Rwanda yakana
Lt Jenerali Faustine Kayumba Nyamwasa
Rwanda imesema haihusiki na kumpiga risasi aliyekuwa mkuu wa majeshi anayeishi uhamishoni nchini Afrika Kusini.
Luteni Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa, mkosoaji wa Rais wa Rwanda, yuko katika hali mbaya baada ya kupigwa risasi nje ya nyumba yake mjini Johannesburg.
Rosette Nyamwasa amesema ilikuwa ni jaribio la mauaji kwani mtu huyo mwenye silaha hakudai fedha au chochote kabla ya kumpiga risasi mume wake.
Serikali ya Rwanda imekana kuhusika na madai hayo.
Luteni Jenerali Nyamwasa alipigwa risasi tumboni na amekuwa akifanyiwa upasuaji katika hospitali moja mjini Johannesburg.
Mchambuzi wa BBC wa masuala ya Afrika Martin Plaut amesema tangu alipoondoka Kigali mwezi Februari, Luteni Jenerali Nyamwasa amekuwa kama mwiba kwa Rais Paul Kagame, ambaye anamshutumu kwa ufisadi.
Kukana rasmi
Familia ya Nyamwasa ilikuwa inarejea kutoka kununua bidhaa kwenye majira ya mchana siku ya Jumamosi wakati mtu huyo mwenye silaha alipokaribia gari lake.
Rais Paul Kagame wa Rwanda
Bi Nyamwasa ameiambia BBC, " Mtu mwenye silaha alizungumza na dereva wangu, lakini alitaka nafasi apate kumpiga risasi mume wangu."
" Mume wangu alipoinama, akafyatua risasi. Na bahati nzuri, imempata kwenye tumbo na si kichwani... Mume wangu alitoka haraka...na akainyakua bunduki. Katika fujo kama hiyo, mtu huyo hakuweza kufyatua risasi."
Amesema Bw Kagame alitaka mume wake afe.
Amesema, " Bw Kagame amesema bungeni kwamba anataka kumwuua mume wangu, na atamfuata popote alipo na kumwuua."
Lakini serikali ya Rwanda imeiambia BBC kwamba "inauamini uwezo wa serikali ya Afrika Kusini wa kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo".
Waziri wa mambo ya nje Louise Mushikiwabo amesema katika taarifa yake, " Tumesikia taarifa hizi kupitia vyombo vya habari, hatuna uthibitisho wa tukio hili."
" Tunaitakia familia ustahamilivu na nguvu."
Ubadilishaji wa uongozi wa jeshi
Askari wa Rwanda
Mchambuzi wetu amesema Lt Jenerali Nyamwasa alikuwa mshirika wa karibu sana wa Rais Kagame, mpaka hapo walipotofautiana.
Tangu amewasili Afrika Kusini, aliyekuwa mkuu wa jeshi amemshutumu Rais kwa kuhusika na ufisadi, madai yaliyopingwa na serikali ya Rwanda.
Amedai pia kuwa mahakama hazifuati sheria na ameiambia BBC katika mahojiano ya hivi karibuni kuwa majaji kwa sasa ni " Mali ya Rais Paul Kagame."
Miezi michache baada ya kukimbilia uhamishoni, pamoja na kiongozi mwengine mwandamizi wa jeshi, Rais Kagame alibadilisha uongozi wa jeshi kabla ya kufanyika uchaguziunaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti.
Wakati huo huo, maafisa wengine wawili waandamizi walisimamishwa kazi na kupewa kifungo cha nyumbani.
Uchaguzi huo wa rais utakuwa wa pili kufanyika tangu mauaji ya kimbari mwaka 1994, ambapo Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa kati walipouawa.
Hati za kukamatwa
Lt Jenerali Nyamwasa alikuwa kiungo muhimu katika kundi la waasi la Rwandan Patriotic Front (RPF), iliyoongozwa na Bw Kagame, iliyofanikiwa kusimamisha mauaji na ambayo iko madarakani kwa sasa.
Mafuvu ya vichwa vya waliouawa katika mauaji ya kimbari Rwanda
Lakini Ufaransa na Uhispania zimetoa hati za kukamatwa dhidi ya Bw Nyamwasa kwa madai ya kuongoza mauaji hayo ya kimbari, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa RPF.
Pia amelaumiwa kwa mfululizo wa mashambulio ya guruneti mjini Kigali katika miezi ya hivi karibuni, jambo alilolikana.
Bw Kagame, ambaye yupo madarakani kwa miaka 16 iliyopita, anaonekana katika nchi nyingi za magharibi kama kiongozi mwenye uwezo mkubwa barani Afrika.
Hata hivyo wakososaji wameonyesha wasiwasi juu ya uongozi wake na serikali hivi karibuni imekuwa ikishutumiwa kuwasumbua upinzani nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment