SUALA La mahakama ya Kadhi limezua tena mijadala huku wanaharakati mbalimbali wakionekana kulivalia njuga suala hilo huku serikali ikionekana kulipiga danadana kutokana na uzito wa uanzishwaji wa mahakama hiyo nchini.
Jana Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akijibu maswali bungeni kuhusiana na mahakama hiyo alifafanua kuwa, serikali imeamua suala hilo lishughulikiwe na waislamu wenyewe ili kuepusha migongano ya kidini nchini.
Alisema serikali haitaki kujihusisha moja kwa moja katika suala hilo kwa kuwa inaheshimu kila maandiko na ibada ya kila dini nchini.
Katika suala hilo ambalo halijapatiwa muafaka kamili waislamu nchini waliazimia leo kufanya maandamano ya hiyari kushinikiza kutekelezwa kwa mahakama hiyo na jeshi la Polisi Kanda Maalum kusitisha maandamano hayo.
Katika maandamano hayo waislamu walikuwa na mikakati ya kuambiana kuhusiana na uchaguzi mkuu ujao na kuwataka waislamu wasiipigie kura CCM kwa kuwa ndio wanaosababishwa kutoanzishwa kwa mahakama hiyo nchini.
Waislamu wanadai CCM iliwadanganya mwaka 2005 katika uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Hata hivyo waislamu hao walisema kuwa hawajakata taamaa na maandamano hayo na wamesitisha na kuwasubiri wenzao wa mikoani na wataitisha tena maandamano hayo.
No comments:
Post a Comment