KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, February 18, 2011

Waathirika wa mabomu kufidiwa Tanzania

Nyumba iliyoporomoka baada ya mlipuko
Wakati wakazi wa jiji la Dar es salaam wakiendelea kutafakari juu ya milipuko ya mabomu katika kambi ya kijeshi ya Gongo la Mboto na athari zake kwa maisha ya watu na mali, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ametoa taarifa maalum kuhusu maafa hayo.

Taarifa hiyo ilijaa ahadi za serikali kuwasaidia waathirika wa milipuko hiyo pamoja na ndugu wa watu waliofariki dunia kwa kuwapatia fidia

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amelielezea tukio hilo kuwa maafa makubwa kwa taifa kutokana na watu kupoteza maisha na mali zao na pia jeshi kupoteza hazina yake ya silaha baada ya maghala 23 kuteketezwa na moto.

Serikali imetangaza kugharamia mazishi ya marehemu popote ndugu zao watakapoamua wakazikwe na baadaye ndugu hao wa marehemu watapatiwa kifuta machozi ambacho hata hivyo hikijatamkwa bayana ni kiasi gani.


Mlipuko Dar es Salaam
Rais Kikwete ambaye ametembelea eneo la tukio na kuwafariji majeruhi wa ajali hiyo katika hospitali mbalimbali za Dar es Salaam walikolazwa,
amesema serikali pia itagharamia matibabu yao na watakaporuhusiwa kutoka hospitali, nao watalipwa kifuta machozi kwa ulemavu walioupata,
ambapo baadhi yao wamepoteza viungo vya miili yao ikiwemo mikono na miguu.

Taarifa hiyo pia imeviagiza vyombo husika kuwahudumia wananchi waliopoteza makaazi yao na waliolazimika kuyakimbia kwa nia ya kuokoa maisha yao kwa kuwapatia haraka makazi ya muda na huduma za malazi, chakula, maji, afya na usafi wa mazingira.

Pia vyombo husika vimeagizwa kuzitambua mapema nyumba, wenye nyumba na kuhakikisha matayarisho na tathmini vinafanyika ili watu hao walipwe fidia inayostahili bila kuchelewa.

Ahadi kama hii ya serikali pia ilitolewa mwaka 2009 baada ya milipuko ya mabomu ya Mbagala,
lakini wengi wa waathirika walilamikia kukosa msaada huo kutokana na usimamizi mbovu,

ambapo wengi walilalamikia upendeleo katika tathmini hususan ya nyumba zilizoharibiwa na kuambulia kupata kiasi kisichokidhi ujenzi mpya wa nyumba zao.


Milipuko ya Gongo la Mboto imesababisha vifo vya watu 20 na mamia wengine kujeruhiwa, huku uharibifu mkubwa wa mali ukionekana.















No comments:

Post a Comment