Makala
Na Venance George, Morogoro
ELIMU haina mwisho, msemo huu wa wahenga umedhihirika baada Veronica Ndalahwa Shija (56) kushangaza watu alipoamua kujiunga na masomo ya awali ya chekechea na kuwa miongoni mwa wanafunzi 83 wanaosoma katika kituo cha Chekechea cha Kihonda Mbuyuni katika Manispaa ya Morogoro.
Suala hilo limeonekana kuwashangaza wengi hasa kutokna na umri wake mkubwa na maamuzi yake ya kuamua kujiunga na kituo hicho kwa lengo la kutaka kujua kusoma na kuandika.
Kama hilo halitoshi, dhamira ya Veronica kuamua kuanza masomo ya chekechea inakwenda mbali zaidi ya hapo, ambapo anatamani siku moja awe ni miongoni mwa wanafunzi wa sekodari na mhitimu wa chuo kikuu.
“Watu wengi wamekuwa wakinicheka na kuniambia zee zima linakwenda kusoma na watoto wadogo, lakini kwavile najua nini ninachokifanya sijali wala kuona aibu kwa vile nikiona aibu siwezi kujifunza,” alisema Veronica katika mahojiano maalum .
Katika hali inayoonesha kutoona aibu, Veronica amekuwa akijichanganya katika darasa moja na watoto wanaosoma pamoja naye na ili asionekana kuwa tofauti na wanafunzi wenzake, aliamua kushona sare sawa na za wenzake.
Akielezea sababu zilizomfanya kujiunga na kituo hicho, Veronica alianza kwa kusimulia historia fupi ya maisha yake ambapo alisema kuwa mwaka 2001 aliolewa na Mayunga Makamu na kuamua kuishi pamoja mkoani Morogoro.
Alisema kuwa Novemba 16, 2006 mumewe alifariki dunia kwa ugonjwa wa Ukimwi na kumwacha mjane anayeishi na virusi vya ukimwi. Hali hiyo ilimfanya kukata tamaa ya maisha na kuamini kuwa siku moja na yeye ataiaga dunia kutokana na ugonjwa huo.
Ni jambo la kushangaza na ambalo watu wengi huenda wakashindwa kuamini lakini kwa hakika Veronica ametangaza kupona ugonjwa huo na hivyo kunyang’anywa uachama katika chama cha Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Mkoa wa Morogoro (WAVUMO).
Veronica alijiunga na WAVUMO muda mfupi baada kupimwa na kubainika kuwa na virusi vya Ukimwi. Alibainika kuwa na ugonjwa huo baada ya marehemu mumewe kumweleza hadharani kuwa yeye ni muathirika wa virusi vya Ukimwi na kwamba ameanza kutumia dawa za kienyeji kujitibu.
Alisema mumewe alifariki dunia kutokana na kuchelewa kuanza matibabu, lakini dawa hizo hizo alizokuwa akitumia mumewe ndizo alizodai kumponywa ugonjwa huo.
“Nimepima mara sita katika vituo mbalimbali vya afya na kuthibitika kuwa sina tena virusi vya ukimwi. Nililazimika kupimwa mara nyingi ili kupata uhakika, sikuwa nikiamini hapo mwanzoni, lakini kwa sasa naamini, mimepona kweli,” alisisitiza Veronica
Kero anazodai Veronica kumlazimu kuanza kujifunza kusoma na kuandika ni pamoja na kushindwa kusoma na kuandika barua. Veronica mwenye watoto tisa ambao wanaishi mkoni Mwanza, Arusha na nchini Kenya wamekuwa wakimtumia barua na kwa kuwa alikuwa hajui kusoma, alilazimika kusomewa na watu na hivyo kusababisha mambo mengi ya kifamilia kuzagaa mitaani.
“Lakini kilichonifanya nione umuhimu wa kujifunza kusoma na kuandika ni baada ya kukosa semina iliyoandaliwa kwa ajili ya wanachama nikiwa bado ni mwanachama wa WAVUMO. Mimi nilikuwa miongoni mwa wanachama 10 tuokosa kushiriki semina hiyo ambayo ilikuwa muhimu sana kwangu kutokana na madai ya kutojua kusoma na kuandika. Semina hiyo si kwa sababu ilikuwa na posho nzuri ya zaidi ya Sh 200,000 kwa kila mwanachama, lakini pia ilikuwa muhimu kwa vile ilihusu afya yangu kama muathirika wa Ukimwi,” alisema Veronica.
