KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Wednesday, May 11, 2011
Kupunguzwa wachezaji weusi Ufaransa
Waziri wa michezo wa Ufaransa amemwondolea lawama kocha wa timu ya taifa ya soka nchini humo Laurent Blanc kuhusiana na ubaguzi wa rangi, baada ya kocha huyo kupendekeza kupunguza idadi ya wachezaji weusi katika timu ya taifa.
Laurent Blanc akiwa na wachezaji wa Ufaransa
Waziri huyo, Chantal Jouanno amesema hakuna ushahidi kwamba Blanc alivunja sheria yoyote kwa kujadili kupunguza idadi ya wachezaji weusi na wale wenye asili ya Afrika Magharibi, wanaojumuishwa katika timu za vijana za Ufaransa.
Blanc amejitetea kwamba alieleweka vibaya.
Kocha huyo pamoja na makocha wengine wa timu za vijana walikuwa wanajadili jinsi ya kuwazuia kwenda kuchezea nchi zingine wachezaji wanaokuzwa nchini Ufaransa.
Bi Jouanno amesema hatma ya mkurugenzi mkuu wa mafunzo katika timu ya taifa Francois Blaquart ambaye alisimamishwa kazi kufuatia kujitokeza kwa habari hizo itaamuliwa na shirikisho la soka la Ufaransa (FFF).
Shirikisho hilo lilitazamiwa kutoa taarifa za uchunguzi wake Jumanne alasiri.
Mapendekezo hayo yamezua tafrani katika shirikisho la soka la Ufaransa, ikiwa bado haijapita mwaka tangu Laurent Blank alipoajiriwa kujenga upya timu ya taifa, baada ya matokeo mabaya kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka uliopita nchini Afrika Kusini.
Wavuti wa taarifa za uchunguzi wa kisiri- Mediapart, ulichapisha taarifa kudai Blaquart alipendekeza kupunguzwa kisiri idadi ya wachezaji weusi na wale wenye asili ya Afrika Magharibi hadi kubakia asilimia 30 kwenye baadhi ya vituo vya kutoa mafunzo kwa vijana chipukizi, kikiwemo kituo mashuhuri cha Clairefontaine.
Ilidaiwa Blanc alikubaliana na mpango huo ili kukuza zaidi wachezaji wenye ''utamaduni na histoaria'' ya Wafaransa.
Wakati wa Kombe la dunia wachezaji wapatao tisa katika timu za nchi zingine walikuwa ambao waliwahi kuichezea timu za taifa za vijana nchini Ufaransa
Kampala ulinzi mkali
Kizza Besigye.
Serikali ya Uganda imeimarisha usalama katika mji mkuu Kampala,huku kiongozi wa upinzani akitarajiwa nchini Jumatano asubuhi.
Kizza Besigye,anatokea mjini Nairobi ambako amekuwa akipokea matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata wiki mbili zilizopita.
Serikali ya Uganda nayo inajiandaa kuwakaribisha viongozi wa nchi mbali mbali kwa sherehe ya kuapishwa ya rais Yoweri Museveni siku ya Alhamisi.
Rais Museveni ameonya wale wanaotaka kuvuruga shughuli hiyo yake kwamba watakabiliwa na sheria,rais alisema hayo akiwa nyumbani kwake magharibi mwa Uganda alipohutubia mkutano wa waandishi wa habari.
Yoweri Museveni
Museveni amesema kwa vyovyote vile hafla hiyo itaendelea, '' Nimeskia watu wengine,wanataka kusimamisha shughuli yangu,hakuna mtu atazuia hiyo shughuli labda Mungu peke yake,'' Alisema Museveni.
Aliongeza kusema kwamba kama viongozi lazima waheshimu serikali iliyochaguliwa kwa njia ya demokrasia ingawa alikiri kuwa polisi walipita mipaka wakati walipokuwa wanamkamata Kizza Besigye
PICHA - Maiti Ndani ya Nyumba ya Osama bin Laden
Picha hizi za kutisha za maiti za watu waliouliwa ndani ya nyumba ya Osama bin Laden unaweza ukaziona lakini picha za maiti ya Osama bin Laden mwenyewe hautaiona kamwe kwani rais Barack Obama wa Marekani ameishatangaza kuwa picha hizo hazitatolewa kamwe.
Picha hizi za kutisha zinaonyesha maiti za wapambe wa Osama bin Laden ambao waliuliwa wakati kikosi maalumu cha jeshi la Marekani kilipovamia nyumba ya Osama bin Laden na kumuua Osama bin Laden.
