KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, May 15, 2012

Udhamini Stars uwe changamoto ya maendeleo soka la Tanzania

Jumatano shirikisho la soka nchini (TFF) lilitiliana saini mkataba na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro kwa ajili ya udhamini wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, kwa miaka mitano. Udhamini huo, kwa mujibu wa mkataba, utagharimu dola za Marekani milioni 10, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya mkataba uliomalizika chini ya kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) ambao walianza kuidhamini Stars mwaka 2006 kwa Sh. milioni 700 kwa mwaka. Katika udhamini mpya, Stars itapatiwa basi la kisasa la kukaa watu 40, wachezaji watakaa katika hoteli za kuanzia nyota tatu zenye bwawa la kuogelea, posho za wachezaji zitaongezeka kwa zaidi ya mara tatu, timu itatafutiwa mechi nyingi za kujipima ndani na nje ya nchi, wachezaji watapatwa vifaa vya kisasa vya michezo vikiwemo viatu, jezi, suti za michezo, suti za kawaida na kadhalika. Udhamini huo utagusa pia mafunzo kwa wafanyakazi wa TFF ndani na nje ya nchi, semina na mikutano ya utawala bora pamoja na uendeshaji wa tovuti ya TFF ambayo kwa sasa ukiifungua taarifa zake nyingi utakazokutana nazo ni za zamani. Ni jambo kubwa na la kupongezwa limefanywa na TBL kwa sababu kukosekana kwa morari ya wachezaji katika kambi ya timu ya taifa ilikuwa ni moja ya matatizo makubwa. Tumewasikia wachezaji wakilalamika kichini chini, na mmojawapo, Athumani Machuppa, amewahi kuandika kilio cha wachezaji katika ukurasa wake Facebook aliposema kwamba posho ya Sh.15,000 kwa wachezaji wa taifa inashusha morari ya wachezaji kambini. Mlengwa mkubwa katika udhamini wa Stars anapaswa kuwa mchezaji mwenyewe kwa sababu yeye ndiye anayeingia uwanjani kupambana na wadhamini wanapaswa kulitazama hilo . Inakuwa jambo kwa timu kufanikiwa ikiwa timu imedhaminiwa kwa vifaa na kadhalika lakini mchezaji mwenyewe anaingia uwanjani akiwa ananung'unika kwamba kambi ya Stars inamuumiza kwa sababu hajaacha hata senti nyumbani kwake. Ndio. Ataacha kiasi gani nyumbani kama amepewa Sh. 15,000 kwa maisha ya sasa? Hauwezi kufananisha maisha ya wachezaji wa timu za taifa za Ulaya kwa mfano, ambao tayari wana mishahara mikubwa katika klabu zao hivyo posho katika timu ya taifa inaweza isiwe 'ishu' sana . Kwa soka letu changa la ridhaa, ambapo wachezaji kwenye klabu zao, wengi wanalipwa pesa ndogo ukilinganisha na ukubwa wa majina yao ama klabu wanazochezea, mazingira mazuri kwa mchezaji wa taifa ni jambo muhimu sana . Hii haimaanishi kwamba wachezaji wetu si wazalendo ambao ni lazima walipwe vinono ndio wacheze 'jihad'. Uzalendo upo, lakini nyumbani watoto wanalia njaa, kutakuwa na umakini kweli katika kudumisha uzalendo hapo? Tunawapongeza TBL kwamba wameliona hilo katika mkataba wao na TFF. Mchezaji anayelala katika hoteli ya hadhi ya juu, anayevaa kiatu kizuri, jezi yenye ubora na posho ya kuridhisha, hakika anaongezeka kujiamini akutanapo na wapinzani wenye majina makubwa uwanjani. Ni suala la kisaikolojia zaidi. Tunaamini kwamba kwa udhamini huu, wachezaji watapigania zaidi nafasi ya kuchezea Stars. Na watakaopata fursa hiyo watapambana zaidi kutafuta matokeo uwanjani, jambo ambalo ni manufaa kwa maendeleo ya soka la Tanzania , ambayo kwa sasa kila viwango vya ubora vya FIFA vinapotolewa sisi tunazidi kupiga hatua za kurudi nyuma. Wachezaji kadhaa wamewahi kutangaza kutoichezea tena taifa pengine kwa kuona kwamba hakuna anayewajali wanapojitoa kuipigania nchi yao . Beki wa Yanga, Stephano Mwasika, aliwahi kutangaza kutoichezea tena Stars baada ya kuumia wakati akiwa na timu ya taifa na kulazimika kwenda kutibiwa na klabu yake iliyomsafiri kwenda India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa goti. Kwa udhamini huu, tunatarajia kwamba, matukio kama haya hayatakuwa na nafasi. Na tunatarajia kwamba kwa kuwa ni mkataba wa taifa, hakutakuwa na mambo ya kufichana-fichana, kila kitu kitakuwa wazi. Kwamba kwamba kiasi gani kinakwenda wapi na watu wapewe nafasi ya kuhoji kama ni kweli thamani ya kitu hicho inalingana na kilichoandikwa kwenye makaratasi? Kumekuwepo na malalamiko kuhusiana wadhamini kujipa wenyewe majukumu yote ya kufanya manunuzi na kisha vifaa vinavyonunuliwa kuwa havilingani na thamani ya pesa iliyotajwa. Tunapenda kuamini alichokisema wakili wa TFF, Alex Mgongolwa, ambaye alikuwepo wakati wa maafikiano hadi kusainiwa kwa mkataba huo kwamba jukumu la manunuzi litaachwa kwa TFF, kwamba hata pesa ya kununulia basi hilo la kisasa itakabidhiwa kwa TFF na kwamba vifaa vitasambazwa na Adidas. Hivi ndivyo vilivyokuwa vilio vikubwa Stars

No comments:

Post a Comment