KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, October 28, 2010

CCM imeua TRC, asema Lipumba



Anthony Kayanda, Kigoma

MGOMBEA urais kwa tiketi ya CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amewaeleza wakazi wa Kigoma kwamba serikali ya CCM imeliua Shirika la Reli (TRC) na sasa wamekaribisha umasikini mkubwa kwa wananchi wa mikoa ya Kigoma na Tabora, na nchi jirani za Burundi na Congo.

Akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mwananchi iliyo Kitongoji cha Mwanga, Prof Lipumba alisema kwa sasa reli ya kati iliyokuwa tegemeo kubwa la usafirishaji wa abiria na bidhaa, imebaki kuwa historia kutokana na uongozi mbovu na ufisadi.

Kigoma inategemea sana usafiri wa reni kwa ajili ya safari za abiria na mizigo kutoka mkoa huo hadi mikoa ya Kanda ya Kati na Mashariki, lakini pia inategemea usafiri wa maji kutokana na kupakana na Ziwa Tanganyika huku mipango ya usafiri wa barabara ikiwa bado haijakamilika.

Prof Lipumba alieleza kuwa katika eneo la mashariki ya Congo kuna watu zaidi ya milioni 40 ambao wana utajiri mkubwa wa madini ya aina mbalimbali, kiasi kwamba wangeweza kutumia reli ya kati na Bandari ya Kigoma kusafirisha bidhaa zao kuingia na kutoka nje ya mkoa.

‘Serikali baada ya kuona TRC imekuwa hoi na inaeleka kuzama waliamua kuwauzia wawekezaji Wahindi waliokuja eti na Kampuni ya TRL kuendesha reli ya kati, lakini kila mmoja ameshihudia inavyozidi kudidimia siku hadi siku na hivyo kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa wakazi wa mikoa ya Kigoma na Tabora wanaoitegemea reli hiyo kwa zaidi ya asilimia 95 kusafiria," alieleza Profesa Lipumba.

"Kwa nini Rais (Jakaya) Kikwete ameitelekeza reli yetu? Nipeni mimi urais niiokoe kutoka katika hali hii mbaya kwa sababu kudorora kwake kumesababisha wengi wenu muendelee kuwa masikini kwa sababu sasa hamuwezi kusafirisha bidhaa kuzipeleka katika masoko kama ilivyokuwa siku za nyuma," alisema mgombea huyo wa CUF.

Lipumba, ambaye kitaalamu ni mchumi aliyebobea, alieleza kuwa mwaka 2002 jumla ya tani milioni 1.446 za bidhaa zilisafirishwa na mwaka 2005 tani milioni 1.169 za bidhaa zilisafirishwa kwa kutumia reli hiyo.

Lakini alisema mwaka 2009 kiwango kiliporomoka zaidi na kufikia tani 237,000 za bidhaa zilizosafirishwa, ikiwa ni upungufu mkubwa kuwahi kutokea katika historia ya shirika hilo kongwe la usafirishaji nchini.

Profesa Lipumba alibainisha kuwa hali imekuwa tete hata katika usafirishaji wa abiria na kwamba mwaka 2001, watu 728,000 walitumia usafiri wa treni na ilipofika mwaka 2005 idadi ilipungua hadi kufikia watu 514,000 na takwimu zinaonyesha mwaka 2009 idadi imeporomoka na kufikia watu 285,000 tu.

"Kuporomoka huku kwa usafiri wa watu na bidhaa kumeathiri sana sekta ya ajira na mapato kwa kuwa hata kiwango cha fedha kinachokusanywa ni kidogo na kinachoshindwa kukidhi uendeshaji wa Kampuni ya TRL ndiyo maana ninaomba muichague CUF ili turekebishe hizi kasoro," alisema Profesa Lipumba

No comments:

Post a Comment