KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, June 4, 2009

Kashfa yayumbisha siasa za Uingereza




Baadhi ya wabunge wameamua kujiuzulu
Shinikizo zaidi zimeendelea kumzonga waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown , huku waziri katika serikali yake akitangaza kujiuzulu kutoka baraza la mawaziri siku moja kabla ya uchaguzi wa wajumbe wa jumuiya ya ulaya.
Waziri wa shughuli za Jamii Hazel Blears anajiunga katika idadi ya maafisa kadhaa wa ngazi za juu katika serikali ya chama cha Labour wanaoondoka serikalini kwenye mabadiliko yanayotarajiwa kutangazwa hivi karibuni.

Mtikisiko umekumba siasa za Uingereza kufuatia kufichuka kwa habari kuhusu wabunge kutumia vibaya fedha za umma katika matumizi ya kibinafsi , na bungeni kiongozi wa chama cha upinzani cha Conservatives David Cameron amesema serikali sasa inaporomoka.

Pia kiongozi wa chama cha Liberal Democrats Nick Cleg amejiunga katika wito huo wa kuitisha uchaguzi ufanyike sasa hivi.

Bwana Brown amepuuzilia mbali wito huo akisema serikali yake ina kazi ya kufanya.

Siku ya jumaatano Gordon Brown aliamka kukumbana na vichwa vya habari vya kutisha magazetini.

Moja linasema 'Mtawanyiko mkubwa katika Downing Street' . Lakini kichwa hicho sio tisho kubwa ikilinganishwa na tahariri kali iliyochapishwa katika Gazeti la The Guardian, ambalo kwa kawaida hukiunga mkono chama cha Labour.

Limeandika kwamba Bwana Brown hana mpango , hana lolote la kutetea mstakabali wake na hana uungwaji mkono. Tahariri hiyo inamsihi Bwana Brown ajiuzulu wiki ijayo.

Hali ya hivi karibuni ya kutafakari katika chama cha Labour imesababishwa na uvumi kuhusu mabadiliko katika Baraza la mawaziri na nyadhifa zingine serikalini.

Jumaanne jioni habari zilifichuka kwamba waziri wa mambo ya ndani Jacqui Smith angejiuzulu baada ya kupatikana kwenye kashfa ya hivi karibuni ya kuhusu matumizi ya fedha za umma na wabunge. Mawaziri wengine wawili pia wametangaza nia ya kujiuzulu.

Jacqui Smith alikuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani. Lakini duru zasema ingawa ameamua kuondoka kama waziri atasalia kuwa mbunge hadi uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya madai yaliyomtia matatani Bi Smith ni fidia kwa gharama ya mume wake kutizama filamu ya kimapenzi.

Wakosoaji wa Gordon Brown wanasema haya yote ni ishara ya uozo ulioko serikalini.

No comments:

Post a Comment