Picha hizi zilipigwa na maafisa usalama wa Pakistan ambao waliingia kwenye nyumba ya Osama bin Laden mapema asubuhi ya jumatatu baada ya Marekani kuvamia kwenye nyumba hiyo kumuua Osama bin Laden na kisha kuondoka na maiti yake.
Maafisa usalama wa Pakistan ambao hawakutaka kutaja majina yao walizipiga picha hizo na kisha kuziuza kwa gazeti la The Gurdian la Uingereza.
Shirika la habari la Reuters limethibitisha kuwa picha hizo ni za kweli na zilipigwa eneo la tukio.
Kuhusiana na picha ya maiti ya Osama bin Laden, Rais Barack Obama wa Marekani alisema kuwa picha hizo hazitaonyeshwa kamwe kwani zitasababisha mtafaruku na pia zitatumiwa na wapinzani wa Marekani kueneza propaganda za chuki.
Rais Obama alisema kuwa picha za maiti ya Osama bin Laden hazitatolwa na wala picha au video zake wakati akizikwa hazitatolewa lakini aliwahakikishia watu kuwa Osama ameuliwa kweli na kamwe hataonekana tena akitembea kwenye ardhi ya dunia hii.
Gonga linki chini kuona picha za hali ilivyokuwa ndani ya nyumba ya Osama bin Laden na picha maiti za watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo
Watu 80 wauawa Sudan Kusini
Wanjeshi wa SPLA
Watu wasiopungua themanini wameuawa katika eneo la Sudan kusini baada ya waasi kuvamia kambi za mifugo, jeshi la Sudan kusini limesema.
Wavamizi hao waliwauwa watu 34 wakiwemo wanawake na watoto, wakati walipoiba mifugo katika jimbo la Warrap, amesema msemaji wa jeshi Philip Aguer.
Lakini wakati wakitoweka na mifugo, wezi hao walishambuliwa na 48 kati yao kuuwawa.
Sudan kusini inajitenga na eneo la kaskazini mwezi Julai mwaka huu. Sudan Kusini inaishutumu Khartoum kwa kusababisha hali ya wasiwasi katika eneo hilo.
Rais wa Sudan
Madai kama hayo yamepingwa na serikali ya Rais Omar al-Bashir.
Umoja wa mataifa umesema kuwa makundi yasiyopungua saba ya wapiganaji waliojihami yanaendesha shughuli zake Sudan Kusini.
Umoja wa mataifa unakadiria kwamba zaidi ya watu 1,000 wameuawa mwaka huu katika mapigano kati ya waasi au makundi yaliyojihami na jeshi la Sudan Kusini.
Jamii nyingi za eneo la Sudan Kusini pamoja na mataifa jirani hutegemea sana mifugo kwa maisha yao
Mwenye sifa achukue fomu- UVCCM
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetangaza na kuwataka vijana wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa Taifa katika umoja huo.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Mfaume Kizigo, alitangaza hayo jana wakati alippokuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Kutangazwa na nafasi hiyo kumekuja baada ya kumtafuta mrithi wa aliyekuwa MWenyekiti ngazi hiyo, Hamad Masauni kujiuzulu kwa mujibu wa kanuni za UVCCM, Ibara ya 95.
Kizigo alisema fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo zitaanza kutolewa leo kwa gharama ya shilingi. 100,000 na mwisho ya kuchukua fomu ni Mei 20, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kizigo, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ilitoa maelekezo na ratiba ya uchaguzi huo ambapo Juni Mosi hadi 30 vikao vya mchujo ambavyo ni Sekretarieti, Kamati ya Utekelezaji na Baraza Kuu la UVCCM vitakaa na kuanzia Julai Mosi hadi 30 kutakuwa na vikao vya uteuzi vya CCM.
Alisema mgombea pia anapaswa kuwa mwanachama hai wa UVCCM na CCM anayetimiza haki, wajibu na masharti ya uachachama na awe raia wa Tanzania
Triesman adai wajumbe wa FIFA walitaka rushwa
Lord Triesman
Shirikisho la soka duniani FIFA limeahidi kufanya uchunguzi juu ya madai ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya wajumbe sita wa kamati yake kuu.
Madai hayo yalitolewa kwa ushahidi ulowasilishwa kwa kamati teule ya bunge juu ya michezo nchini Uingereza ambapo aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha soka nchini Uingereza FA David Triesman alidai kuwa wajumbe hao wa Fifa walidai rushwa kama sharti la kuipigia kura England kuwa mwandalizi wa kombe la dunia.
