KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Friday, May 20, 2011
Sheikh Yahya Hussein afariki dunia
Sheikh Yahya Hussein
Mnajimu maarufu wa Afrika Mashariki, Sheikh Yahya Hussein amefariki dunia nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Tanzania kutokana na maradhi ya moyo.
Sheikh Yahya ambaye wakati wa uhai wake alipata umaarufu mkubwa kutokana na kutabiri matukio makubwa katika maeneo mbalimbali duniani, alizaliwa wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani, mashariki mwa Tanzania mwaka 1932.
Alipata elimu yake ya awali katika shule ya Al Hassanain jijini Dar es Salaam, kabla ya kwenda visiwani Zanzibar ambako aliendelea na masomo katika chuo cha Muslim Academy.
Baada ya kuhitimu alikwenda nchini Misri alikopata elimu ya juu zaidi katika masuala ya dini ya Kiislam katika chuo kikuu cha Al Azhar kilichoko jijini Cairo.
Sheikh Yahya Hussein baadae alirejea nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya sitini na kuanza shughuli zake za utabiri wa elimu ya nyota akiwa mtabiri wa mwanzo kabisa kueneza shughuli za utabiri wa nyota katika magazeti mbalimbali ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Mnajimu huyo, amewahi kuendesha shughuli zake katika nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.
Pamoja na elimu yake ya unajimu, vile vile Sheikh Yahya Hussein alikuwa kiongozi wa dini ambaye pia alijihusisha na uchambuzi wa masuala ya siasa kupitia utabiri hususan wakati wa uchaguzi, ingawa hakushiriki kikamilifu katika kuwania nyadhifa zozote za kisiasa.
Pia alivuma sana katika kutabiri matokeo ya mechi kubwa za soka katika michuano ya Gossage na hata timu za Simba na Yanga za Tanzania bila kusahau vifo vya watu mashuhuri kama wanasiasa na wasanii pamoja na matukio makubwa duniani.
Marehemu Yahya Hussein ameacha mjane na watoto wapatao ishirini.
KUMBU KUMBU YA MAREHEMU
Habari za Mawe
Sheikh Yahya Hussein
Nimetumia namna ya utabiri mwepesi kabisa wa namba kwani watu wengi wangeelewa kwa urahisi. Unaweza kuutumia mfumo huu wa Pembe hata mara elfu moja kwa siku kwani hakina siku inayofaa au isiyofaa.
Unaweza kufanikiwa kujua hali ya nchi au hewa au mtu mara unapopata namba inayohusika.
Kwa vile mtungaji ni mzima basi ningependa kumsaidia mtu yeyote ambaye anataka mwangaza zaidi na pia ningependa nipate maoni ya wasomaji kwa simu (+255-0744-672464) au barua ya kielektroniki sheikhyahya@raha.com ili nijue jinsi wasomaji wanavyoupokea mfumo huu wa utabiri wa ajabu.
Unaweza kutabiri kila kitu mipira, michezo na kadhalika. Ukiona nambari ya timu yako ni nzuri zaidi kuliko ya mwenzio basi utashinda. Nawaombea Mungu awabariki nyinyi na sisi sote.
Amina
Sheikh Yahya Hussein
Price: Tsh. 2000/=. USD. 1.55
ISBN 9987 638 74 0
Israili yapinga pendekezo la Rais Obama
Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israili Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepinga pendekezo la rais wa Marekani Barack Obama kuwa Jamhuri ya Palestina lazima iundwe kuzingatia mipaka iliyochorwa mwaka wa 1967.
Katika hotuba muhimu ya serikali ya Marekani, Bw Obama amesema ''makubaliano ya kubadilisha mipaka kwa haraka'' yatasaidia kuunda Palestina salama .
Lakini Bw Netanyahu amesema mipaka hiyo, ambayo ilikuwepo kabla ya vita vya 1967, katika Mashariki ya kati hayawezi kulindwa.
Bw Netanyahu amajiandaa kukutana na Bw Obama kwa mazungumzo katika Ikulu ya White House.
Takriban raia wa Israel 300,000 wanaishi katika makazi waliojenga katika ukingo wa magharibi mwa mto Jordon, ambayo yako nje ya mipaka hiyo.
Makazi hayo yamejengwa kinyume na sheria za kimataifa, japo Israel inapinga hilo.
Katika hotuba yake, ya sera za Marekani katika Mashariki ya Kati, Rais Obama amesema msingi wa mazungumzo ya amani ni kuunda Palestina mpya na yenye salama.
Bw Obama amesema, ''Marekani inaamini kuwa matokeo ya mashauriano yanapaswa kuwa nchi mbili, huku Palestina ikiwa na mipaka ya kudumu kati yake na Israel, Jordon na Misri''.
Strauss-Kahn hatimaye apewa dhamana
Dominique Strauss-Kahn
Aliyekuwa Mkuu wa IMF Dominique Strauss-Kahn
Aliyekuwa mkuu wa shirika la fedha duniani, Dominique Strauss-Kahn, amepewa dhamana na jaji katika mahakama moja mjini New York.
Hii ni baada ya kushtakiwa rasmi kwa kujaribu kumbaka mhudumu wa hoteli moja.
Awali, Strauss-Kahn alijiuzulu kutoka kwa wadhifa wake kama Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Mawakili wa Bw Strauss-Kahn walisema yeye ni mtu mwenye heshima na kwamba hawezi kutoroka.
Mawakili wake wamemwambia jaji kuwa mkuu huyo wa zamani wa shirika la fedha duniani (IMF) yuko tayari kuwekwa chini ya kifungo cha saa 24 nyumbani na pia avalie kifaa cha elektroniki kitakachochunguza mienendo yake.
Mke wa Strauss-Kahn ambaye alikuwa mahakamani wakati wa kesi hiyo, alijitolea kutoa dhamana ya dola millioni moja.
Baada ya kipindi kifupi cha mapumziko jaji alikubali dhamana hiyo, lakini pia akapendekeza kutolewa kwa bima ya dhamana yake ya dola millioni tano.
Bali na kutoa dhamana, jaji aliamuru awekewa mlinzi mmoja aliyejihami wakati wote na pia asalimishe stakabadhi zake za kusafiri.
Strauss-Kahn sasa ameshtakiwa rasmi baada ya kikao cha baraza la uchunguzi, kilichohudhuriwa na mwanamke mwenye umri wa miaka 32 anayemtuhumu.
Baraza hilo liliamua kuwa Strauss-Kahn ana kesi ya kujibu.
Mwanamke aliyemfungulia mashataka ni raia wa Guinea, Magharibi mwa Afrika.
Strauss-Kahn amekanusha mashtaka yoke dhidi yake.
Anatarajiwa kufika tena mahakamani Juni sita, ambapo atatarajiwa kusema kama anakubali mashtaka dhidi yake au la.
Ikiwa, Strauss-Kahn, mwenye umri wa miaka 62, atapatikana na hatia, atahukumiwa kifungo cha miaka 25 jela.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment