Mwanasheria mkuu wa Kenya amesema atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ukisema kuwa mahakama za kiislamu, "Kadhi" si halali.
Siku ya Jumatatu, majaji watatu walisema mahakama hizo zinaupendelea Uislamu zaidi ya imani nyingine, na kwamba ilikuwa kinyume na katiba kwa kuwa Kenya ni nchi isiyotawaliwa katika misingi ya kidini.
Mahakama za kiislamu zimezua ubishani mzito katika katiba mpya iliyopendekezwa nchini humo.
Mahakama za Kadhi- zilizoanzishwa wakati wa utawala wa kikoloni wa Mwingereza - aghlabu hushughulikia masuala ya ndoa na urithi kwa Waislamu wachache waishio Kenya.
Mwanasheria huyo Amos Wako amesema uamuzi huo peke yake ni kinyume na sheria na unatoa mfano mbaya.
Serikali ya Kenya akiwemo Bw Wako inaiunga mkono rasimu ya katiba mpya inayohusisha mahakama za Kadhi.
Makanisa nchini Kenya yalifikisha malalamiko yao kuhusu suala hilo mahakamani miaka sita iliyopita.
Kama sehemu ya makubaliano ya kugawana madaraka ili kumaliza mgogoro kufuatia uchaguzi wa mwezi Desemba 2007, ilikubalika kuandikwa kwa katiba mpya.
Katiba hiyo inatarajiwa kupigiwa kura ya maoni mwezi Agosti mwaka huu.
No comments:
Post a Comment