KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 3, 2010

Theluji milima Ruwenzori yayeyuka Uganda


Maafisa wa mamlaka ya wanyama pori nchini Uganda wanasema theluji juu ya milima ya Ruwenzori imeyeyuka kwa sababu ya ongezeko la joto duniani.

Kilele kiitwacho Margherita kilicho cha tatu kwa urefu barani Afrika imekuwa vigumu kukifikia kwa sababu ya mwanya mkubwa uliojitokeza.

Mkuu wa mamlaka hiyo Moses Masepa amesema huenda mwanya huo umesababishwa na ongezeko la gesi aina ya carbon hali ambayo husababisha ongezeko la joto duniani.

Amewashauri watu kupunguza shughuli ambazo zinaathiri mazingira ya milima hiyo.

Kulingana na wataalam,miaka hamsini iliyopita theluji juu ya kilele hicho ilikuwa imesambaa eneo la kilomita 50 lakini sasa theluji iliyosalia imepungua kwa kiwango kikubwa.

Mamlaka ya wanyama pori nchini Uganda imetuma wataalam juu ya milima hiyo ya Ruwenzori ili kubaini kiwango cha uharibifu katika kilele cha Margherita.

Kilele hicho ni mojawapo ya vivutio vinavyotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni UNESCO.

No comments:

Post a Comment