KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, June 21, 2010

Mapenzi salama



TAYO

Moja ya mbinu bora na rahisi za kuzuia mimba, ni kuweka kizuizi, kwa lengo kuwa mbegu ya mwaname na ile mwanamke zisikutane. Kwa maana hiyo kifaa maalum kinaweza kuwekwa katika njia inayotumiwa na mbegu ya kiume ndio isilifikie yai la mwanamke.

Baadhi ya vifaa hivi (hasa kondom) pia vinaweza kukinga kuambukizwa virusi vya Ukimwi, na magonjwa mengine ya kuambukizana kupitia ngono.

Kuna aina kadhaa za vifaa vya kuzuia mimba. Kondom za wanaume na zile za wanawake ndio vifaa vinavyofahamika zaidi, hata hivyo kuna pia vifaa vyenginevyo viitwavyo diaphragm na caps kwa kimombo ambavyo vinaweza kutumiwa na wanawake.

Kondom za wanaume: Hivi hutengenezwa kutokana na aina maalum ya mpira uitwao latex, au plastiki nyembamba. Kondom ya mwanaume huvaliwa kwenye uume iliyosimama, tena kabla ya uume kuingizwa ukeni. Ikitumiwa kama inavyotakikana inakadiriwa kuzuia mimba kwa asilimia 98.






Kwa kawaida kondomu hupatikana kwenye vituo au kliniki za upangaji uzazi, kwenye maduka ya madawa au hata maduka ya kawaida.

Kondomu za wanawake: Halkadhalika hutengenezwa kwa mipira laini ya latex au plastiki nyembamba maalum. Huvaliwa ndani ya uke, huku sehemu iliyowazi ikichomoza nje kidogo. Kwa kawaida kondom za wanawake ni ghali, na pia utendaji kazi wake unakadiriwa kuzuia mimba kwa asilimia 95.


Aina nyenginezo na vifaa vya kuzuia mimba huwa hazipendekezwi kwa vijana lakini ni vyema kuvijua.

Kuna aina nyenginezo za vifaa vya kuzuia mimba viitwavyo diaphragms na caps. (tazama michoro) Hivi hutengenezwa kutokana na kitu kiitwacho silicone au mpira laini maalum. Vikiwekwa ukeni hutumika kama vizibo vya kuzuia mbegu za mwanamme kupenya hivyo basi haiwezi kukutana na yai la mwanamke.

Kwa kawaida caps ni ndogo kuliko diaphragms lakini kwa vile wanawake pia wana maumbo tofauti, ni sharti upate saizi utakayokutosha. Hapa ni sharti upate usaidizi wa daktari wako, au muuguzi, kuiweka.

Inapowekwa mahali pake ndani ya uke, iwe diaphragm au cap, huziba kilango cha mfuko wa uzazi hivyo basi mbegu ya mwanamme haitapatanafasi ya kupita. Ukishaonyeshwa na daktari jinsi ya kuipachika, baadae unaweza kuipachika mwenyewe kabla ya kufanya mapenzi.

Kwa matokeo bora zaidi, diaphragms na caps hutumiwa pamoja na dawa iitwayo (spermicide) ambayo huuwa mbegu za uzazi za mwaname. Hapo diaphragms au caps humpa mwanamke kinga dhidi ya mimba kwa asilimia kati ya 92 na 98.

Hata hivyo itachukua mazoezi ya muda ili kuvitumia itakikanavyo. Wakati mwengine pia hutumiwa na gel yake maalum lakini bado havina hakikisho la asilimia moja kuzuia mimba.

Faida yake nyengine ni kuwa, kwa kiasi fulani, vinaweza kukinga dhidi ya magonjwa ya zinaa na saratani ya (cervix) lango la nyumba ya uzazi.

Ikiwa wewe hutumia vifaa kama diaphragms au caps, au hata kondom, ni vyema kujipangia mapema ndio usikose akiba, ndio haitakuwa karaha kuvitafuta pale unapovihitaji.


Mbinu nyingine za kuzuia mimba

Kuna chembe chembe za kimaumbile, zinazojulikana vyema kama homornes ambazo hutumiwa kutengeneza tembe au chanzo ya kuzuia mimba.

