KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, July 1, 2010

'Michael Jackson Asingefariki Kama Angekuwa Muislamu'


Katika kuadhimisha mwaka mmoja tangia alipofariki, kaka yake Michael Jackson, amesema kuwa anaamini kaka yake angekuwa hai hadi leo kama angebadili dini kuwa muislamu.
Akiongea na shirika la habari la Uingereza la BBC katika mahojiano ambayo yatarushwa hewani leo, kaka yake Michael Jackson, Jermaine Jackson amesema kuwa anaamini kaka yake angekuwa hai hadi leo hii kama angefanikiwa kubadili dini kuwa muislamu.

Jermaine alisema kuwa kama Michael angebadili dini kuwa muislamu basi maisha yake yangebadilika na asingekuwa na maisha ambayo yalipelekea kifo chake.

"Naamini kama Michael angekuwa muislamu, angekuwa hai hadi leo, nasema hivi kwasababu nyingi sana", alisema Jermaine ambaye yeye alibadili dini kuwa muislamu miaka mingi sana iliyopita.

"Sababu ni kwamba mtu unapokuwa muislamu na ukafahamu kwa asilimia 100 sababu ya wewe kuwepo duniani na sababu ya watu waliokuzunguka kuwepo duniani, basi maisha hubadilika na kuwa mazuri", alisema Jermaine.

Jermaine aliongeza kuwa alimnunulia Michael vitabu vingi vya kiislamu toka Saudi Arabia na Bahrain.

"Alisoma vitabu vingi vya kiislamu", alisema Jermaine na kuongeza kuwa Michael hakuwa akiupinga uislamu.

"Walinzi wake wote walikuwa waislamu kwa kuwa aliuamini Uislamu, aliwaamini kwakuwa waislamu hujaribu kuwa watu wazuri kadri wawezavyo, si kwaajili ya Michael Jackson bali kwaajili ya Mungu".

"Wakati unapozungukwa na watu kama hawa unajua kwamba Mwenyezimungu atakulinda", alimalizia kusema Jermaine.

Michael Jackson alifariki akiwa na umri wa miaka 50, juni 25 mwaka jana kutokana na shambulizi la moyo lililotokana na matumizi makubwa ya madawa ya kupunguza maumivu.

Washabiki wake wanajiandaa kuadhimisha mwaka mmoja wa kifo chake siku ya ijumaa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kukumbuka kazi zake za muziki.

No comments:

Post a Comment