KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, July 3, 2010

Mataifa matano ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yanajumuika rasmi katika ushirika mpya wa kiuchumi kwenye kanda hiyo.


Mataifa matano ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yanajumuika rasmi katika ushirika mpya wa kiuchumi kwenye kanda hiyo.

Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania na Burundi wanaunda soko la pamoja Julai mosi.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya amesema ushirika huo mpya ambao unachukuliwa kuwa hatua ya kwanza kufikia muungano wa kisiasa utachangia kuongeza mitaji, kuleta ajira na kuimarisha uhuru wa biashara na pia kufanya kazi bila kikwazo katika nchi yoyote mwanachama.

Huu ni mwendelezo uliotokana na kuwepo kwa mfumo wa umoja wa forodha ulioanza miaka mitano iliyopita ambapo baadhi ya bidhaa kutoka Kenya zinapoingia nchi wenzake wanachama zilikuwa zikitozwa ushuru ambao ulipungua kila mwaka hadi kumalizika hapo 2010.

Ilhali bidhaa kama hizo kutoka mataifa hayo ya Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi hazikutozwa ushuru zilipokuwa zikiingizwa katika soko la Kenya.

Hatua ya soko la pamoja haihusu tu bidhaa bali pia kulegezwa kwa masharti kwa usafiri wa watu na upatikanaji wa ajira na huduma katika mataifa hayo matano, jambo linaloendelea kuzua mijadala.

Mijadala mingi inaelezea hofu kuwa mataifa yaliyo na uchumi mkubwa katika jumuiya hiyo kama vile Kenya huenda yakafaidi zaidi hasa katika upatikanaji wa nafasi za kazi na fursa nyinginezo za maendeleo.

Ili kuepusha hali kama hiyo kila mwanachama alipewa fursa kuwa huru kuchagua sekta zipi za ajira zifunguliwe kwa raia wa eneo hilo na kwa wakati gani ili kukidhi mahitaji ya nchi husika.

Makubaliano hayo ni baadhi ya yaliyojadiliwa na kufikia hatua ya kutia saini mkataba huo.

Kenya ndilo taifa lililotoa fursa nyingi ikiwa ni ajira kutoka fani 96 ambao utekelezeji wake unaanza mwaka huu huku wanachama wenzake wakitoa nafasi pungufu kwa mfano Uganda 46 , Rwanda 16, Tanzania 10, Burundi 6 na baadhi zitatekelezwa kufikia 2015.

Taratibu za uvukaji mipaka japo zimeboreshwa hati za kusafiria bado ni lazima kutumika.

Kwa upande wa vibali vya kazi, yeyote kutoka nchi wanachama hana haja ya kuwa navyo akitaka kutafuta kazi nchini Kenya na Rwanda pekee.

No comments:

Post a Comment