Chembe chembe hizi kwa jina maalum progestogen yaani mchanganiyko wa oestrogen na progestogen, huingizwa mwilini mwa mwanamke kwa mpangilio na kiwango maalum ili kuzuia mimba kutungwa.
Hufanya kazi kwa namna hii:

Kwa kuzuia ovari kuangua mayai
Kwa kuzuia mbegu za mwanamme kulifikia yai (kwa kufanya majimaji ua ukeni kuwa mazito na kunata hivyo kuzuia mbegu ya mwanamme kupenya)
Kwa kulizuia yai kujipachika kwenye kiota cha nyumba ya uzazi.
Tembe mchanganyiko - huwa ni kidonge cha dawa kilichotengenezwa kwa mchanganyiko wa chembe chembe za oestrogen na progestogen. Hii huzuia mimba kwa njia zote tatu tulizozitaja hapo juu na ikitumiwa itakikanavyo, vinategemewa kuzuia mimba kwa asilimia 99.



Tembe mchanganyiko

Tembe ni rahisi kutumia - Mradi tu unakumbuka kumeza vidonge kulingana na maagizo. Wakati mwengine pia huifanya hedhi, kupungua na kupunguza pia maumivu wakati wa hedhi.

Lakini athari zinazoandamana na utumiaji wa vidonge hivyo ni pamoja na kuchafukwa na moyo, kuongezeka unzani, na athari mbaya zaidi ni iwapo itatokea hali ya kuganda kwa damu kwenye mishipa ya kupitisha damu.

Vidonge vya Progestogen pekee (POP) - Aina hii ya Tembe huitwa pia “mini pill” na huwa ina chembe chemba za progestogen pekee. Huzuia mimba kwa njia kama zile zile zinazozuia tembe za mchanganyiko, na ina utendaji kazi wa kati ya asilimia 96 na 99. Hata hivyo kama una uzani wa zaidi ya kilo 70 uwezo wake wa kuzuia mimba hupungua

Faida kuu ya kutumia vidonge hivi ni kwamba vina athari ndogo za kiafya. Lakini tatizo ni kuwa ni sharti tembe imezwe wakati ule ule kila siku , kama umechelewa basi isipitishe zaidi ya masaa matatu.

Sindano - Hii ni chanjo ya kuzuia mimba inayotengenezwa na chembe chembe hizo hizo za homoni ya progestogen. Tofauti na tembe, ambazo ni sharti kumeza moja kila siku, sindano pindi inapodungwa inakupa kinga dhidi ya mimba, kwa mda wa kati ya wiki nane hadi 12 kuambatana na aina inayotumiwa.

Hudungwa takoni, na dawa kuingizwa ndani ya mishipa ya damu na ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99.

Faida kuu ya njia hii ya sindano, ni kwamba hutakuwa na wasiwasi wa kupata mimba unapofanya ngono, kwa mda wa angalau wiki nane au 12.

Lakini pia ina athari zake - ni kwamba huenda dawa hii ikavuruga mpangilio wako wa kawaida wa kupata hedhi, au ukatoka hedhi kiwango kisicho cha kawaida cha damu, au kwa mda mrefu, au hedhi ikapotea kabisa. Pia inaweza kusababisha kuongezeka uzani.

Homoni au Vidonge vya kupachika chini ya ngozi Hapa dawa kama ile ile ya tembe au chanjo, hutengenezwa na kuwekwa kwenye kifaa cha plastic mfano wa kijiti cha kiberiti. Hupachikwa ndani ya ngozi chini ya kwapa kwa kufanyiwa upasuaji mdogo.

Hii ni njia ya mda mrefu ya kuzuia mimba. Inaaminika kuzuia mimba kwa aslimia 99 na inaweza kufanya kazi kwa mda wa hadi miaka mitatu.

Kuna aina nyenginezo za upangaji uzazi ambazo, ingawa kwa hali ya kawaida hazipendekezwi kwa vijana, si vibaya kuzijua.

Kitanzi au koili, ambacho kwa lugha ya kitaalam kinajulikana kama Intra-uterine device au IUD hutengenezwa kwa plastiki na shaba, na hupachikwa kwenye mfuko wa uzazi na daktari au muuguzi.

Vitanzi huanza kufanya kazi pindi kinapopachikwa. Hufanya kazi kwa njia mbili kuu. Kwanza, kwa kuzuia mbegu za kiume kutangamana na yai, na pili kuzuia yai kukubaliwa kujipachika ndani ya mfuko wa uzazi.



IUDs

Kitanzi au koili kinakadiriwa kuzuia mimba kwa asilimia 98 na 99. Na pindi kikitolewa asili ya uwezo wa wanamke wa kushika mimba anapofanya ngono, unarudi vilevile.

