KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Saturday, July 3, 2010
Afrika yaomboleza kilio cha Ghana
Nafasi ya kwanza ya nusu fainali katika Kombe la Dunia kwa timu kutoka Afrika ilikuwa umbali wa sekunde kumi tu, lakini fursa hiyo iliwaponyoka Ghana, na kuwakatisha tamaa mamilioni ya mashabiki barani Afrika walioungana kuwashabikia Black Stars.
Uruguay ilikatisha ndoto ya Ghana ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufuzu nusu fainali baada ya kuwashinda Black Stars mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penali, baada ya timu zote kutoka sare 1-1 kufikia mwisho wa muda wa kawaida na pia kipindi cha ziada.
Sekunde chache kabla ya mchuano kumalizika Ghana walipata fursa ambayo ingewawezesha kujiandikishia nafasi katika nusu fainali walipopewa penalti baada ya Luis Suarez kuondosha kwa mkono mpira wa kichwa uliokuwa unaelekea kuingia kwenye lango la Uruguay, lakini Asamoah Gyan akatoa nje penalti hiyo.
Mikwaju
Ilipoingia mikwaju ya penalti mlinda lango wa Uruguay, Fernando Muslera, aliokoa mikwaju ya John Mensah na Dominic Adiyah, huku Sebastian Abreu akifunga tuta la mwisho la Uruguay na kuipa timu yake ushindi wa mabao 4-2.
Kwenye nusu fainali siku ya Jumanne, Uruguay itachuana na Uholanzi ambayo awali iliiondoa bingwa mara tano Brazil kwa kuishinda 2-1.
Ghana ilikuwa ya kwanza kufunga kabla ya mapumziko kupitia Sulley Muntari aliyepiga mpira wa mbali.
Dakika 10 baada ya kipindi cha pili kuanza Diego Forlan alipiga mpira wa adhabu hadi kwenye nyavu za lango la Ghana na kusawazisha.
Ustahimilivu wa Ghana
Ghana waliendeleza mashambulizi makali wakipania kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufuzu nusu fainali ya Kombe la Dunia lakini umiliki wao wa mpira ukawa haudumu muda wa kutosha kufanya umaliziaji unaotakiwa.
Uruguay walidhibiti mchezo katika dakika 15 za mwanzo huku Diego Forlan akitoa shuti lililopaa juu ya lango, naye mlinda lango wa Ghana, Richard Kingson akilazimika kutoa nje mpira uliopigwa na Luis Suarez.
Lakini ghafla Ghana walizinduka na kupata kona ya kwanza ambayo mlinzi Isaac Vorsa alitoa nje kwa kichwa.
Dakika chache baadaye Asamoah Gyan alipokea pasi nzuri lakini mpira wake ukapaa juu ya lango.
Ngome ya ulinzi ya Uruguay ilipata pigo wakati nahodha Diego Lugano alipojeruhiwa na kuondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Andres Scotti.
Kosakosa
Kuelekea kumalizika kwa kipindi cha kwanza, Sullay Muntari alipiga mpira wa mbali ambao kipa wa Uruguay, Fernando Muslera hakuuona.
Muda wa kawaida ulimalizika matokeo yakiwa 1-1, na mchezo ukalazimika kuingia muda wa ziada.
Nafasi ya kwanza ya kufunga katika kipindi hicho cha ziada ilipatikana na Kwadwo Asamoah lakini akaupiga nje badala ya kuchukua muda kujipanga.
Dakika chache baadaye Gyan mwenyewe alizingwa alipojaribu kuipenya ngome ya Uruguay.
Ghana walizidisha mashambulizi na muda wa ziada ukielekea kumalizika chipukizi Dominic Adiyah alipiga mpira wa kichwa ulioelekea kuingia langoni mwa Uruguay lakini Luis Suarez akauondosha kwa mikono, hatua iliyomsababisha kupata kadi nyekundu na Ghana kuzawadiwa penalti.
Hiyo ilikuwa fursa ya kuandika historia, lakini Asamoah Gyan aliyepewa nafasi hiyo ili kuongeza idadi yake ya magoli aliupiga nje mpira, mechi ikamalizika 1-1 na kuingia mikwaju ya penalti.
Gyan alifarijika kwa kufunga tuta la kwanza la Ghana naye Stephen Appiah akafunga la pili, kabla ya kipa wa Uruguay Fernando Muslera kuokoa mikwaju ya John Mensah na Dominic Adiyah.
Kilio cha Ghana ni cha Afrika, na sasa ni muda wa kwenda kujipanga upya kwa ajili ya fainali za 2014 zitakazofanyika Brazil.
This content requires Flash Player version 10 (installed version: No Flash Flayer installed, or version is pre 6.0.0)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment