KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Tuesday, June 22, 2010
'Waliompiga' risasi Nyamwaga wakamatwa
Polisi nchini Afrika Kusini imewakamata watu sita wanaohusishwa kumpiga risasi Jenerali wa zamani wa jeshi la Rwanda Kayumba Nyamwasa anayeishi uhamishoni mjini Johannesburg.
Polisi wanasema wale waliokamatwa watafikishwa mahakamani karibuni, lakini hawakusema watu hao ni wa kutoka nchi gani.
Hata hivyo inaaminiwa kuwa miongoni mwao ni raia mmoja wa Rwanda anayefahamiana na Luteni huyo.
Luteni Jenerali Nyamwasa anaendelea kupata nafuu na alitoka hospitalini siku ya Jumatatu.
Familia yake inadai kuwa hilo lilikua ni jaribio wazi la serikali ya Rwanda la kutaka kumwuua.
Serikali ya Rwanda imekansuha kabisa madai hayo.
Jenerali Nyamwasa ameomba hifadhi ya kisiasa nchini Afrika Kusini baada ya kutofautiana na Rais wa Rwanda Paul Kagame.
Kukana rasmi
Familia ya Nyamwasa ilikuwa inarejea kutoka kununua bidhaa kwenye majira ya mchana siku ya Jumamosi wakati mtu huyo mwenye silaha alipokaribia gari lake.
Bi Nyamwasa ameiambia BBC, " Mtu mwenye silaha alizungumza na dereva wangu, lakini alitaka nafasi apate kumpiga risasi mume wangu."
" Mume wangu alipoinama, akafyatua risasi. Na bahati nzuri, imempata kwenye tumbo na si kichwani... Mume wangu alitoka haraka...na akainyakua bunduki. Katika fujo kama hiyo, mtu huyo hakuweza kufyatua risasi."
Amesema Bw Kagame alitaka mume wake afe.
Amesema, " Bw Kagame amesema bungeni kwamba anataka kumwuua mume wangu, na atamfuata popote alipo na kumwuua."
Lakini serikali ya Rwanda imeiambia BBC kwamba "inauamini uwezo wa serikali ya Afrika Kusini wa kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo".
Waziri wa mambo ya nje Louise Mushikiwabo amesema katika taarifa yake, " Tumesikia taarifa hizi kupitia vyombo vya habari, hatuna uthibitisho wa tukio hili."
" Tunaitakia familia ustahamilivu na nguvu."
Ubadilishaji wa uongozi wa jeshi
Mchambuzi wetu amesema Lt Jenerali Nyamwasa alikuwa mshirika wa karibu sana wa Rais Kagame, mpaka hapo walipotofautiana.
Tangu amewasili Afrika Kusini, aliyekuwa mkuu wa jeshi amemshutumu Rais kwa kuhusika na ufisadi, madai yaliyopingwa na serikali ya Rwanda.
Amedai pia kuwa mahakama hazifuati sheria na ameiambia BBC katika mahojiano ya hivi karibuni kuwa majaji kwa sasa ni " Mali ya Rais Paul Kagame."
Miezi michache baada ya kukimbilia uhamishoni, pamoja na kiongozi mwengine mwandamizi wa jeshi, Rais Kagame alibadilisha uongozi wa jeshi kabla ya kufanyika uchaguziunaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti.
Wakati huo huo, maafisa wengine wawili waandamizi walisimamishwa kazi na kupewa kifungo cha nyumbani.
Uchaguzi huo wa rais utakuwa wa pili kufanyika tangu mauaji ya kimbari mwaka 1994, ambapo Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa kati walipouawa.
Hati za kukamatwa
Lt Jenerali Nyamwasa alikuwa kiungo muhimu katika kundi la waasi la Rwandan Patriotic Front (RPF), iliyoongozwa na Bw Kagame, iliyofanikiwa kusimamisha mauaji na ambayo iko madarakani kwa sasa.
Lakini Ufaransa na Uhispania zimetoa hati za kukamatwa dhidi ya Bw Nyamwasa kwa madai ya kuongoza mauaji hayo ya kimbari, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa RPF.
Pia amelaumiwa kwa mfululizo wa mashambulio ya guruneti mjini Kigali katika miezi ya hivi karibuni, jambo alilolikana.
Bw Kagame, ambaye yupo madarakani kwa miaka 16 iliyopita, anaonekana katika nchi nyingi za magharibi kama kiongozi mwenye uwezo mkubwa barani Afrika.
Hata hivyo wakososaji wameonyesha wasiwasi juu ya uongozi wake na serikali hivi karibuni imekuwa ikishutumiwa kuwasumbua upinzani nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi mkuu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment