hilo na shirika la misaada siku 10 baadaye.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Goma, Bw. Meece amesema wanavijiji huenda waliogopa kusema jambo hilo kwa kuhofia waasi hao, au kutokana na kuona aibu kutokana na unyanyapaa wa kubakwa uliopo nchini humo.
'Watoto wa vita' Yatima na watoto waliopotea katika makao Goma.
Bw. Meece amesema Umoja wa Mataifa sasa unafanya uchunguzi wa jinsi ya kurekebisha uhusiano na wakazi wa huko.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, bado linakabiliwa na ghasia zinazofanywa na waasi, licha ya kumalizika kwa vita vilivyodumu kwa miaka mitano, mwaka 2003.
Majeshi ya kulinda usalama ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakisaidia jitihada za kutokomeza kundi la waasi la FDLR, ambalo viongozi wake wanahusishwa na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994. Waasi hao wanafanya harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
No comments:
Post a Comment