Mahakama nchini Afrika Kusini imemkuta na hatia ya ufisadi aliyekuwa mkuu wa polisi Jackie Selebi.
Bw Selebi, aliyekuwa pia Rais wa idara ya polisi ya kimataifa Interpol, alishutumiwa kwa kushiriki katika uhalifu na kupokea rushwa yenye thamani ya dola za kimarekani 156,000.
Lakini mahakama ilimkuta hana hatia ya kupotosha haki. Bw Selebi alikana mashtaka yote mawili.
Waandishi wanasema kesi hiyo iliyodumu kwa miezi tisa imeonekana kuwa moja ya kesi muhimu tangu siasa za ubaguzi wa rangi kumalizika nchini humo.
Bw Selebi mwenye umri wa miaka 60 sasa anakabiliwa na hukumu ya takriban miaka 15 gerezani, japo atakuwepo nje kwa dhamana mpaka hukumu yake itakapotolewa tarehe 14-15 Julai huku akiwa nia ya kukata rufaa.
Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg, Karen Allen amesema kesi hiyo ilijaa mvuto na mchanganyiko.
Lakini mwisho wa siku, licha ya kuwa na uhusiano na wanasiasa wengi, Selebi amepatikana na hatia.
' Mikoba ya wabunifu wenye majina maarufu'
Kwenye kiini cha madai hayo ulikuwepo uhusiano wa Bw Selebi na mfanyabiashara wa dawa za kulevya aliyekutwa na hatia Glen Agliotti, ambaye pia anashutumiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara maarufu wa madini mwaka 2005, Brett Kebble.
Waendesha mashtaka wamedai Agliotti, ambaye pia alikuwa akitoa taarifa kwa polisi, amelipa hongo na kutoa zawadi kwa kamsihna wa taifa wa polisi Afrika Kusini (Saps) na badala yake Selebi asishughulike kupambana na biashara ya dawa za kulevya.
Katika ushahidi alioutoa Agliotti katika kesi hiyo mwezi Oktoba alisema, " Mtuhumiwa na mimi tulipokutana, nilifurahia kununua vitu mbalimbali naye pia alifurahi. Kwa kuwa ni rafiki yangu, nilikuwa nikiwaambia wauzaji wa maduka hayo kulipia nguo zote kupitia akaunti yangu."
Alisema wakati wa sherehe ya siku ya kuzaliwa mkewe Selebi alimnunulia mkoba wa ngozi iliyopakwa rangi ngumu inayong'aa sana ya mbunifu maarufu Louis Vitton wenye thamani ya dola za kimarekani 1300.
Mawakili wa utetezi wa Selebi wanadai kwamba mteja wao, anayejulikana kwa kuvaa suti kali, anafanyiwa ubaya na waendesha mashtaka.
Wanasema kesi hii ni sehemu ya njama iliyozingirwa na masuala ya kisiasa na madai ya kuwa karibu sana wakati wa uongozi wa aliyekuwa Rais, Thabo Mbeki.
Selebi alikuwa mshirika wa karibu na Bw Mbeki, mpinzani mkuu wa Rais aliye madarakani, Jacob Zuma.
Lakini wakati wa kutoa uamuzi siku ya Ijumaa, Jaji Meyer Joffe alitupilia mbali madai ya mawakili wa utetezi na kusema waendesha mashtaka walitoa ushahidi wa kutosha kuwa Selebi alipokea takriban randi 120,000 kutoka kwa Agliotti.
Selebi aliteuliwa na licha ya kutokuwa na uzoefu wowote wa masuala ya polisi alipokuwa mtu wa kwanza mweusi kuwa mkuu wa SAPS mwaka 2000.
Alijiuzulu kama rais wa Interpol mwaka 2008 baada ya waendesha mashtaka upande wa serikali kuthibitisha madai yanayomkabili na kusimamishwa kazi na SAPS.
No comments:
Post a Comment