Hata hivyo moja ya matatizo ya kitanzi ni kwamba vinaweza kuifanya hedhi yako kuwa nzito (damu kutoka nyingi) na pia huenda ukapatwa na maumivu, mara nyengine inaweza kutoka mahali kilipowekwa na kusukumwa nje ya mfuko wa uzazi.

Hivyo ni vyema kumuona daktari mara kwa mara ili kama imechomoka, ipachikwe tena vyema.

Njia asilia ya mpango wa uzazi.

Njia hii inahitaji makini sana kuitumia. Kwani inafanya kazi tu ikiwa wanamke anafanya mapenzi tu wakati ule ambao kiasilia hawezi kushika mimba.

Hii inawezekana kwa kutayarisha tarakimu za siku za hedhi, na kupima hali ya joto la mwili. Njia hii inahitaji uangalifu na uzoufu mkubwa – Kwa vile ni ya kubahatisha haipendkezwi kwa vijana ambao hawako tayari kupata mtoto.

Kwa bahati mbaya watu wengi hudhani kwamba kutoa uume kutoka ukeni, pindi tu kabla ya kufikia kilele cha kumwaga manii, ni moja ya njia za kuzuia mimba.

La sivyo kwani mara nyingi mbegu za kiume hutangulia kutoka hata kabla kufikia kilele katika hali ya kufanya mapenzi. Hivyo basi hata ukitoa uume huenda umeshachelewa!

Vasectomy au Tubuligation, Hii ndiyo njia pekee ya kudumu ya kuzuia mimba.

Vasectomy ni njia ya kumfanya mwanamme asiwe na uwezo wa kutunga mimba ilhali Tubuligation ni njia ya kumfanya mwanamke asiwe na uwezo wa kushika mimba. Hii inafanyika kwa njia ya upasuaji mdogo.

Mwanamme anafanyiwa upasuaji kwa kukata vibomba vinavyopitisha mbegu za kiume kutoka kwenye makende hadi kwenye uume. Upasuaji huu kwa mwanamke unahusisha kukatwa au kuzibwa kwa vibomba vinavyopitisha mayai kutoka kwa ovari hadi kwenye mfuko wa uzazi.

Baada ya upasuaji huu, ni vigumu mwanamke au mwanamme kurudishwa tena katika hali ya mwanzo ya kuweza kuzaa, kwa hivyo njia hii inatumiwa tu kwa sababu za kimatibabu au ikiwa mhusika amefikia uamuzi wa hakika kwamba hataki tena kupata watoto (zaidi).

Kitanzi cha Intra uterine system au IUS - Hiki nacho kimetengezwa kwa plastiki, yenye muundo wa T kikiwa na chechembe za homoni ya progestogen ndani. Kinaweza kupachikwa ndani ya mfuko wa uzazi na daktari au muuguzi.

Kitakapopachikwa, progestogen pole pole huingia ndani ya mwili, na kuzuia mimba katika njia ile ile kama vinavyozuia tembe. Kinaweza kutumika kwa mda wa miaka 5, na kinakadiriwa kuzuia mimba kwa asilimia 99.

Kitanzi cha IUS ni kizuri kwa wale walio na matatizo ya maumivu wakati wa hedhi, kwa sababu kinapopachikwa (ingawa wakati wa kupachikwa huenda ukapata maumivu kidogo) baadaye husaidia kupunguza hedhi au hata kuisitisha kabisa, kutokana na homoni hizo za progestogen.

Madhara ya njia hii nayo ni kama, kuongeza uzani, kuumwa na kichwa, kutokwa na damu kusiko na mpango, na mabadiliko ya majira ya hedhi. Pia inaweza kuchopoka, hivyo itabidi kumwona muuguzi au daktari kila mwezi kuhakikisha kiko sawa.

Ni vyema kujadili juu ya aina mbalimbali za mpango wa uzazi ili kuchagua vyema. Daktari wako au muuguzi atakushauri ipasavyo.

Hata hivo kumbuka njia hizi za kuzuia mimba hutumiwa zaidi kwa minajili ya mpango wa uzazi, hivyo basi haziwezi kukukinga dhidi ya maambukiko ya virusi vya Ukimwi, au magonjwa mengine yayayosambazwa kupitia ngono.

Ni busara kutumia kondom kila unapofanya mapenzi na mtu ambaye afya yake ya uzazi huifahamu - Hakikisha pia unaufahamu vizuri jinsi ya kutumia kondom na unajua jinsi ya kufanya ngono salama kwa jumla

No comments:

Post a Comment