KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, August 18, 2010

Mkenya akamatwa akimuuza albino Tanzania



Jeshi la polisi huko Tanzania linamshikilia raia mmoja wa Kenya kwa tuhuma za kumsafirisha albino na kutaka kumuuza nchini humo.

Mtu huyo ambaye anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatano, alikamatwa na polisi wa Mwanza - Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, baada ya maafisa wa upelelezi kuwasiliana naye kama wateja wa viungo hivyo.

Mtu huyo alikuwa akiviuza viungo hivyo kwa kiasi cha shilingi milioni 400 za Tanzania, takriban dola 400,000 za kimarekani.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Bw Simon Sirro, amesema mtu huyo raia Kenya, Nathan Mutei mwenye umri wa miaka 28 alikamatwa Jumapili baada ya maafisa kujifanya wao ni wachimbaji madini ambao ni wateja wa viungo vya albino ambavyo mtu huyo alidai kuwa anavyo.
Raia wema

Baada ya kupewa taarifa na raia wema, na ndipo mnamo Jumapili iliyopita polisi walipoenda kwa mfanyabishara huo wakiwa na shilingi milioni 400 tayari kwa biashara hiyo ya viungo ambapo hata hivyo walikuwa wameletewa albino akiwa hai ambaye ni Bw Robinson Mukwano.



Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, tarehe 15 mwezi huu ndipo maafisa wake walipoenda kwenye eneo waliokuwa wamepanga kukutana na mfanyabiashara huyo wakiwa na kiasi cha shilingi milioni 400 na baada ya kufika eneo hilo walimkamata mtuhumiwa huyo ambaye sasa anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumsafirisha albino huyo kwa lengo la kumuuza.

Bw Robinson, alidai kuwa mtuhumiwa alikuwa akimwambia kuwa angeweza kumtafutia kazi kwenye gari kubwa aina ya lorry, na hivyo mwishowe akakubali kwenda naye Tanzania kwa ajili ya kumtafutia kazi hiyo, lakini kwa muda wote huo Mutei hakupenda kumruhusu albino huyo kuzungumza kwenye simu na watu hao waliotakiwa kumpatia kazi.


Na hatimaye Jumapili ya tarehe 15 Agosti ndipo watu kadhaa walipokuja katika hoteli walikofikia na kumkamata mtu huyo na yeye Bw Robinson kujulishwa kuwa hapakuwa na mpango wa kazi bali mpango uliokuwepo ni wa yeye kuuzwa na hatimaye kuuawa ili kukatwa viungo.
Hasira

Akizungumzia jinsi alivyojisikia baada ya kupoata taarifa ya yeye kuuzwa, alisema alishikwa na hasira ambapo alitamani kumrukia Mutei ili kumdhuru na laiti angeweza kupora bastola kwa askari polisi hao huenda angeweza kumuua yeye mwenyewe.

Hii ni mara ya kwanza polisi wa Mwanza kuzuia mpango wa biashara ya viungo vya albino ambayo mwisho wake huwa ni mauaji dhidi ya mlengwa yaani albino, ambapo kuna taarifa kuwa katika mpango huu Bw Mutei aliwauliza polisi iwapo walihitaji viungo au albino aliye hai ambapo polisi hao waliepusha mauaji kwa kutaka albino aliye hai ili wakamkatekate viungo wao wenyewe.

Zaidi ya maalbino 50 wamekwishauawa nchini Tanzania katika mauaji haya yaliyoanza takriban miaka mitatu iliyopita.

No comments:

Post a Comment