Lord David Triesman alitoa madai hayo mbele ya kamati ya bunge alipotakiwa kueleza kwa nini England ilishindwa kupata kura za kuandaa kombe la dunia mwaka 2018.
Lord Triesman alisema mmoja wa wajumbe alitaka apewe dola milioni nne,huku akitoa madai dhidi ya mjumbe mwengine wa Paraguay Nicolas Leoz ambaye alitaka atambuliwe kwa kupewa cheo cha hadhi na Uingereza.
Sepp Blatter
Mapema kamati hiyo ilisema kuwa itachapisha ushahidi wote kutoka kwa gazeti moja ukidai kuwa wajumbe wawili wa bara Afrika,Issa Hayatou na Jacques Anouma walilipwa dola milioni moja unusu na taifa la Qatar ili waweze kuwapigia kura wapate kuandaa michuano ya mwaka 2022.
Rais wa FIFA Sepp Blatter ametaka kamati ya bunge kuwapa ushahidi huo akisema ni baada tu ya kupokea ushahidi huo ndiyo wataweza kufanya uchunguzi.
Lakini wakati akitoa hakikisho hilo hakuwatetea moja kwa moja wajumbe hao wa kamati kuu ya FIFA akisema ni vigumu kubaini ikiwa wote walikuwa na nia njema au la.
Awataka wajivue gamba-JK
RAIS Jakaya Kikwete awataka mawaziri ambao wameshindwa kuendesha wizara hizo wajiondoe wenyewe kwenye nafasi zao kwani wananchi wamechoshwa na ubabaishaji wa utendaji kazi wao.
Hayo aliyasema jana mjini Dodoma katika semina elekezi kwa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu.
Ameyasema hayo baada ya mawaziri kuzidi kukaa kimnya kuweka wazi mambo yanayohusiana na wizara hizo na kuleta wasiwasi kwa wananchi na kupata tabu ya kuwajibia maswali .
Baadhi ya wizara zimekuwa zikipinga utekelezaji na kupinga mawazo na maamuzi ya Baraza la mawaziri na kuwataka wanaoona vigumu kuuafiki ni bora kutoka mapema.
Aliwataka mawaziri, manaibu, makatibu wanapoamua jambo kwa pamoja basi waonyeshe ushirikiano kwa pamoja na malumbano amesema ni kukiuka maadili ya uongozi na uwajibikaji wa pamoja.
Pia amekemea tabia ya mawaziri wasioeleza mafanikio ya wizara zao ni kutoitakia mema Serikali.
Amewaagiza mawaziri hao kuwa wepesi kusahihisha upotoshwaji unapotokea kwa kuwa wakikawia kutoa taarifa sahihi, wanaigharimu Serikali
Wapiganaji wa Gbagbo 'waliwachinja raia'
Ivory Coast
Watu takriban 200 wengi wao raia wameuawa na wapiganaji na mamluki wa rais aliyeondolewa madarakani Laurent Gbagbo, maafisa wamesema.
Mauaji hayo yalitokea wiki iliyopita katika jamii ya watu wanaoishi pwani wakati wapiganaji hao wakielekea mpakani mwa nchi hiyo na Liberia, idara ya Ulinzi ilisema.
Madai hayo hayajathibitiswa na vyanzo huru.
Bwana Gbagbo wiki iliyopita alikuwa anahojiwa kuhusu tuhuma ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu
Alikamatwa mwezi mmoja uliopita baada ya kutaa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa November 2010 .
Rais Alassane Ouattara aliapishwa rasmi wiki iliyopita na anajaribu kurejesha hali ya kawaida baada ya machafuko ya miezi minne ambayo inakadiriwa watu 3,000 waliuawa.
Mauzo nje ya Kakao yalirejea tena na kuifanya Ivory Coast kushika nafasi ya kwanza tena ya uuzaji wa zao hilo duniani mwishoni mwa wiki, maafisa walisema.
"Mamluki wa kulipwa na rais wa zamani Laurent Gbagbo, walitokea Liberia na wapiganaji wa Ivory Coast," Waziri wa Ulinzi alisema katika taarifa iliyosainiwa na Waziri Mkuu Guillaume Soro, ambaye pia ni waziri wa ulinzi.
"Baada ya kuondolewa walielekea kwenye makazi yao" alisema."
