KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, July 1, 2010

Kondomu Zenye 'Meno' Kwaajili ya Wabakaji Zazinduliwa Afrika Kusini


Kondomu mpya kwaajili ya wanawake zenye meno kwaajili ya kuwafundisha adabu wabakaji zimezinduliwa nchini Afrika Kusini.
Kondomu hizo zinazoitwa "Rape-aXe" zilikuwa ni ndoto ya miaka 40 ya daktari wa nchini Afrika Kusini, Dr Sonnet Ehlers ambaye wakati akiwa na umri wa miaka 20 akisomea udaktari alikutana na mwanamke aliyebakwa ambaye alikuwa akilalamika sana.

Mwanamke huyo alimuambia Ehlers "Natamani kama kungekuwa na meno huko chini, ningemfundisha adabu yule".

Ehlers alisema kuwa alimwahidi mwanamke huyo kuwa siku moja atatengeneza kitu cha kuwasaidia.

Katika kuthibitisha ahadi yake, Ehlers amezindua kondomu kwaajili ya wanawake zinazoitwa "Rape-Axe" ambazo zimeanza kutumika wakati huu wa kombe la dunia.

Kondomu hizo zina kitu kama meno kwa ndani. Mwanamke anayeivaa kondomu hiyo anapobakwa, meno katika kondomu hiyo huunasa uume kama pingu.

Kondomu hiyo inaponasa kwenye uume, huwa haitoki kirahisi na mtu anapolazimisha kuitoa ndivyo inavyozidi kuubana uume kwa meno yake.

Ni madaktari pekee ndio wanaoweza kuinasua kondomu hiyo hivyo kuwawezesha madaktari kuwagundua wabakaji kirahisi na kuwaripoti polisi.

"Inasababisha maumivu makali", Ehlers aliiambia televisheni ya CNN katika mahojiano na televisheni hiyo kuhusiana na kondomu hizo.

"Mbakaji hataweza kukojoa wala kutembea wakati inaponasa kwenye uume wake, kama atajaribu kuitoa kwa nguvu, itaubana zaidi uume wake", alisema Ehlers.

Ehlers anasambaza jumla ya kondomu 30,000 kwa wanawake nchini Afrika Kusini ili wajilinde na wabakaji wakati wa fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini humo.

Hata hivyo kondomu hizo zimekumbwa na malalamiko toka kwa watu ambao wanahofia kondomu hizo zinaweza kutumiwa vibaya na wanawake kuwakomesha wanaume.

Mwanamke mwenye hasira kwa mpenzi wake anaweza kuzitumia kondomu hizo kumuaibisha mpenzi wake.

Hatari nyingine iliyoelezwa kuhusiana na kondomu hizo ni mwanamke kushambuliwa na mwanaume mbakaji kwa hasira za maumivu atakayoyapata.

Ehlers kwa upande wake amezitetea kondomu hizo kuwa zinahitajika ili kupunguza idadi ya wanawake wanaobakwa kila siku nchini Afrika Kusini.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa matukio ya ubakaji duniani ambapo asilimia 16 ya raia wa Afrika Kusini wanaishi na virusi vya ukimwi.

No comments:

Post a Comment