Watu mbalimbali wamekuwa wakimuelezea mama huyu kuwa ni mwenye mwamko wa kipekee katika masuala ya elimu, asiyeona aibu wala kukata tamaa kutokana na umri wake mkubwa kama jinsi ambavyo watoto Rahmu Rajab (6), Gift John (6) na Christina Sebastian Magova (6) wanaosoma na Veronica. Watoto hao wanasema wanasema kuwa mama huyo ni msikivu na anayewapenda sana.
Watoto hao pamoja na wenzao wamekuwa akimwita bibi kutokana na umri wake, lakini wamedai kuwa katika michezo pamoja na kuimba Veronica amekuwa hashiriki kabisa isipokuwa amekuwa akishiriki pamoja nao katika masomo ya darasani.
Veronica alisema kuwa toka kujiunga na kituo hicho Mei mwaka jana, ameanza kuona mabadiliko makubwa kwa vile sasa baadhi ya herufi anaweza kuziandika na kuzisoma vizuri. Bado mambo madogo madogo ndiyo yanayoendelea kumtatizoa, lakini anaamini ya kuwa hadi kufika mwishoni mwa mwaka huu, ataweza kusoma na kuandika kwa ufasaha zaidi.
“Nilipokwenda nyumbani watoto na ndugu zangu wengi walifurahia sana maamuzi yangu ya kujifunza kusoma na kuandika na kwa sasa ninaweza kusafiri na treni kwenda Mwanza pasipo kuelekezwa na mtu behewa ninalopaswa kupanda na kiti ninachopaswa kukaa,” alisisitiza Veronika huku akionyesha tabasamu lililoashiria kufurahia maamuzi yake.
Katika kuhakikisha kuwa lengo la kujua kusoma na kuandika linatimia na kuweza kusonga mbele kielimu, Veronica amekuwa akijaribu kuomba msaada kwa watu mbalimbali wakiwemo wapangaji wenzake katika nyumba anayoishi katika eneo la Kihonda Mbuyuni ili waweze kumwelekeza baadhi ya mambo katika kujifunza.
Akizungumzia kuhusu anavyoweza kuugawa muda wake, Veronica anasema kuwa amejipangia ratiba ambayo huizingatia ambapo majira ya asubuhi kabla na baada ya kutoka shuleni hujishughulisha na shughuli za kutafuta riziki na kutafuta kodi ya nyumba.
Kwa upande wake, mwalimu James Magai ambaye ni msimamizi mkuu wa kituo hicho, amemwelezea Veronica kuwa ni mwanamke jasiri asiyeona haya na ambaye kweli ana nia ya dhati ya kujifunza na kwamba watu wazima wasiojua kusoma na kuandika ikiwa watahitaji kujiendeleza ni lazima kujiamini na kufuta aibu wanaweza kufanikiwa kufikia ndoto zao.
“Mama huyu alipokuja kutaka kujiunga na kituo hiki nilishangaa sana, lakini baada ya kunieleza sababu za kutaka kujifunza kusoma na kuandika, niliridhika kabisa na niliona ni wajibu wangu kumsaidia tena posipo kumtoza chochote,” alisema Mwalimu Magai.
Kulingana na maelezo ya Mwalimu huyo, Veronica kwa muda mfupi sana ameweza kumudu kuandika na kusoma sirabi vizuri, lakini bado maneno ambatano yanampa shida kidogo na ni matarajio ya mwalimu huyo kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu atakuwa akisoma na kuandika vizuri zaidi.
Kituo hicho licha ya kuwa bado hakijapata usajiri rasmi kutokana na urasimu walionao baadhi ya watendaji wa mamlaka zinazohusika, kimekuwa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa Kata ya Mwembesongo katika Manispaa ya Morogoro kutokana na kuchukua idadi kubwa ya watoto ambao kama si hivyo basi wangelazimika kutembea umbali mrefu kutafuta elimu hiyo na wengine wangebaki kuzangaa mitaani.
Magai alisema kuwa kazi ya kuwafundisha watoto hao kwa ushirikiano na walimu wengine wawili wamekuwa wakiifanya kwa kujitolea zaidi hasa kutokana na kiasi kidogo cha fedha ambacho wazazi wanachangia kama ada ikilinganishwa na gharama kubwa za kiuendeshaji.
Katika suala hili serikali haina budi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na kituo hicho kwa kuhakikisha kuwa kinakuwa na sehemu maalumu ya kuendeshea mafunzo ya awali kuliko ilivyo sasa, ambapo kipo katika jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM) tawi la Kihonda, Mbuyuni.
Mbali na hatua hiyo, pia serikali ni vema ikaweka mikakati ya kuweza kuwasaidia wajane kama Veronica, ambaye kwa makusudi pasipo kujali umri wake ameamua kuanza kujifunza kusoma na kuandika
No comments:
Post a Comment