Baada ya kukimbia mji mkuu Abidjan, wapiganaji hao walipitia eneo la makazi ya jamii za pwani zikiwemo za Irobo, Grand Lahou, Fresco na Sassandra mahali mauaji hayo yalipotokea" ilisema taarifa hiyo.
Wengi wa waliouawa walichaguliwa kwa kufuata makabila yao au kama waliishi maeneo ambayo yanamuunga mkono Rais Ouattara" ilisema.
Awali mkuu wa kitengo cha Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast Guillaume Ngefa alisema miili 68 ya wanaume ilipatikana katika kaburi la pamoja katika eneo la Yopougon, wilaya ya mwisho ya Abidjan kuendeleza utii wake kwa rais wa zamani Gbagbo.
Walisema mauaji hayo yalifanyika siku moja tu baada ya Gbagbo kukamatwa na wanaomuunga mkono Rais Ouattara
Masalia kuchomwa kesho, wakazi watakiwa kuondoa hofu
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), linatarajia kuchoma masalia na baruti ya mabomu yaliyobaki katika kambi ya Jeshi Gongo la Mboto.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya JWTZ iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam ilisema, masalia hayo yatachomwa kwasiku mbili ambapo ni kesho na keshokutwa.
Na yataanza kuchomwa kuanzia saa 3. asubuhi hadi saa 6 mchana, katika kambi hiyo ya Gongo la Mboto.
Hivyo wananchi wametakiwa kutokuwa na hofu, kwani hakutakuwa na madhara ya aina yoyote katika zoezi hilo na kutakiwa waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa kama kawaida
Maiti yakutwa chooni, alikopa laki 4
BWANA FETO Philemon, mkazi wa Ubungo Maziwa amekutwa amekufa chooni, nyumbani kwake
Maiti hiyo ilikutwa chooni jana majira ya saa 7 mchana wakati alipoingia kwa lengo la kupata haja.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, Bw. Charles Kenyela alisema, taarifa hiyo kituoni ilipelekwa na mke wa marehemu, aliyetambulika kwa jina Jesca Andrew (33),
Kenyela amesema kuwa, mke huyo wakati anatoa taarifa hiyo alisema huenda mume wake alikuwa amekunywa sumu kwa kuwa hakukuwa na maelewano kati yao.
Alisema mke huyo alidai walikuwa na ugomvi uliosababishwa na mke kumgombeza baada ya marehemu kukopa shilingi laki nne na kuzimaliza kutumia katika starehe zake binafsi.
“Huenda alikunywa vidonge ama chochote kwa kuwa alishakopa pesa hiyo na aliitumia kinyume na malengo” mke
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala na upelelezi wa kina wa kipolisi kuhusiana na tukio hilo unaendelea
Wabara wachomewa makazi Zanzibar
IMESADIKIWA Watu wapatao 120 wenye asili ya Tanzania Bara wamekosa makazi kwa kuchomewa nyumba zao moto katika kijiji cha Pwani, Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mbali na kuchomewa makazi pia watu hao wameweza kupoteza mali zao kwa kuteketeza maduka na mali mbalimbali wakati motohuo ukiendelea
Watu wanaodaiwa kutoka kijiji hicho ndio waliosababisha moto huo kwa kuanza kumwagia mafuta ya petrol maduka hayo huku wakiwa na vifaa vya mapigano yakiwemo mapanga na marungu walipovamia eneo hilo.
Imedaiwa kuwa wakati moto huo ulipoanza watu wenye mali hizo walipokuwa katika juhudi za kuokoa mali zao walizuiliwa kwa kushikiwa mapanga wasiokoe mali hizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mselem Mtuliya alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi majira ya saa 10 jioni.
Alisema tayari watu saba wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku jeshi la polisi likiendela na uchunguzi na taratibu za kuwafikisha mahakamani watu hao zinaendelea.
WAtu hao wengi wanaodaiwa kuwa wenyeji wa Kilimanjaro walikuwa wamewekeza kijijini hapo kwa kufanya biashara kama vinyago na nyingine nyingi kuwauzia watalii na wenyeji wa eneo hilo walikuwa wakiwabughudhi na kuwataka waondoke kijijini hapo
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Zanzibar (DCI), Muhidini Juma Mshiri, aliwataka wananchi wawe watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
Nae Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, aliwataka waathirika waorodheshe thamani ya mali walizopoteza ili serikali iangalie njia za kuwasaidia.
Pia ameagiza waathirika hao wapewe eneo jipya la kuishi na amekemea suala la ubaguzi, akisema kila raia wa Tanzania ana uhuru wa kuishi sehemu yoyote nchini Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment