KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, May 15, 2012

Mawaziri wawa madalali

Kamati ya kuchunguza ubadhirifu wa mali za umma ikiwemo ardhi na majengo ya serikali iliyoundwa na Baraza la Wawakilishi (BLW), imesema imegundua kuwa baadhi ya mawaziri wa Zanzibar wamejigeuza madalali wa kuuza mali za umma kinyume na sheria. Kwa mujibu wa ripoti ya kamati hiyo iliyoogozwa na Omar Ali Shehe, mawaziri hao badala ya kutekeleza majukumu yao, wamegeuka madalali wa kutafuta wateja wa kuwauzia mali za serikali kinyume na sheria, yakiwemo majengo. Kamati hiyo imesema kwamba, uwanja wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano umeuzwa kwa mfanyabiashara maarufu Said Salum, Bakhressa, bila kufuata taratibu. Imeelezwa kwamba kiwanja hicho kilitengwa na serikali katika Mtaa wa Mtoni Zanzibar kwa lengo la kujengwa makao makuu ya wizara hiyo, lakini aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Machano Othman Said, aliamua kukiuza bila kufuata sheria ya manunuzi na uuzaji wa mali za serikali, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria. Aidha, Ripoti hiyo, imesema kwamba uwanja huo umeuzwa kwa bei poa ya Sh. milioni 200 bila ya kushirikishwa watendaji wakuu wa wizara hiyo, akiwemo Katibu Mkuu wake. “Hapa inatubidi tuseme kwamba mawaziri wa wizara badala kutekeleza majukumu yao wamegeuka madalali wa kuuza mali za umma kinyume na sheria,” imesema ripoti hiyo yenye kurasa 224. Imeeleza kwamba, baada ya kuwahoji viongozi na watu mbali mbali, kamati hiyo ya uchunguzi imegundua kuwa uwanja huo umeuzwa bila kufuata sheria ya manunuzi na uuzaji wa mali za serikali namba 9 ya mwaka 2005. Kadhalika, imeeleza kwamba kwa mujibu wa sheria hiyo, kila wizara inatakiwa kuwa na bodi ya zabuni kwa ajili ya kuuza na kununua, lakini Bakhressa aliuziwa kiwanja hicho bila ya kupitia bodi ya zabuni ya wizara hiyo. “Katika hali kama hii, bila shaka kuna harufu ya rushwa, jambo la kushangaza hata watendaji wakuu wa wizara hawajui nani haswa aliyehusika kumtafuta mteja,” imeongeza ripoti hiyo. Hata hivyo, ripoti hiyo imesema kamati baada ya kuwahoji watendaji wakuu wa wizara hiyo, walimtaja Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo, Abdalla Kombo, ndiye aliyehusika na kazi ya kumtafuta mteja na kufanikiwa kumpata mfanyabiashara huyo. “Wakati wakitoa ufafanuzi mbele ya kamati, viongozi wa wizara walisema ndugu Abdalla Kombo ndie aliyekuwa kiungo wa waziri katika kumtafuta ndugu Said Salum Bakhressa na ndiye aliupeleka mkataba wa kuuzwa kwa kiwanja hicho,” sehemu ya ripoti hiyo imesema na kuongeza kwamba utaratibu mzima wa kuuza mali ya serikali haukufuatwa. Hata hivyo, alipohojiwa na kamati hiyo kwa mujibu wa ripoti, Kombo, alisema kwamba yeye hajawahi hata siku moja kuzungumza na Kampuni ya Coastal Fast Ferries LTD inayo milikiwa na Bakhressa kuhusu kununua kiwanja hicho. Kwa upande wake, akihojiwa na kamati hiyo, Bakhressa, alisema kwamba yeye alipigiwa simu na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Machano Othman Said, na kumtaarifu kuwa kuna kiwanja kinauzwa cha wizara kama yupo tayari kukinunua. Hata hivyo, ripoti hiyo imesema kitendo cha waziri huyo kuuza ardhi kwa mtu binafsi ni kinyume na sheria kutokana na mamlaka ya kuuza ardhi kuwa chini ya Waziri wa Ardhi kwa mujibu wa kifungu cha 7 (a) cha sheria ya umiliki wa ardhi namba 12 ya mwaka 1992. Vile vile, kamati hiyo imesema uuzaji wa kiwanja hicho umefanywa kwa kuzingatia maslahi binafsi, kitendo ambacho ni kinyume na misingi ya utawala wa sheria. Kamati ilisema kuwa ilipata ushahidi kuwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi), ilitoa amri kupitia barua yenye kumbukumbu namba MFEA/PSM.30/4/05/69 ya Novemba 25 mwaka 2009, lakini wizara ilishindwa kuheshimu amri hiyo. Ripoti hiyo imeshangazwa na kitendo cha waziri kuuza uwanja huo harakaharaka siku mbili kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Hata hivyo, katika mahojiano na kamati hiyo, Waziri Machano ambaye sasa ni Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum, alisema uwanja huo waliamua kuuza ili wapate fedha za kujenga jengo jipya la wizara hiyo baada ya kupata baraka kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume. Machano alisema kutokana na jengo la sasa kukabiliwa na uchakavu, aliamua kukutana na watendaji wake na kufikia mwafaka wa kuuza kiwanja kilichokuwa kikutumiwa na Idara ya Ujenzi eneo la Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Pia, ripoti hiyo imesema kwamba viongozi wa wizara hiyo wamebainika kulidaganya Baraza la Wawakilishi baada ya kuomba kuidhinishiwa Sh. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya huku wakifahamu kiwanja tayari kimeuzwa katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2009/2010. Imeleezwa kwamba baada ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuidhinisha fedha hizo na milioni 49, badala yake zilichukuliwa na wizara na kutumika kukarabati Bohari ya Shirika la Meli Zanzibar (ZSC). Ripoti hiyo imesema pia kwamba baada ya kamati kufuatilia mkataba wa uuzaji wa uwanja huo, ilifanikiwa kupata mkataba usiokuwa na nembo ya serikali wala muhuri wa wizara, jambo ambalo ni kinyume na sheria. Imeeleza kwamba baada ya kamati kufanya uchunguzi wa kina ikiwemo kukutana na Kaimu Meneja wa Kampuni ya Fast Ferries LTD, Ahmad Saleh Karama, ilibahatika kupata mkataba wa pili wenye mihuri yote miwili, ukiwemo wa kampuni na wizara husika. Ripoti hiyo imesema baada ya kupitia mkataba huo ilibainika kuwa mkataba huo ni batili kutokana na kukosekana kwa saini ya mnunuaji baada ya mkataba kusainiwa kwa niaba yake na kaimu meneja huyo, jambo ambalo kinyume ni sheria. Kamati hiyo ya uchunguzi imeitaka serikali kuhakikisha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said na watendaji wote waliohusika kuingia mkataba huo wanawajibishwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ili liwe fundisho kwa viongozi na watendaji wengine Zanzibar. Pia ripoti hiyo imemtaka Waziri wa Miundo Mbinu Hamad Masoud na Naibu wake, Issa Haji Gavu, kuliomba radhi Baraza la Wawakilishi baada ya kubainika walitaka kupotosha ukweli juu ya uuzaji wa kiwanja hicho kinyume na sheria na kwa bei poa. Kamati hiyo imeelekeza uwanja huo urejeshwe mara moja serikalini baada ya kubainika uliuzwa kinyume na sheria pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo achukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo mali za umma

No comments:

Post a Comment