KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, July 1, 2010

Wakongo wa Uingereza wasaidia watoto


Jamii ya watu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaoishi nchini Uingereza wamezindua kampeni maalum mjini London, iitwayo Congo Unite.

Lengo ni kuchangisha fedha ili kuwasaidia watu wenye maradhi ya selimundu (sickle cell) na watoto walioachwa yatima kutokana na maafa ya vita nchini Congo.

Kampeni hiyo imeanza kwa uzinduzi wa mkanda maalum wa video na CD za wimbo maalum uitwao Congo Unite ulioimbwa kwa kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa Congo wanaoishi nchini Uingereza.

Video hizo zitauzwa duniani kote kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia mpango huo.

Kampeni hii imepewa jina la Congo Unite ikiwa ni wito kwa raia wote wa Congo duniani kusahau tofauti zao na kuungana na kushirikiana kwa pamoja katika kujaribu kusaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili raia nchini humo.

Kampeni hii imeanza kwa kulenga kuwasaidia watu wanaokabiliwa na ugonjwa wa selimundu, watoto yatima na matatizo mengine yatokanayo na maafa ya vita.

Akizungumza na BBC mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa CONGO50 ambaye pia ndiye aliyeongoza utengenezaji wa video hiyo ya Congo Unite amesema mbali na kutumia fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya CD na Video hizo kutumika kusaidia waathirika wa selimundu, wanategemea pia kuanzisha kituo cha kulelea watoto yatima nchini Congo.

Naye mratibu wa kampeni hiyo, Mimi Zabu Litambola, amesema moja ya mambo yanayotiliwa mkazo ni kukusanya fedha ili kutafsiri vitabu na maelezo kuhusu ugonjwa wa selimundu kutoka lugha ya kiingereza kwenda katika lugha zote zinazutumika nchini Congo.

Hatua hiyo itaiwezesha jamii ya Congo kupata elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huo.

Kampeni ya Congo Unite ni moja ya mipango iliyoandaliwa na raia wa Congo nchini Uingereza katika kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

No comments:

Post a Comment