







Uhasama wa kisiasa nchini Zimbabwe umekwisha, anasema Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai huku akiongeza kwamba mambo sasa ni shwari kati yake na Rais Robert Mugabe.
Bwana Tsvangirai ametoa kauli hiyo huku akijiandaa kwenda kuomba msaada kutoka Ulaya ambako atakutana na Waziri Mkuu Gordon Brown, na Marekani ambako ataonana naye Barack Obama.
Zimbabwe inahitaji takriban dola za Marekani bilioni 45 mnamo miaka mitano ijayo ili kufufua uchumi wake ambao ulidorora kwa kiasi kikubwa kutoka na msukosuko wa kisiasa.
Ni miezi minne tangu Bwana Tsvangirai wa chama cha upinzani, MDC, kukubali kugawana madaraka na Rais Mugabe.
Mapema wiki hii, Muungano wa Ulaya ulitoa dola za Marekani milioni 11 kutumia katika mpango wa kutoa msaada wa kibinadamu nchini Zimbabwe.
Lakini nchi nyingi tajiri zimesita kutoa msaada hadi pale serikali ya muungano ya Zimbabwe itakapodhihirisha kuwepo kwa hali halisi ya kugawana madaraka, kukomeshwa kwa unyakuzi wa mashamba na kudumisha utawala wa kisheria.
No comments:
Post a Comment